Kila ifikapo Mei 3 ya kila mwaka wanahabari na wadau wa vyombo vya habari ulimwenguni huadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani. Maadhimisho ya mwaka huu (2017) kitaifa nchini Tanzania yalifanyika mkoani Mwanza na kushirikisha wanataaluma ya habari na wadau anuai wa vyombo vya habari.
Miongoni mwa hoja zilizoteka mijadala katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani kwa mwaka 2017 jijini Mwanza ni suala zima la usalama wa wanahabari wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao pamoja na uwepo wa mafunzo anuai ya mara kwa mara kwa wanahabari kuwanoa zaidi.
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), ni miongoni mwa taasisi wadau waliofanikisha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani mwaka 2017 kitaifa yaliofanyika mkoani Mwanza. Bi. Valerie Msoka ni Mwanachama wa TAMWA, akizungumza katika maadhimisho ya mwaka huu kuwasilisha ujumbe wa chama hicho kwa wadau wa habari.
Anasema TAMWA imejitahidi katika kuwanoa wanahabari ili kuhakikisha wanabobea kwenye maeneo mbalimbali ya uandishi wa habari huku lengo likiwa kuwajengea uwezo zaidi. Bi. Msoka ambaye pia aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA hapo nyuma kabla ya uongoziwa wa Mkurugenzi wa sasa wa chama hicho, Edda Sanga anabainisha wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia weledi na ubobezi wa wanahabari hasa katika uandishi wa habari za ukatili kwa jamii.
Anasema tamwa katika mpango mkakati wake wa kuelimisha jamii kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto kwa kipindi cha mwaka 2015 na 2016 imeelimisha idadi kubwa ya wanahabari kwenye ubobezi wa uandishi wa habari za ukatili wa kijinsia eneo ambalo limekuwa likionekana kupwaya kiuandishi.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini zaidi ya wanahabari 2350 na wahariri 120 walijengewa uwezo wa jinsia ya kuandika habari za ukatili wa kijinsia zenye kuleta mabadiliko katika jamii ambapo kwa sasa vitendo hivyo vinatolewa taarifa kwa usahihi ukilinganisha na awali.
Anasema waandishi hao baada ya kupata mafunzo hayo wamekuwa wakitumia ujuzi huo kuandika na kuibua habari za vitendo vya ukatili wa kijinsia jambo ambalo limesaidia baadhi ya maeneo mamlaka husika kuchukua hatua juu ya vitendo hivyo, hali ambayo imekuwa ikisaidia kupungua kiasi fulani kwa vitendo hivyo kwenye jamii ukilinganisha na hapo awali.
Aidha Bi. Msoka anaongeza kuwa utaratibu huo wa kuwajengea uwezo wanahabari umekuwa ukifanywa mikoa mbalimbali huku ukijumuisha wanahabari kuandaliwa kimafunzo katika semina kadhaa na baadaye kufuatiliwa kwenye utendaji ili kubaini mabadiliko kimafanikio kabla ya mafunzo na baada ya mafunzo waliyopata. Wananchi kwa upande mmoja nao wamekuwa wakihamasika na kutumia vyombo vya habari katika kuibua matukio hayo ya kikatili, jambo ambalo limeanza kuleta mafanikio kiasi fulani.
Bi. Msoka anaendelea kubainisha kuwa TAMWA katika kutekeleza mradi wake wa GEWE II kimeweza kuunda kamati za kuelimisha jamii jinsi ya kushughulikia vitendo vya ukatili wa kijinsia katika wilaya kumi za Tanzania Bara na Tanzania Visiwani, ambazo zinawahusisha wanahabari ili kuwezesha jamii kushirikiana na vyombo vya habari kuweza kuvitolea taarifa vitendo hivyo bila woga. Anaeleza kuwa kwa kisi kikubwa kamati hizo zimesaidia kuibua matukio hayo kwa kiasi kikubwa kwa vyombo vya habari.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika-Tanzania, Salome Kitomari akizungumza kwenye kongamano la maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari 2017 linalofanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
Pamoja na hayo Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania kinaamini kuwa kupitia maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ya mwaka huu (2017) wanahabari kwa kutumia changamoto zilizoibuka dhidi yao, katika kujitathmini, watafanya kazi zao kwa weledi na uaminifu ikiwa ni pamoja habari zenye usawa wa pande zote husika.
Hii ni pamoja kujitahidi wanatasnia hiyo kuibua mambo yanayoweza kukwamisha jitihada za maendeleo ili yafanyiwe kazi, pia kujiepusha na habari ambazo kwa sehemu zinaweza kuleta machafuko na kuhatarisha maisha yao wenyewe au wananchi katika taifa la Tanzania.
Kama hiyo haitoshi TAMWA, imeendelea kuwanoa wanahabari katika nyanja nyingine za kimafunzo. TAMWA ilijiunga katika mapambano ya ajali za barabarani kwa kutoa mafunzo kwa wanahabari mbalimbali. Katika ufafanuzi juu ya hatua hiyo inabainisha kuwa ajali za barabarani zimekuwa zikiwaathiri wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Eda Sanga anasema katika moja ya mafunzo kwa wanahbari kuwa wana kila sababu ya kuingia katika mapambano ya ajali nchini kwa kuwa zimekuwa zikiwaathiri wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa.
Anasema licha ya ajali nyingi kupoteza maisha ya wanaume na kujeruhi wengine kundi hilo limekuwa likiwaacha wake zao na watoto pasipo na msaada kwa kuwa wengi humtegemea baba kama mtafutaji katika familia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇