Clement
George Kamaha, almaarufu Sir George Kahama, (pichani), amefariki dunia alasiri Machi
12, 2017 wakati akipatiwa matibabu kwenye hospitali ya taifa Muhimbili jijini
Dar es Salaam.
Rais
John Pombe Magufuli, ametoa pole kwa familia ya marehemu Sir George ambaye aliwahi
kuwa waziri kuanzia serikali ya awamu ya kwanza hadi ya tatu.
Makala
hii ya gazeti la Jamhuri inaeleza zaidi kuhusu maisha ya Sir George Kahama.
Msemo wa Kiswahili usemao, “kimya kingi kina mshindo mkuu, ni sahihi kwa mujibu wa
mwenendo wa kisiasa aliokuwa nao mwanasiasa mkongwe wa nyakati zote,
aliyeingizwa kimyakimya katika harakati za kudai uhuru wa iliyokuwa Tanganyika
miaka kadhaa kabla ya nchi kujitawala.
Clement
George Kahama, al-maarufu Sir. George, ni mtumishi wa umma aliyekuwa mtendaji
mkuu na mwanasiasa aliye mahiri na makini, katika utendaji kazi kuanzia nyakati
za Tanganyika kudai uhuru mnamo miaka ya 1950, hadi kujitawala mwaka 1961, na
baada ya
uhuru mpaka alipostaafu utumishi wake kwa umma si miaka mingi iliyopita.
uhuru mpaka alipostaafu utumishi wake kwa umma si miaka mingi iliyopita.
Kwa
hakika, ni nadra mwanasiasa kukiri mapungufu katika matamanio ya utendaji wake,
hata kama msingi wa mapungufu yale haukuwa ndani ya maamuzi yake binafsi,
isipokuwa ni mkakati wenye kuamuliwa na dola.
Hata
hivyo, kwa kuwa mapungufu yale yalihusu matamanio yaliyotokana na utafiti wake,
anachukuliaa ni mapungufu yake.
Viporo
vyake hivyo ni pamoja na vva kiuchumi amnbavyo tutavijadili baadaye.
Kwanza
tutazame ni jinsi gani Sir George aliingizwa kimyakimya katika harakati za
kudai uhuru wa iliyokuwa Tanganyika, na katika mazingira ya aina gani, na nani
alimwingiza na kwa sababu gani.
Wengi
wanajua na kukiri ya kuwa, Sir. George Kahama alikuwa rafiki wa karibu wa Baba
wa Taifa, Mwalimu Julius Kambaragae Nyerere, ambapo chanzo cha urafiki wao,
ndilo jibu la jinsi gani mwanasiasa huyo mkongwe, aliingizwa kwa faragha katika
siasa, hususan mazingira yaliyohusika.
Kwa
wale wanaotambua kwamba dhamira ya wakoloni kuwa, ni kuendelea kutawala na
kunyonya makoloni, wana imani ya kuwa Mwalimu Nyerere alipopelekwa masomoni
Uingereza kuboresha taaluma yake ya ualimu, ilikuwa ni mbinu ya wakoloni ya
kuzima japo kwa muda, vuguvugu lake la kudai uhuru wa Tanganyika, na ndiko
alikokutana na Sir. George Kahama akisoma pia.
Kahama
alipelekwa Uingereza na Chama cha Ushirika wa Zao la Kahawa cha jimbo lililoitwa
Ziwa Magharibi wakati ule, likiwa na wilaya za Bukoba, Karagwe, Biharamulo na
Ngara, na sasa ni mkoa wa Kagera, ili kusomea taaluma ya ushirika na masoko kwa
ajili ya maendeleo ya chama kile.
Katika
kutimiza dhana yao ya kuzima harakati za Nyerere za kudai uhuru, na kwa vile
hakuwa peke yake katika harakati zile, wakoloni walimpatia masurufu yasiyokidhi
mahitaji yake akiwa masomoni, kusudi akose uwezo wa kuwasiliana na waasisi
wenzake kwa kuwatumia nyaraka kwa njia ya posta.
Alipokwisha
taabika kwa muda mrefu akisaidiwa na baadhi ya wanachuo wenzake kutoka
Tanganyika waliokuwa katika vyuo mbalimbali vya Uingereza, ndipo alipodokezwa
ya kuwa yupo mwenzao aitwaye Clement George Kahama katika chuo kingine kuwa,
alikuwa na uwezo kifedha kutokana na kusomeshwa na chama cha ushirika wa zao la
kahawa.
Mwalimu
Nyerere alifurahi akawa na matumaini ya kusaidiwa, kwanza kwa sababu
alikwishaona ushirikiano wa Watanganyika wengine, akajua hata Kahama
atamsaidia.
Lakini
kwa mujibu wa Sir George, tumaini la Nyerere lilizidishwa na ukweli kwamba,
wote wawili ni watani wa jadi.
Tangu
walipokutana mpaka waliporejea nyumbani baada ya kuhitimu masomo, gharama zote
za kutuma nyaraka za kisiasa kuja kwa waasisi wa harakati za kudai uhuru,
zilitolewa na Sir George, kiasi kwamba, hata wenye kujadili ni jinsi gani
alipachikwa cheo cha Sir, wanadhani Nyerere kiutani huenda ndiye alimwita vile
kutokana na mazingira ya msaada huo.
Kwa
mujibu wa mazungumzo yangu na Sir George niliyofanya naye kwa nyakati tofauti
kati ya mwaka 1987 na 1990, nikiwa naye Beijing, China alipokuwa Balozi wa
Tanzania nchini humo, na mimi nikiwa mtangazaji katika Idhaa ya Kiswahili ya
Radio China, Sir George alikatiwa hata kadi ya TANU na Nyerere akapelekewa
Uingereza kwa njia ya posta.
Wote
wawili, Nyerere na Kahama walipokwisha rejea nchini na kila mmoja akaripoti kwa
mwajiri wake, Mwalimu Nyerere alijiuzulu kazi ya ualimu katika Shule ya
Sekondari Pugu, Dar es Salaam kusudi aendeleze kikamilifu siasa za kudai uhuru,
ambapo Kahama aliendelea na kazi katika chama cha ushirika wa zao la Kahawa
jimboni Ziwa Magharibi (BCU), mjini Bukoba.
Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisafiri nchi nzima akishawishi
wananchi waunge mkono madai ya uhuru, akawa amekumbana na mikikimikiki toka kwa
watawala wa kikoloni, yakiwa ni pamoja na kushtakiwa Mahakamani kwa tuhuma ya
kichochea uasi kwa utawala wa kikoloni.
Alipokwisha
dai uhuru hadi katika Umoja wa Mataifa New York, ndipo Nyerere alipopewa fursa
na watawala wa kikoloni mwaka 1958, ya kuunda Serikali ya Madaraka wakiwa na
lengo la kuhakiki uwezo wa Watanganyika kujiendeshea nchi yao wenyewe.
Wakati
inaundwa Serikali ile, ndipo Mwalimu Nyerere alipomwita Sir George kutoka
Bukoba, ili ajiunge na Baraza la Mawaziri la Serikali hiyo, akamteua kuwa
Waziri wa Ushirika na Masoko na mwenyewe (Nyerere) akawa Waziri Mkuu.
Baadhi
ya mawaziri walioteuliwa walikuwa Paul Bomani, Chifu Abdallah Fundikira, Rashid
Mfaume Kawawa, Solomon Eliofoo, Nsilo Swai, Said Maswanya, Dereck Noel
Bryceson, Sir. Ernest Versey na Amir Jamal.
Serikali
ya Madaraka iliendelea kuwapo sambamba na ya kikoloni na ilipofika
Desemba 9, 1961 kama ilivyoahidiwa na Umoja wa Mataifa, Tanganyika
ilitangazwa kuwa huru, na Baraza la Mawaziri lenye madaraka kamili likaundwa,
Sir George akiwa waziri wa kwanza wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mbali
ya nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali, Sir George alipata kuteuliwa
kuanzisha taasisi nyeti za kimaendeleo, zikiwa ni pamoja na Shirika la Taifa la
Maendeleo ya Viwanda (NDC); Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA); na
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Kati
ya maswali mengi niliyomuuliza Sir George pasipo nia ya kuyatumia kihabari,
lakini yakawa yamedumu katika kumbukumbu zangu, ni pamoja na jinsi gani baadhi
ya watendaji kama yeye, waliweza kubaki karibu na Mwalimu Nyerere mpaka
alipong’atuka madarakani, na wengine kama yeye akawashurutisha wabaki kumalizia
voporo vyake.
Kwa
tabasamu lake lisilokwisha katika sura yake, Sir. George aliniambia ya kuwa,
aliweza kudumu karibu na Nyerere kwa sababu mbili: Kwanza ni kwa kuwa alijuana
naye wakiwa wanafunzi ugenini, kwa hiyo, waliunda ukaribu wa aina yake kwa
jinsi walivyosaidiana. Lakini pili, ni kwa kumjua Nyerere matakwa yake katika
nafsi.
Nilipomtaka
anifafanulie hiyo sababu ya pili, alisema kwa kuwa Nyerere ni mzaliwa katika
ukoo wa utemi wa kimila, alitawaliwa na dhana itokanayo na mienendo ya utemi.
Akasema
mtemi, licha ya kuwa na washauri wake, lakini fikra ya mwisho hata ikitoka kwa
washauri, mwenye nayo ni yeye.
Kwa
hiyo, alipokuwa madarakani akishauriana na washauri wake ambao ni pamoja na
mawaziri wa Serikali yake, uamuzi wake ukishagota mahali, kila mmoja anatakiwa
awe makini na jinsi gani azidi kuchangia mawazo ili asitofautiane na uamuzi
wake.
Aliendelea
kufafanua kuwa, endapo mshauri ataamini kuwa wazo lake ni la busara, hana budi
atafute wakati muafaka kama vile kumtembelea nyumbani kwake kwa matembezi ya
kawaida, halafu akishamdokeza wazo lake na Mwalimu akaliona lina mantiki,
likiletwa mezani kujadiliwa na washauri wengine, basi wazo lile linakuwa ni
lake yeye Mwalimu, na si la mshauri husika.
Alinichekesha
pale aliponipa mifano ya washauri wa Mwalimu ambao sitataja majina yao, kwamba
baada ya mawazo yao kupokelewa na Nyerere yakawa yamefanyiwa kazi, walinong’ona
kwa watu kuwa ni mawazo yao.
Mwalimu
alipopewa habari juu ya ‘majigambo’ ya watu waliompatia ushauri, washauri hao
ukawa ni mwisho wa kuionekana kuwa karibu na Mwalmu.
Alisema
ya kuwa kimsingi huo ndio mwenendo wa watawala karibu wote duniani.
Nilipenda
kujua kwa nini yeye Sir George, aliteuliwa na Nyerere mwishoni mwa utawala wake
kabla ya kung’atuka mwaka 1984, aende kuwa Balozi wa Tanzania China, ambapo
alikwisha nidokeza mapema kabla ya kuwa alitaka naye astaafu.
Alinijibu
ya alishindwa kumkatalia kwa sababu hakutaka kumkaidi Mwalimu wakati
anapumzika.
Alikiri
ya kuwa, uteuzi ule japokuwa aliupokea akijihisi kuchoka, lakini alijifunza
mengi China kuliko mahali popote alikopata kuwa Balozi wa Tanzania.
Ni
wakati huo alipopata wazo la kuifanya Zanzibar iwe kama Hong Kong ya Afrika
Mashariki, Kati na Kusini, kama kitovu cha biashara cha eneo hili, kama ilivyo
Hong Kong yenyewe kwa eneo la Asia Kusini Mashariki na Mashariki ya mbali.
Lengo
la Mwalimu Nyerere kumteua Sir George kuwa Balozi wa Tanzania nchini China ilikuwa
ni kwenda kujifunza jinsi Wachina licha ya siasa yao ya ujamaa, waliweza
kukaribisha sera za kibepari ili ziwasaidie kuboresha ujamaa wao, jambo ambalo
linabainika dhahiri hivi sasa. Mwalimu alitaka mbinu hiyo itumike hapa
Tanzania.
Jibu
la jumla alilopata Sir George ni kwamba uwekezaji wa mitaji ya kigeni
ilikaribishwa China bila kuacha ujamaa wake, na sasa taifa hilo limekuwa tishio
kwa mataifa makubwa ya kibepari.
Taifa
hilo limekuwa tishio kiuchumi wakati ujamaa wa nchi hiyo ungali palepale
ukiungwa mkono na wananchi wake.
Sir
George anasema kuwa, hata wakati utawala wa China unarudishiwa eneo la Hong
Kong na Waingereza, China ilitangulia kuboresha miji yake ya pwani iliyoko
mkabala na Hong Kong, kiasi kwamba mataifa ya kibeberu hayakufurukuta kuitambia
China juu ya mji wa Hong Kong, kwa sababu miji ya Guanghjou, Zhuhai, Shengzhen
na Shanghai, ilikwishakuwa na hadhi sawa na Hong Kong au kuizidi.
Sir
George Kahama alimalizia mahojiano yake ya hivi karibuni kwa kusema kuwa, licha
ya mazoea ya wanasiasa kutokiri mapungufu katika utendaji wao, lakini yeye
anasikitishwa na kutokamilisha ndoto zake tatu anazoamini kwa umuhimu wake
ulivyo, siku moja walioko madarakani watazitekeleza.
Ndoto
hizo tatu ni pamoja na ileile ya kuigeuza Zanzibar kuwa Hong Kong ya eneo la
Afrika Mashariki, Kati na Kusini; ya pili ni kuanzishwa kwa benki ya ushirika
ambayo wadau wake wakuu watakuwa ni Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS);
na ya tatu ni kuyafanya makao makuu Dodoma yawe ya kweli ili Serikali ihamishie
kabisa makao yake huko.
Baada
ya kurejea kutoka China alikokuwa Balozi na kuhamia kwa muda Zimbabwe,
Sir George alianzisha Kituo Cha Uwekezaji Mitaji Tanzania, yaani Tanzania
Investment Centre (TIC), kwa lengo la kuvuta mitaji ya ndani na nje ili
kuzidisha maendeleo ya kiuchumi nchini, ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya miaka
50 ya uhuru inayosherehekewa hivi sasa.
Mungu ailaze roho yake pahala pema..
ReplyDelete