Na Mwandishi Maalum
Abbas Kondo Gede
na Albeto Mandes wamehukumiwa kwenda
jela miaka 22 kila moja kwa kosa la kujihusisha na usafirishaji wa dawa za
kulevya aina ya Cocaine na Heroin.
Washitakiwa hao
ambao walitenda makosa yao kwa nyakati tofauti wamehukumiwa pia kulipa faini ya
jumla ya shilingi 320.7 milioni.
Hukumu ya Abbas Kondo Gede ya kwenda jela miaka 22 na
kulipa faini ya jumla ya
shilingi 175,764,000/= imetolewa
leo ( Jumatano)
na Mhe. Jaji Korosso
baada ya kujiridhisha pasipo shaka kwamba, mshtakiwa alikuwa
na hatia ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Abbas Kondo
Gede mtanzania, na mkazi wa
mtaa wa Lindi, Wilaya ya Ilala, Mkoa
wa Dar es Salaam, na ambaye alikuwa ni
mcheza mpira wa miguu. Alikamatwa tarehe
14/5/2011 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere akitokea Sao Paulo, Brazil, kwa usafiri wa
Shirika la Ndege la Quater akiwa
na kete 77 sawa na gramu 1,171.75 za cocaine
zilizokuwa na thamani ya shilingi
58,588.000/= milioni.
Kesi ya Abbas Gede iliendeshwa na Mawakili wa Serikali Batilda Mushi na Frank Tawala ambapo
katika maelezo yao waliiomba Mahakama
kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.
Kwa upande wa
Albeto Mendes ambaye ni raia wa
Guinea Besau yeye alikamatwa tarehe 15/4/2012 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa na gram 1,277.41 za Heroine zilizokuwa na thamani ya shilingi
milioni 57,483.000/= akiwa katika
harakati za kusafiri kwenda nchini Mali.
Hukumu ya Albeto Mendes
ya kwenda jela miaka 22 na kulipa faini
ya shilingi 144,955,700/=
imetolewa leo ( jumatano) na Mhe. Jaji Mfawidhi Matogolo baada ya kujiridhisha pasipo shaka kwamba mshtakiwa
alikuwa na hatia.
Mawakili wa Serikali walioendesha kesi hiyo na kuiomba Mahakama kutoa adhabu kali
walikuwa ni Joseph Maugo ambaye
ni Wakili wa Serikali Mwandamizi na
Wakili Clara Chalwe.
Imetolewa na
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Dar es Salaam
20/9/2017
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇