NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi. Waride Bakari Jabu amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kero za muungano ambapo kwa sasa zimebakia Tatu kati ya 15, zilizokuwa zikiukabili muungano huo.
Akizungumza huko Afisini Kwake CCM Afisi Kuu Kisiwandui Zanzibar, alisema juhudi hizo zinatakiwa kupongezwa kwani haikuwa kazi rahisi kufikia kiwango hicho cha ufumbuzi wa kero hizo zilizokuwa zikitumiwa na wapinzani kujenga ajenda za kuhatarisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alieleza kwamba pamoja na kuwepo na changamoto mbali mbali za vikwazo na kauli zisizofaa kutoka kwa baadhi ya wanasiasa waliodhani kuwa kero hizo haziwezi kutatuliwa, ambapo Kamati ya pamoja ya kushughulikia kero na masuala ya muungano yenye wajumbe kutoka Serikali zote mbili chini ya Makamo wa Rais , Samia Suluhu Hassan ipo katika hatua za mwisho za kutatua kero zilizobaki kwa lengo la kuimarisha mfumo huo wa kiutawala.
Bi. Waride alisema Ufumbuzi wa kero 12 kati ya 15 ni kielelezo tosha cha kuonyesha Dunia kwamba Chini ya Utawala wa Serikali zinazotokana na CCM, hakuna kisichowezekana katika utekelezaji wa mambo yanayogusa maisha ya wananchi wa Pande zote mbili za mfumo huo.
Katibu huyo akizungumzia changamoto na mafanikio kadhaa za muungano ambao leo unatimiza miaka 53 toka kuzaliwa kwake, alisema hakuna jambo lolote zuri linaloweza kukosa kasoro ndogo ndogo na muundo wa muungano uko hivyo ambapo kwa sasa Mamlaka husika zinajadiliana usiku na mchana kumaliza kasoro hizo.
Alisema kero ambazo bado zinazungumzwa ni pamoja na ya vyombo vya usafiri wa moto kutoa huduma ya usafiri au kutumika pande zote mbili.
Kero ambayo aliitaja kuwa inajadiliwa kutokana na kuhitajika matakwa ya Kikatiba kwa kutungwa kwa sheria mpya ya usafiri barabarani , ambapo hivi sasa mchakato wa kutunga sheria unaendelea na tayari waraka upo umashaandaliwa.
Alifafanua kwamba kero nyingine ni suala la Hisa za Zanzibar za iliyokuwa Bodi ya Sarafu ya Afrika mashariki, ambayo Zanzibar alikuwa ni Mjumbe wake mpaka ilipokufa, hisa zake zilihamishiwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na akafafanua kwamba kwa mujibu wa maelekezo ya Kamati inayoshughulikia masuala ya muungano wameeleza kuwa zipo nyaraka zinazoonyesha suala hilo, na wakati wowote linapatiwa ufumbuzi wake.
Hata hivyo aliitaja Kero ya tatu ambayo ni ya mwisho kuwa ni kuanzishwa kwa akaunti ya pamoja ili kuangalia fedha za mapato zinazoingia kupitia Benki Kuu ya Tanzania ambazo haziingii kupitia Benki ya Watu wa Zanzibar.
Alisema Mazungumzo yanafanyika ili kuwepo mgawo wa mapato ya fedha za akaunti hiyo na namna gani itafanyika kuhusu kuchania muungano na ripoti yake itatolewa wakati wowote mwaka huu.
Alieleza kwamba kwa kuwa bado mazungumzo hayo yapo chini ya utekelezaji wa Kamati maalum iliyopewa mamlaka kisheria kufanikisha suala hilo, basi wananchi waendelee kuwa na matarajio makubwa ya kumalizika kwa kero hizo katika hali ya amani.
Alisema Waasisi wa muungano huo wa serikali mbili ambao ni Mwl. Juliusi Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume walifunga rasmi mkataba wa muungano April 22, 1964 .
Mkataba huo ilithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi April 26,1964 na April 27,1964 viongozi hao walikutana katika ukumbi wa Karimjee , Jijini Dar es saalam kubadilishana Hati za Muungano.
Sheria za Muungano kwa wakati huo ilitamka kwamba, Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zililazimika, kuwa Dola ya Jamhuri kwa jina la jamhuri ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar , jina ambalo lilibadilishwa Octobar 28, 1964 na kuwa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia sheria ya jamhuri ya muungano , sheria namba 61, ya mwaka 1964.
Alisema faida kubwa zilizopatikana kwa kipindi cha miaka 53 ya muungano ni kuimarika kwa sekta za Ulinzi, Elimu, fursa za kiuchumi na kibiashara, miundombinu ya majini nchi kavu na Anga pamoja na ustawi wa kijamii.
Pia alisisitiza kwamba mambo hayo yameimarika kutokana na juhudi za Chama na serikali kuwa waumini wa kueneza siasa na sera zinazohimiza kusimamia Amani na Utulivu wa nchi ili zanzibar na Tanzania bara ziwe sehemu tulivu na yenye amani ya kudumu.
Alitoa wito kwa wananchi wa visiwa vya Zanzibar na Tanzania bara bila ya kujali itikadi zao za kisiasa na kiimani kuendelea kuwa wamoja katika mambo yanayohusu maslahi ya nchi, na waepuke kutumiwa na kushwa kauli na ajenda dhaifu za kusababisha vurugu na migogoro isiyo ya lazima katika jamii.
Aidha alieleza kwamba Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar , kitaendelea kulinda na kutetea kwa vitendo muungano wa Serikali mbili bila kujali vikwazo wala vizuizi vya wapinzani wanaotamani muungano huo uvunjike ili wapate nafasi ya kujipenyeza katika madaraka.
Your Ad Spot
Apr 25, 2017
Home
Unlabelled
CCM Z'BAR YASIFU JUHUDI ZA SMT NA SMZ ZA KUTAFUTA UFUMBUZI WA KERO ZA MUUNGANO
CCM Z'BAR YASIFU JUHUDI ZA SMT NA SMZ ZA KUTAFUTA UFUMBUZI WA KERO ZA MUUNGANO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇