Na Is-haka Omar, Zanzibar.
ZAIDI ya shilingi milioni 43 zimetumika kununua vifaa mbali mbali vya Jimbo la Chumbuni Zanzibar, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Viongozi wa jimbo hilo kwa wananchi katika Kampeni za Uchaguzi uliopita.
Akisoma Risala katika hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo, Abrahman Abass alisema vifaa hivyo vimetolewa na viongozi wa jimbo hilo ambao ni Mbunge, Mwakilishi na Madiwani.
Alivitaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni Gari moja aina ya Canter, Dawa za binadamu kwa ajili ya vituo vya Afya vya jimbo hilo pamoja na jezi za mpira wa miguu kwa timu za jimbo zenye usajili wa ZFA.
Alisema tangu viongozi hao waingie madarakani kwa kipindi cha miezi 14 kwa mbunge na miezi minane kwa Mwakilishi na Madiwani tayari wameshatumia zaidi ya milioni 205 katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ndani ya jimbo hilo.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa wananchi mbali mbali wa Chumbuni, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Vuai Ali Vuai aliwasihi wafuasi wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazofanywa na viongozi hao.
Alisema endapo wananchi wa Jimbo la Chumbuni wataendelea kushirikiana na viongozi wao vizuri jimbo hilo litakuwa miongoni mwa majimbo ya kuigwa kimaendeleo hapa nchini.
Vuai ambaye pia ni Mlezi wa Jimbo hilo alisema Chama hicho kwa sasa kinahitaji viongozi imara na wabunifu wenye uwezo wa kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 bila ya kusukumwa kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
“ Suala la maendeleo halina Chama wala kabila kwani misaada inayotolewa na viongozi wetu wa jimbo hili na mengine naamini wanaonufaika ni wananchi wote na sio Wana CCM pekee, hivyo tuwaunge mkono juhudi zao na kuthamini na kutunza vifaa wanavyotoa ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
Pia wananchi nakukumbusheni kuwa juhudi hizi ni matunda ya Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyofanywa na wazee wetu kwa lengo la kutuweka huru ili tujitawale na kutengeneza miundombibu imara ya maendeleo ya nchi yetu.”, alifafanua Vuai na kuwataka viongozi hao kuendelea kutoa misaada mbali mbali ya kimaendeleo kadri hali za kiuchumi zitakavyoruhusu ili wananchi waweze kunufaika na fursa hizo.
Aidha alipongeza viongozi hao kwa utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho kwa wananchi na kuongeza kuwa wametekeleza kwa vitendo matakwa ya Katiba ya CCM.
Hata hivyo aliwasihi vijana, wanawake na wazee wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika mwaka 1964.
Pamoja na hayo alitoa ahadi ya shilingi milioni moja kwa Vikundi mbali mbali vya ujasiriamali vya jimbo hilo ili ziweze kuwasaidia katika harakati zao za kimaendeleo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo hilo, Ussi Salum Pondeza “Amjadi” alisifu ushirikiano uliopo baina yake na viongozi wengine wa Jimbo hilo na kuahidi kuwa wataendelea kuwatumikia wananchi kwa ufanisi zaidi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇