RAIS SHEIN ATIMIZA AHADI YA KUTOA VIFAA KUKAMILISHA UJENZI WA MSIKITI MKUU BARIADI
Na Stella Kalinga, SIMIYU
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Ali Mohamed Shein ametimiza ahadi ya kutoa sadaka ya vifaa vya ujenzi wa Msikiti wa MASJID RAUDHAL mjini Bariadi, ambao ni Msikiti mkuu Simiyu.
Rais Shein alitoa ahadi hiyo mwezi Oktoba 2016 wakati alipokuwa Mkoani Simiyu kuwaongoza Watanzania katika Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Wiki ya Vijana na Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwl.Nyerere.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo,Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka amemshukuru Mhe.Rais Shein na kubainisha kuwa ujio wake mwaka jana umeleta mafanikio makubwa kwa mkoa na kujenga uhusiano mazuri kati ya Mkoa wa Simiyu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mtaka amesema ujio wa Dkt Shein mkoani Simiyu umefungua milango ya ushirikiano wa kibiashara kati na Zanzibar, ambapo alimtuma Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe.Riziki Pembe Juma mwezi Desemba mwaka jana kuja kuona Chaki za Maswa na sasa Mkoa huo unauza chaki Zanzibar.
Aidha, ameongeza kwa kupitia ujio wake alimtuma Waziri wa Biashara,Viwanda na Masoko, Balozi Amina Salum Ali kuona fursa za biashara na sasa wananchi wa Simiyu wamehakikishiwa soko la Mchele na mazao ya mikunde Zanzibar kupitia makubaliano yatakayowekwa kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkoa wa Simiyu.
"Dkt.Shein Akiwa Simiyu amefanya ya kimwili na ya kiroho sisi kama Mkoa tutakuwa mashahidi wa kazi na utumishi wake;kupitia yeye tumefanya biashara Zanzibar, kupitia yeye Msikiti wetu unajengwa kwa sadaka yake na kupitia yeye tumefungua milango mipana ya ushirikiano" alisema.
Amesema Serikali ya Mkoa iko tayari kushirikiana na BAKWATA katika kuhakikisha mapungufu yatakayojitokeza yanatatuliwa ili Msikiti wa Kisasa na Ofisi za kisasa za BAKWATA zinajengwa ambazo zitaendana na hadhi ya makao makuu ya Mkoa.
Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi na waumin wa Kiislamu Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mahamoud Kalokola amesema anamshukuru Rais Shein kwa sadaka yake hiyo ambayo ina thawabu kubwa kwa Mwenyezi Mungu.
"Tunamshukuru sana Mhe.Rais Shein kwa sadaka yake na tunamwomba Mwenyezi Mungu amuongezee pale alipotoa, maana Quran inasema ajengaye msikiti anajijengea nyumba peponi" alisema.
Vile vile Sheikh Kalokola ametoa wito kwa watu wote wenye mapenzi mema kusaidia mahali popote misikiti inapojengwa ili kuwawezesha waumin kupata mahali pa kuswali jambo ambalo litawapa thawabu kwa Mwenyezi Mungu.
Vifaa vilivyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Ali Mohammed Shein kama sadaka yake ni saruji,nondo, rangi,mbao n.k ikiwa ni pamoja na fedha taslimu kwa ajili ya malipo ya mafundi na vimewasilishwa kwa niaba yake na Ally Habshy Abdallah, ili kukamilisha msikiti wa MASJID RAUDHAL.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇