Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi, Naibu wake Mhe. Dkt. Angeline Mabulla, Katibu Mkuu; Dkt Yamungu Kayandabila na Viongozi wengine wakuu wa wizara wakikagua magari ya kuhudumia ofisi za ardhi za kanda nchini.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi akikabidhi funguo ya gari kwa Kamishna wa kanda ya Dar es Salaam; Matthew Nhone.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi, Naibu wake Mhe. Dkt. Angeline Mabulla, Katibu Mkuu; Dkt Yamungu Kayandabila na Viongozi wengine wakuu wa wizara wakikagua magari ya kuhudumia ofisi za ardhi za kanda nchini.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeboresha ofisi zake za kanda za ardhi zilizopo nchini ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma za ardhi karibu zaidi na wananchi.
Wizara imegawa magari katika kanda zake zote ili kurahisisha utekelezaji wa kazi za ardhi na kuharakisha huduma za sekta nzima ya ardhi katika maeneo yote ya nchi badala ya wananchi kuja ofisi za Dar es Salaam ambazo kwa sasa zinahamia makao Makuu ya Nchi Dodoma.
Hatahivyo, huduma nyingine za kisekta kama vile za malipo ya kodi ya pango la ardhi, kituo cha huduma kwa mteja na ofisi za kanda za Dar es Salaam zitaendelea kufanyika kama ilivyokuwa awali.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi wakati akitangaza kuhamia rasmi kwa Wizara yake mkoani Dodoma amesema kuwa Wizara imepanga kuwaweka wataalam wa sekta nzima ya ardhi katika ofisi za kanda ili kuondoa usumbufu uliokuwepo wa kufuata huduma za hati, usajili, Uthamini upimaji na ramani na mipango miji na vijiji – Dar es Salaam na Dodoma.
Katika kutekeleza hili kila Kanda itakuwa na viongozi wake walio na mamlaka za utoaji wa huduma za ardhi na kuidhinishwa kwa nyaraka mbalimbali za ardhi na hata utoaji wa hati miliki kutolewa katika kanda.
Viongozi ambao watakuwepo katika kanda hizo ni pamoja na Kamishna na Kanda Msaidizi wa Ardhi, Msajili Msaidizi wa Hati wa Kanda, Mthamini Mkuu Msaidizi wa Kanda, Mkurugenzi Msaidizi wa Upimaji na Ramani wa Kanda, Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango Miji na Vijiji wa Kanda na Msajili Msaidizi wa Baraza la Ardhi na Nyumba wa Kanda.
Aidha jumla ya kanda ni nane ambazo ambazo zimeboreshwa na kuundwa upya. Kanda hizo ni; Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, ambayo itahusika na mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, na Dar es Salaam ndio makao makuu ya kanda. Kanda ya Nyanda za Juu Kusini; itahusika na mikoa ya Mbeya, Njombe, Rukwa na Songwe, ambapo Mbeya ndio makao makuu ya kanda. Kanda ya Kati; ni pamoja na mikoa ya Dodoma, Singida, Iringa na Morogoro na Dodoma ni makao yake makuu.
Aidha, Kanda ya Kaskazini; ni mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara, ambapo makao yake makuu ni Arusha. Kanda ya Ziwa; Ni mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera, ambapo Mwanza ndio makao yake makuu. Nyingine ni Kanda ya Magharibi; yenye mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi na Tabora ndio makao makuu ya kanda. Kanda ya Kusini; Ni mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na Mtwara ndio makao makuu ya kanda, na kanda ya nane ni Simiyu; yenye mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara na Simiyu ndio makao makuu.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇