LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 18, 2017

UJERUMANI YAISAIDIA TANZANIA BILIONI 521 KUIMARISHA SEKTA MBALIMBALI ZA KIUCHUMI NA KIJAMII


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango  Amina Khamis Shaaban na Naibu Mkuu wa Ushirikiano wa kiuchumi Kanda ya Afrika Mashariki kutoka Ujerumani Georg Rademacher, wakibadilishana kumbukumbu za Mkutano wa Mashauriano baada ya kusazisaini katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam, leo.
--------------------------------------------------------------


NA MWANDISHI MAALUM, DAR ES SALAAM
Ujerumani imeipatia Tanzania kiasi cha Euro milioni 198.5 sawa na Sh. Bilioni 520.86  zilizotumika kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo ya Maliasili na Mazingira, Afya, Maji, Nishati, Udhibiti wa Fedha za Umma (Good Financial Governance) na Kusaidia Huduma za Wakimbizi katika mkoa wa Kigoma, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban wakati wa tukio la Tanzania na Ujerumani kusaini kumbukumbu za Mkutano wa Mashauriano ya Kimaendeleo (Bilateral Development Consultations) ambapo Ujerumani imeonesha nia ya kuendelea kuisaidia Tanzania katika Sekta hizo kuanzia mwaka 2018 hadi 2021.

Kumbukumbu za Mashauriano hayo zimesainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban  kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Naibu Mkuu wa Idara ya Kanda ya Afrika Mashariki katika Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya Ujerumani  Bw. Georg Rademacher kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani. 

Mkutano huo ni maandalizi ya mkutano wa Majadiliano ya Kimaendeleo (Bilateral Negotiations) kati ya nchi hizi mbili unaotarajiwa kufanyika mwaka 2018 ambapo Serikali ya Ujerumani itatangaza kiasi cha fedha watakazotoa kama msaada kwa ajili ya kufadhili Sekta zilizoainishwa katika kumbukumbu zilizosainiwa.

“ Tunaishukuru Ujerumani kwa kuwa miongoni mwa washirika wa muda mrefu wanaotoa misaada mikubwa ya kimaendeleo kwa Tanzania na sisi tunaahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa faida ya pande zote mbili” alisema Bi. Amina Khamis Shaaban.

Kwa upande wake Bw. Georg Rademacher kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani amesema kwamba Tanzania imekuwa na sifa njema nchini Ujerumani hasa kwa sababu ya amani iliyopo, jinsi ambavyo imehifadhi maliasili zake na kuifanya kuwa nchi yenye vivutio vya kipekee vya utalii.

Bwana Rademacher aliongeza kwamba kwa sasa nchi ya Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika kupambana na ubadhirifu wa mali za Umma na kwamba Ujerumani itaendelea kuisaidia Tanzania ili kuweza kuleta maendeleo kwa watu wake na kuondoa umaskini.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages