JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
Katibu Mkuu,
Dodoma, Januari 5, 2017:
Ndugu wanahabari,
Nimewaita hapa leo kwa lengo la kuwapa taarifa rasmi wanataaluma ya habari na wananchi kwa ujumla kuhusu mada iliyotajwa hapo juu. Kama mnavyofahamu, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alisaini Sheria ya Huduma za Habari Novemba 16, 2016 na siku mbili baadaye yaani Novemba 18, 2016 Sheria hiyo ikatangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
Kwa mujibu wa kifungu cha 1 cha Sheria hiyo, ili ianze kutumika rasmi, Waziri wa Habari anatakiwa kuitangaza tarehe ya kuanza kutumika. Napenda kuufahamisha umma kuwa nikiwa Waziri mwenye dhamana hiyo nimeshatekeleza wajibu wangu kwa kutangaza kwenye gazeti la Serikali kuwa sheria hii imeanza kutumika tangu Desemba 31, 2016.
Ndugu wanahabari,
Kuanza kutumika kwa sheria hii ni jambo muhimu sana kwa tasnia, kwa sababu kunaanzisha mchakato rasmi wa kuihamisha taaluma ya habari kutoka fani ambayo mtu yeyote anaweza kujinasibu nayo, hadi kuwa taaluma kamili yenye sifa mahsusi, maadili yanayojulikana lakini na vyombo vya kusaidia kusimamia utekelezaji wake.
Kama tulivyosisitiza awali, sheria hii pia inaleta mfumo madhubuti wa kulinda haki za wanahabari kukusanya, kuchakata na kusambaza habari zao kwa uhuru. Vyombo vya sasa vitatekeleza haki yao hii ya kikatiba bila vikwazo visivyokuwa na sababu.
Aidha, umma na wanatasnia ya habari pia wanakumbushwa kwamba kwamba sheria hii, kwa lengo la kuwa na wanataaluma wanaotekeleza vyema wajibu wao, na kama ilivyo kwa taaluma nyingine, imeweka wajibu kwa wale watakaokiuka misingi na maadili ya taaluma. Hii ina maana ukurasa mpya wa haki na wajibu umefunguliwa.
Simu: +22 2126826 Nukushi: +22 2126834 Tovuti: www.habari.go.tz Baruapepe: km@habari.go.tz
Jengo la LAPF, Ghorofa ya Nane, S. L. P. 25, DODOMA
Katika utekelezaji wa sheria hii kuna vyombo vilivyopo sasa vitaongezewa majukumu au kazi zake kuhuishwa, kuna vyombo vipya vitaanzishwa na kuna taratibu mpya za kiutendaji zitaandaliwa. Yote hayo Serikali itaendelea kuufahamisha umma kadiri yanavyoendelea kukamilika.
Kanuni za Sheria ya Huduma za Habari, 2017
Ndugu wanahabari,
Kwa mujibu wa kifungu cha 65 nikiwa Waziri wa Habari nimepewa jukumu la kutunga kanuni za kusaidia utekelezaji wa sheria hii. Napenda kwanza kuwashukuru wadau wengi walioleta maoni yao tena kwa kujenga hoja kwa maandishi na utafiti. Ninayofuraha leo kuwataarifa kuwa tumefaidika sana na maoni hayo na kanuni hizo zimeshachapishwa kwenye Gazeti la Serikali la Ijumaa Februari 3, 2017.
Kanuni hizi zimesheheni masuala ya kusaidia utekelezaji wa sheria na hasa muktadha mzima wa kufikia Tanzania kuwa na kile nilichokiainisha hapo juu-vyombo vya habari vyenye uhuru wa kutosha lakini pia vinavyowajibika ipasavyo kwa umma.
Kubwa katika kanuni hizi na ambalo limetolewa maoni na wengi wakati wa kukusanya maoni ya wadau, nafahamu wengi pia wanasubiri kusikia, ni kiwango cha elimu ili mtu aweze kuruhusiwa kufanyakazi ya taaluma ya habari nchini.
Tumesoma, tumechambua maoni ya wengi; wapo waliotaka iwe cheti, wengine diploma, wengine digrii wengine walitaka iwe hata PhD na wapo waliotaka iwe mtu yeyote anayejua tu kusoma na kuandika!Serikali imesimama katikati ya maoni hayo. Sifa ya chini kabisa kwa kuanzia itakuwa ni diploma ya uandishi wa habari.
Hata hivyo, Serikali imetoa kipindi cha mpito cha miaka mitano kuanzia Januari mosi mwaka huu kwa waandishi waliopo sasa na wanaotaka kuingia katika taaluma hii ambao hawana sifa hizi wakasome.
Ili kusaidia wanahabari hasa waliopo sasa makazini waweze kujiendeleza, kupitia Idara ya Habari MAELEZO, tutaendelea kutoa “press card” bila kuwabana sana wanahabari kwa kuangalia vigezo hivi vya kitaaluma bali dhamana ya waajiri wao tu.
Masuala mengine ya utekelezaji wa sheria na kanuni hizi tutaendelea kuutaarifa umma kadiri yanayokamilika au kuanza kutekelezwa.
Nawashukuru kwa kunisikiliza.
Nape M Nnauye (MB)
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Your Ad Spot
Feb 5, 2017
Home
Unlabelled
KUANZA KUTUMIKA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI, 2016 NA KANUNI ZAKE, 2017
KUANZA KUTUMIKA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI, 2016 NA KANUNI ZAKE, 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇