Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bw. James Ihunyo (aliyesimama) akizungumza katika mkutano wa pamoja na wanachama wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mkula,iliyopo katika kijiji cha Mkula wilaya ya Kilombero.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bw. James Ihunyo (aliyesimama) akihimiza jambo wakati akizungumzia kukamatwa kwa wajumbe wa Bodi ya Skimu ya Umwagiliaji ya Mkula ambao wamezembea kusimamia mkopo wa TADB.
Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Adam Kamanda (kushoto) akiongea kwa uchungu kitendo cha wajumbe wa Bodi ya Skimu ya Umwagiliaji ya Mkula ambao wamezembea kusimamia mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 790 zilizotolewa TADB.
Baadhi ya wanachama na wanakijiji wa kijiji cha Mkula wakifuatilia mazungumzo wakati wa kikao cha pamoja kati ya Mkuu wa Wilaya hiyo, wawakilishi wa Benki ya Kilimo na wanachama wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mkula.
Baadhi ya wanakijiji wa kijiji cha Mkula wakitoa maoni yao kuhusu kutoridhishwa na kitendo cha kucheleweshwa marejesho ya mkopo wa TADB.
Zoezi la kukamata wajumbe likiendelea.
Zoezi la kukamata wajumbe likiendelea.
...................................................................................................
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Bw. James Ihunyo ameagiza kukamatwa kwa wajumbe wa bodi ya Skimu ya Umwagiliaji ya Mkula kufuatia kuchelewesha kwa makusudi malipo ya mkopo walioupata kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).
Akizungumza wakati wa mkutano wa pamoja na wanachama wa Skimu hiyo, Bw. Ihunyo alisema kuwa uzembe wa Bodi hiyo umepelekea kuchelewesha marejesho ya mkopo wa takribani shilingi milioni 790.
Mkuu huyo wa wilaya aliongeza pia kitendo cha Bodi hiyo inarudisha nyuma juhudi za serikali katika kupambana na umaskini nchini.
“Lengo la mikopo hiyo ni kuinua ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania, hivyo kuchelewesha mikopo hiyo kwa makusudi ni kurudisha nyuma juhudi hizi,” Bw. Ihunyo alisema.
Bw. Ihunyo aliongeza kuwa kuchelewesha kurudisha mikopo hiyo kunakosesha wakulima wengine kuchelewa kupata fursa hizo za mikopo hiyo nafuu inayotolewa na TADB ambayo imelenga kuchagiza na kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Adam Kamanda alisema kuwa tangu wapatiwe mkopo huo, baadhi ya wakulima wa skimu hiyo wamekuwa wakichelewesha kwa makusudi kurejesha mkopo huo licha ya jitahada za kuwahimiza kurejesha mkopo huo.
"Malengo ya Mheshimiwa Rais anahimiza watu kufanya kazi kwa bidii sasa vitendo hivi ni kukaidi maagizo hayo hivyo kupingana na dhana ya hapa kazi tu inayochagiza kufanya kazi kwa bidii,” alisema.
Bw. Kamanda aliongeza kuwa Benki ya kilimo imejipanga kuhakikisha inatekeleza maelekezo ya serikali ya kuwawezesha wakulima nchini kwa kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.
Mwakilishi huyo wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji alisema kuwa TADB imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji na utoaji wa fedha ikiwa ni pamoja sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.
“Tuna dira ya Kuwa benki ya mfano na ya kisasa katika kuleta mapinduzi ya kilimo Tanzania kutoka kilimo cha kujikimu kwenda katika kilimo cha kibiashara na uzalishaji wenye tija katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini,” alisema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇