LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 20, 2017

KINANA NA DK. SHEIN KUUNGURUMA KESHO ZANZIBAR, WAKATI WA KUFUNGA KAMPENI ZA CCM JIMBO LA DIMANI

Katibu Mkuu wa CCM,Andulrahman Kinana akimnadi Mgombea wa Ubunge jimbo la Dimani Juma Ali Juma, katika uzinduzi wa kampeni za Uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo hilo, mjini Zanzibar, Januari 5, 2017.
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kesho wanatarajia kuunguruma katika  Kiwanja Cha Shule ya Fuoni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja, wakati wa shughuli pevu ya kufunga kampeni za CCM za Uchguzi mdogo jimbo la Dimani.

Hayo yamesemwa leo na Katibu wa Idara ya Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar,  Waride Bakari Jabu wakati akizungumza na Waandishi wa habari, kueleza maandalizi ya kufungwa kwa kampeni hizo kwa upande wa CCM na kuongeza kwamba maandalizi hayo yamekamilika kwa kufuata miongozo, ratiba na masharti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)

Alisema Dk. Shein ambaye atawahutubia wananchi kwa kueleza sera, mikakati na muelekeo wa utekeleza wa shughuli za kimaendeleo zilizotekelezwa na Chama hicho na zinazotarajiwa kutekelezwa katika maeneo mbali mbali nchini hasa katika jimbo la Dimani, akitanguliwa na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Zanzibar Vuai Ali Vuai. 

Aidha alisema matarajio ya CCM katika Uchaguzi wa Jimbo hilo ni kuendeleza ushindi wa kihistoria kutokana na wananchi wa rika mbali mbali kumkubali mgombea wa Chama hicho, Juma Ali Juma na kuahidi siku ya uchaguzi watamchagua rasmi bila pingamizi awe Mbunge wa jimbo hilo.

“ Tunawaomba wafuasi wetu na wananchi kwa ujumla mjitokeze kwa wingi katika Mkutano wa Ufungaji wa kampeni za CCM kesho (leo) ili muweze kusikiliza sera na mipango endelevu inayotekelezeka kwa vitendo itakayoelezwa kuwa ufasaha na Dk. Shein pamoja na viongozi wengine.

Pia wale ambao ni wakaazi na wapiga kura halali wa Jimbo la Dimani  tuendelee kuhamasishana nyumba kwa nyumba ili siku ya uchaguzi Januari 22 mwaka huu, tujitokeze kwa wingi katika vituo vya kupigia kura kwa lengo la kumpa ridhaa Juma Ali Juma aweze kuwatumikieni kupitia vipaumbele vyake.”, alieleza Waride na kuongeza kuwa CCM ndio Chama pekee kinachotambua thamani na utu wa makundi yote ya kijamii yaliyopo nchini.

Aliwasihi wafuasi wa CCM kufuata utaratibu na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoashiria vurugu na uvunjaji wa kanuni za wapiga kura siku ya uchaguzi badala yake wale waliotimiza umri wa kupiga kura na wamekamilisha taratibu zote kisheria wafike mapema katika vituo kwa kupiga kura na kurudi nyumba kusubiri matokeo.

Uchaguzi huo unafanyika kufuatia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani Unguja, Hafidh Ali Twahir kufariki Dunia ghafla mwaka uliopita  akiwa katika utekelezaji wa Majukumu yake huko bungeni Mjini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages