Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi (katikati) akiwa na baadhi ya
wafanyakazi wa Taasisi hiyo kwenye banda la Tasisi hiyo, kwenye Maonyesho ya 41 ya Kimataifa ya
Biashara Dar es Salaam, leo. Kushoto ni Afisa Uhusiano wa Taasisi hiyo Anna
Nkinda. Picha:Frank Shija – MAELEZO.
----------------
NA FRANK MVUNGI- Maelezo
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi kupima afya zao hasa magonjwa ya moyo bure, katika banda lake, katika Maonyesho ya Kimataifa ya 41 ya Biashara ya Dar es Salaam yanayofanyika katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika viwanja vya maonyesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi amesema kumekuwa na muitikio mkubwa sana kwa wananchi kutembelea banda lao ambapo amesema kuwa kwa siku takribani watu 700 wanafika katika banda hilo kwa ajili ya kupata huduma na ushauri.
“Ni vizuri watanzania wakatumia fursa hii kufika hapa na watapatiwa baadhi ya vipimo na ushauri bure katika banda letu lililopo ndani ya viwanja vya sabasaba kwa kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwahudumia wananchi wake kwa kuhakikisha kuwa wanapata huduma zote za msingi zenye kiwango na ubora,” Alisisitiza Prof. Janabi
Akifafanua Prof. Janabi amesema Taasisi hiyo imedhamiria kuwahudumia wananchi wakati wote wa maonesho na hata baada ya hapo wapo tayari kuwahudumia wale wanaohitaji huduma katika taasisi hiyo.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete imekuwa ikitoa huduma za upasuaji wa moyo tangu kuanzishwa kwake hali inayosaidia kupunguza gharama zilizokuwa zinatumika kusafirisha wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu kwa kipindi kirefu sasa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇