Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema hakuna
uthibitisho wa kuwepo kwa ugonjwa wa Zika nchini humo.
Ufafanuzi wa Wizara hiyo umekuja
siku moja baada ya Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR),
kutoa ripoti ya utafiti uliofanywa na taasisi hiyo kwa kushirikia na
Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Bugando, inayoeleza kuwepo maambukizi ya
virusi vya Zika katika jamii ya Watanzania.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Ummy Mwalimu ametoa ufafanuzi huo
kwa waandishi wa habari , ambapo alisema wananchi wanapaswa kuondoa hofu
kwa kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini.
Awali, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini Tanzania
(NIMR) ilitangaza kuwa, virusi vya Zika vimegunduliwa nchini
humo. Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini
Tanzania (NIMR), Dkt Mwele Malecela, ambaye alitangaza kugunduliwa kwa
virusi vya Zika nchini Tanzania, amefutwa kazi.
Taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Ikulu, Gerson Msigwa inasema Rais wa John Magufuli wa
Tanzania ametengua uteuzi wa mkurugenzi huyo mkuu. Tayari Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemteua Prof Yunus Mgaya kuwa
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
(NIMR) saa chache baada ya kumfuta kazi mkurugenzi wa awali Dkt. Mwele
Malecela.
Brazil ndiyo chimbuko la mbu
wanaosambaza kirusi cha Zika ambacho sasa kimeenea katika nchi 46
duniani tokea kuibuka kwa mara ya kwanza mwaka 2015. Kirusi hicho pamoja
na mambo mengine husababisha wanawake wajawazito kujifungua watoto
wenye vichwa vidogo na walio na matatizo ya ubongo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇