LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 7, 2017

MABODI: DHANA YA UMOJA WA KITAIFA ZANZIBAR ILIASISIWA NA HAYATI KARUME

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema dhana ya kuanzishwa kwa fikra ya Umoja wa Kitaifa ilianzia kwa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Zanzibar  Marehemu Mzee Abeid Aman Karume, na sio ajenda ya vyama vya upinzani.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar Dk. Abdallah Juma Abdallah “Mabod”  wakati akizungumzia historia ya maisha ya Mwasisi wa ASP ambayo ni CCM kwa sasa Marehemu Mzee Karume huko Afisini kwake Kisiwandui Unguja.

Amesema  Mwasisi huyo alikuwa ni kiongozi anayepinga utengano na ubaguzi misingi ya kidini, kikabila na kisiasa ndio maana katika Baraza la mwanzo la Mawaziri kupitia Baraza la Wawakilishi la Wakati huo aliteuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani ili kujenga Umoja wa kitaifa na kuondosha ubaguzi.

Aidha alisema kuwa viongozi walioteuliwa kutoka vyama vya upinzani walikuwa ni waadilifu waliofuata miongozo na matakwa ya serikali kwa wakati huo licha ya kujitokeza kwa vitendo vya usaliti kwa viongozi hao.
“ Mzee karume alikuwa na moyo wa huruma na akiwapenda wananchi wa visiwa vya Zanzibar wawe na maendeleo endelevu.”, alisema Dkt. Mabodi.

Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa lengo la kufanyika kwa Mapinduzi ya Mwaka 1964, lilikuwa ni kurejesha heshima ya wazawa waliotawaliwa kimabavu na utawala wa Kisultani kwa zaidi ya miaka 100.

Alisema baada ya mapinduzi hayo Marehemu Mzee Karume na Jopo lake la Umoja wa Vijana wa ASP, waliweka mipango mikakati ya kuimarisha maendeleo ya Zanzibar.

Pia aliweka vipaumbe mbali mbali vikiwemo kuanziasha mpango wa kuboresha Sekta ya Elimu na Afya kwa kuwapeleka vijana mbali mbali nje ya nchi ikiwemo China, Urusi, Cuba na mataifa mengine ili wapate utalamu wa fani tofauti zikiwemo Udaktari na masuala ya  Uongozi  ili  kuharakisha maendeleo ya nchi.

Hata hivyo aliweka mfumo wa Elimu bure ili Watoto wa Kiafrika waliokuwa hawana fursa ya kusoma wakati huo wajifunze na kuelimika ili waweze kusaidia katika masuala mbali mbali ya kiutendaji.

Dkt. Mabodi alisema kuwa Mzee Karume alikuwa ni kiongozi jasiri na asiyetaka kukaa Ofisini bali alikuwa akitembea maeneo mbali mbali na kujionea mwenyewe changamoto zinazowakabili wananchi, tofauti na baadhi ya viongozi wa sasa wanaosubiri taarifa za utekelezaji ofisini.

 Hata hivyo alisema Mzee Abeid Amani katika Harakati za kupinga ubaguzi ambao ulikuwa umejenga ngome, enzi za utawala wa kifalme aliwatangazia wananchi kuwa wanatakiwa kuoana makabila mbali mbali ili kuchanganya rangi kwa lengo la kufuta ubaguzi uliokuwa kukisambazwa na watu waliokuwa ni miongoni mwa Waliopinduliwa.

Aidha alisema Mzee Karume pamoja na mambo mema aliyoyafanya enzi za uhai wake pia ni mwasisi wa kwanza wa Demokrasia kwani aliwakaribisha mataifa mbali mbali kuja Zanzibar kuwekeza na kushauri masuala ya Kisiasa.

Aliimarisha miundombinu ya barabara na kujenga nyumba za kisasa ambazo hivi sasa zinajulikana kama nyumba za maendeleo Unguja na Pemba.

Pia aliimarisha Sekta ya Mawasiliano kwa kuanzisha Televisheni ya mwanzo ya rangi Afrika Mashariki na kati iliyoitwa TVZ ambayo kwa sasa ni ZBC TV, sambamba na radio ya kisasa ya Sauti ya Tanzania Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu huyo aliweka wazi kuwa kiongozi huyo ametenda mengi mazuri kwa nchi ya Zanzibar, hivyo viongozi na watendaji wa sasa waendeleze mambo mema yaliyoachwa huku nao wakibuni vitu vingine vipya vinavyoendana na wakati uliopo sasa.

Pia alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kufanyia kazi kwa vitendo kauli mbiu ya “ Zanzibar kujitawala yenyewe kielimu, kiafya na kimiundombinu ya kisasa” huku ikipiga vita adui ujinga na maradhi.

Pamoja na hayo alimpongeza pia Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa msimamo wake wa kulinda Muungano wa Serikali mbili na Mapinduzi ya Zanzibar mambo ambyo ndio urithi wa Waasisi wa ASP na TANU wakiwemo  Marehemu Mzee Karume na Hayati Mwl. Nyerere.

Pamoja na hayo aliwambia wananchi kuwa kila ifikapo  April 7 ya kila mwaka ni maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya mashujaa wa Zanzibar na waasisi wote waliofariki , na sio sherehe ndio maana panafanyika hitima na kuombwa dua kwa lengo la kuenzi juhudi zao.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages