Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo ,akikabidhiwa mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo ,alhaj Majid Mwanga ,kabla ya makabidhiano ya Mkoa huo na Morogoro ,ambapo Mwenge ukiwa Bagamoyo ulitembelea miradi 22 ya bil.129 .
Mkuu wa Mkoa Wa Morogoro ,Dkt .Kebwe Steven Kebwe ,akipokea mwenge wa Uhuru kutoka kwa mkuu wa Mkoa wa Pwani ,mhandisi Evarist Ndikilo ,makabidhiano hayo yamefanyika eneo la Bwawani mpakani mwa mikoa hiyo ,Mwenge wa Uhuru ukiwa Pwani ulitembelea miradi 81 yenye thamani ya bil. 225.1
Na Mwamvua Mwinyi ,Pwani
KIONGOZI wa mbio za mwenge kitaifa ,Amor Hamad Amor ,ameupongeza mkoa wa Pwani kwa kusheheni viwanda mbalimbali na kuiomba jamii ivitumie kwa lengo la kujikwamua kiuchumi .
Aidha amewataka wawekezaji kutoa ajira pale inapostahiki na kushiriki huduma za kijamii kwenye maeneo yao husika ili wananchi waweze kunufaika nao .
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mwenge wa uhuru kutoka Pwani kwenda mkoani Morogoro ,eneo la Bwawani ,Amor alisema wameagizwa kufanya kazi hivyo kwa mkoa wa Pwani wameiona na wamefanyakazi .
Alieleza ,mkoa huo una viwanda vya kutosha ambapo vinaendana na dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kuelekea kwenye uchumi wa viwanda .
"Tumejionea baadhi ya viwanda vinavyoendelea na ujenzi na vilivyokamilika ikiwemo cha vipodozi ,kile kinachotengeneza dawa za viuadudu vya malaria ,cha kusindika matunda cha Sayona "
"Vya kuchakata mihogo ,vya kutengeneza vigae ambavyo vyote vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuinua mapato ya halmashauri, wilaya ,mkoa na taifa " alibainisha Amor .
Amor ,hakusita kuwataka vijana na makundi yote kufanyakazi na kuachana na tabia ya kukaa kimazoea .
Alisema ni wakati wa kujiunga hata kimakundi kuanzisha viwanda vidogo na shughuli za kijasiriamali ili kujikomboa na hali ya umaskini .
Nae mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo ,akimkabidhi mwenge huo ,mkuu wa mkoa wa Morogoro dk.Kebwe Steven Kebwe ,alisema mkoa wake unatekeleza ukuaji wa sekta ya viwanda na uwekezaji .
Mhandisi Ndikilo ,alieleza ,mkoa huo umejipanga kuwa ukanda wa viwanda kwani kitaifa kuna viwanda vikubwa 304 huku kimkoa vikiwa 84 na vilivobakia ndio mikoa mingine .
"Mkoa huu unatekeleza kwa vitendo ujumbe wa mwenge “Shiriki kukuza uchumi wa Viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu” ambapo kwa sasa una viwanda 264"
"Kati ya hivyo viwanda vikubwa ni 84 na vidogo 186 na kila Halmashauri imetenga maeneo kwa ajaili ya uwekezaji na kuna mazingira mazuri kwa wawekezaji,” alisema mhandisi Ndikilo.
Mhandisi Ndikilo ,alipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Dar es salaam ,June mosi ambapo umetembea halmashauri Tisa, miradi 81 yenye thamani ya sh.bil 225.1.
Kati ya miradi hiyo ,27 itawekewa mawe ya msingi, na miradi 27 itazinduliwa na minne itafunguliwa na miradi 25 itakaguliwa.
Alifafanua ,miradi hiyo yote imechangiwa kwa pamoja na wananchi, serikali kuu, Halmashauri na wahisani wa ndani na nje .
Awali mkuu wa mkoa wa Pwani alikabidhiwa mwenge huo kutoka wilaya ya Bagamoyo, ambako Mkuu wa wilaya hiyo ,alhaj Majid Mwanga ,alisema kumetembelewa miradi 22 iliyogharimu sh.Bilioni 129 ..
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇