Rais Dk. John Magufuli akijadiliana jambo na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta baada ya kutangazwa rasmi kwa Jina la Mwalimu Julius Nyerere katika kituo hicho cha Amani na Usalama.
Rais Dk. John Magufuli akijadiliana jambo na Rais wa Rwanda Paul Kagame wakati wakielekea katika Kituo cha Amani na Usalama cha Makao Makuu ya Umoja wa Afrika kilichopewa jina la Rais wa kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere, Addis Abba nchini Ethiopia, leo. PICHA NA IKULU
----------
TAARIFA RASMI KUTOKA ETHIOPIA
----------
TAARIFA RASMI KUTOKA ETHIOPIA
Jengo
la amani na usalama lililopo makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) Mjini Addis
Ababa nchini Ethiopia leo tarehe 29 Januari, 2017 limetangazwa rasmi kuwa
litaitwa Mwalimu Julius Nyerere.
Jengo
hilo limepewa jina hilo rasmi katika hafla ya chakula cha mchana iliyofanyika
leo na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli pamoja na Marais mbalimbali wa nchi wanachama wa Umoja wa
Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Antonio Guterres, Mawaziri na
Mabalozi mbalimbali wanaohudhuria Mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa
Umoja wa Afrika unaoendelea Mjini hapa.
Akizungumza
katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli amewashukuru viongozi wote wa Umoja wa
Afrika kwa kuamua jengo hilo liitwe jina la Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni
kutambua mchango wake katika kupigania amani na usalama na amebainisha kuwa
Mwalimu Nyerere alikuwa Mwafrika halisi na kiongozi mahiri na shupavu.
“Na
kwa hakika naweza kusema kuwa alikuwa mmoja wa viongozi bora kabisa ambaye
amewahi kutokea katika Bara letu, katika maisha yake yote Mwalimu Nyerere
alipambana ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Afrika, alikuwa mmoja
wa waanzilishi wa umoja huu, sisi Watanzania kwa hakika tunajivunia sana
Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa”
amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika
kupambana na ubaguzi na unyonyaji wa kila aina, alisaidia ukombozi wa nchi
nyingi za Afrika, na hata alipong’atuka katika hatamu za uongozi wa Taifa la
Tanzania aliendelea kutoa mchango wake kupigania amani katika nchi za Afrika.
“Wito
wangu kwenu, waheshimiwa viongozi ni kwamba, sambamba na kumuenzi Mwalimu
Nyerere kwa jengo hili, itakuwa ni jambo jema zaidi kama tutajitahidi kufuata
nyayo zake pamoja na kuishi maisha ya viongozi wengine hodari wa Bara hili
wakiwemo Hayati Kwame Nkhrumah, Ahmed Ben Bella, Sekou Toure, Gamal Abdel
Nasser na bila kusahau shujaa wetu mwingine Hayati Nelson Mandela”
amesisitiza Rais Magufuli.
Mkutano
wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaendelea kesho tarehe 30
Januari, 2017 hapa Addis Ababa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇