Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MAKACHERO wa jeshi la polisi mkoani Pwani,wakishirikiana na waliotoka makao makuu ya polisi wanawashikilia watuhumiwa 16 akiwemo Khalid Mohammed (29)mkazi wa Kwamatias,Kibaha ,wanaodaiwa kufanya uporaji na mauaji kwenye maeneo mbalimbali.
Aidha baadhi ya watuhumiwa hao wanadaiwa kuhusika katika tukio la mauaji ya aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Liwale tangu mwaka 2012 hadi 2016,Ephraim Mfingi Mbaga(54).
Akizungumzia tukio hilo,kamanda wa polisi mkoani hapo,Boniventure Mushongi ,alieleza kwamba Khalid ambae ni fundi ujenzi,alikamatwa juzi huko eneo la Misugusugu kata ya Misugusugu.
Alisema mbali ya hayo ,alikamatwa akiwa na silaha aina ya SMG ambayo namba zake zimefutwa na risasi 14.
Kamanda huyo ,alisema alikutwa pia na risasi nne za shortgun,mlipuko mmoja,sime moja,mask moja na koti moja vyote vikiwa vimehifadhiwa kwenye mfuko wa rambo chini ya ardhi katika shamba la aliyejulikana kwa jina moja la Swai.
Hata hivyo,kamanda Mushongi alifafafanua kuwa,uchunguzi wa awali umebaini mtuhumiwa na wenzake 15 wamekiri kujihusisha na matukio ya uporaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
“Tukio mojawapo ni mauaji ya aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Liwale tangu mwaka 2012 hadi 2016, Ephraim Mbaga,aliyeuawa akiwa nyumbani kwake baada ya kupigwa risasi kwenye paja la mguu wa kushoto “
“Pia alijeruhiwa kwa kitu chenye ncha kali ambapo alipoteza maisha akiwa njiani akipelekwa hospitali ya rufaa ya Tumbi.”alisema.
Kwa mujibu wa kamanda Mushongi,tukio hilo lililotokea februari 18 mwaka huu saa 3.30 usiku,ambapo watu watatu wanaosadikiwa ni majambazi walimpiga na kitu kinachohisiwa ni silaha.
Alielezea ,marehemu alifariki njiani akipelekwa hospital ya rufaa ya Tumbi baada ya kuvuja damu nyingi.
Inaelezwa kuwa ,akiwa nyumbani kwake watu hao waliingia na kumtaka atoe pesa na aliposhindwa kufanya hivyo walianza kumjeruhi.
Katika eneo la tukio kilipatikana kichwa cha risasi kinachodhaniwa kuwa ni 7.62 mm inayotumiwa na silaha SMG/SAR ,na walifanikiwa kupora laptop mbili,simu za mkononi nne na vitu vingine ambavyo bado havijafahamika.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇