Na Bashir Nkoromo
JUMUIA ya Wazaziya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametakiwa kuiunga mkono Serikali, katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya ili kuwaokoa Watanzania hasa vijana katika janga linalotokana na matumizi ya dawa hizo.
Mwito huo umetolewa jana, na Katibu mpya wa Jumuia hiyo mkoa wa Dar es Salaam, Stanley Mkandawile wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Jumuia ya Wazazi Wilaya ya Ilala, akiwa katika ziara ya kujitambulisha kwa viongozi na watendaji hao.
Alisema, wana-CCM hasa jumuia hiyo ya Wazazi ni lazima waonyeshe kwa dhati kuunga mkono mapambano hayo kwa sababu serikali inatekeleza mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuwa inatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015-2020 ibara ya 118 hadi 119.
"Pamoja na kwamba kila mwana CCM analo jukumu hili na kuisaidia serikali kutokomeza dawa za kulevya, lakini lazima mtambue kuwa sisi Jumuia ya Wazazi tuna wajibu mkubwa zaidi kwa kuwa jumuia hii, ndiyo hasa imebeba jukumu la kuhakikisha vijana wetu wanakuwa katika malezi sahihi na salama", alisema Mkandawile.
Alisema, miongoni mwa madhara ya dawa za kulevya, ni vijana kushindwa masomo na kutokomea mitaani au kukaa nyumbani kama mazezeta na wengine hasa wasichana kupata maabukizi ya ukimwi kutokana na kujiingiza katika mapenzi hatarishi ili kupata fedha za kununua dawa hizo za kulevya.
Mkandawile alisema, anaamini chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, vita hiyo ambayo sasa imesambaa nchi nzima, itafanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuokoa nguvu kazi ya taifa hasa vijana.
Pia Mkandawile alisema, Jumuia hiyo inaunga mkono Serikali, kupigavita matumizi ya viroba kwa kuwa navyo vina mchango mkubwa katika kudumaza baadhi ya wanafunzi, ambapo alisema, baadhi wakipewa fedha kwa ajili ya masomo hununua viroba na wakishalewa wanahonga machangudoa na kujikuta wamepata maabukizi ya ukimwi.
Akizungumzia uhai wa Jumuia hiyo, Mkandawile aliwataka viongozi kuhimiza wananchama kulipa ada kwa jumuia na Chama, na pia kuhakikisha wanachama na viongozi wanashiriki mara kwa mara katika shughuli za kijamii, ili kuwavutia wananchi wengine kujiunga na CCM na jumuia zake.
Alionya viongozi kujiepusha na tabia iliyojengeka kwa baadhi yao, kupendelea zaidi kuchagua au kuwapa nafasi za uongozi watu kwa kutazama uwezo wa kifedha, akisema, kufanya hivyo kunasababisha Chama au Jumuia kuwa na viongozi maslahi wasio na uwezo wa kusimamia shughuli za chama badala yake wanashughulika na maslahi yao.
Mkandawile aliwataka katika uchaguzi ujao wa Chama, kuhakikisha wanawakwepa wanaotafuta uongozi kwa njia za fedha, na badala yake wahakikishe wanawachagua wale ambao kwa dhati kabisa wanawaona kuwa wanao uwezo wa kiutendaji na ari ya kuwatumikia wananchi.
"Mambo haya lazima muwe nayo makini sana, unakuta mtu kauza korosho au mazao mengine, anaibuka ghafla eti na yeye anataka uongozi, hata kadi ya CCM hana, anarubuni viongozi kwa fedha zake anapewa kadi leo leo lakini kwa sababu ya rushwa inaonyesha ni ya miaka 20 iliyopita, hili lazima tulipite vita kabisa", alisema Mkandawile
Mkandawile alihamishiwa hivi karibu kuwa Katibu wa Jumuia hiyo ya Wazazi mkoa wa Dar es Salaam, akitokea mkoani Kigoma ambako pia alikuwa Katibu wa Jumuia hiyo.
Your Ad Spot
Mar 2, 2017
Home
Unlabelled
MKANDAWILE: VITA YA SERIKALI DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA NI UTEKELEZAJI ILANI YA CCM
MKANDAWILE: VITA YA SERIKALI DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA NI UTEKELEZAJI ILANI YA CCM
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇