Mbunge
wa Jimbo la Ilala Mhe. Azzan Musa Zungu akiwa amelazwa katika Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya moyo
ambapo kwa sasa hali yake inaendelea vizuri. Kutoka kulia ni Muuguzi
Mwandamizi Sr. Chagui Mgaza na kushoto ni Mwinyi Maulidi ambaye ni
dereva wa Mhe. Zungu.Picha na Anna Nkinda - JKCI.
Na Anna Nkinda – JKCI.
1/12/2016 Mbunge wa Jimbo la Ilala Mhe. Azzan Musa Zungu amewashukuru
wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma
nzuri ya matibabu wanayompatia na kuiomba taasisi hiyo kutoa huduma kama
hiyo kwa watanzania wote.
Mhe.
Zungu ambaye amelazwa katika Taasisi hiyo amezitoa shukrani hizo leo
wakati akiongea na waandishi wa habari waliotaka kufahamu kuhusu
maendeleo ya afya yake.
“Namshukuru
Mwenyezi Mungu naendelea vizuri hali yangu siyo kama jana. Nilianza
kuumwa majira ya saa nane 8:30 mchana nikiwa nyumbani katika mazingira
magumu ambapo mapigo ya moyo yalipanda ghafla nikapelekwa Hospitali ya
Amana na baadaye Muhimbili kitengo cha Huduma ya dharula majira ya saa
12jioni kisha nikaletwa hapa”.
“Kwa
namna ya pekee nawashukuru sana wafanyakazi wa Amana, Muhimbili na
Taasisi ya Moyo ambao wamenipokea na kunipa huduma nzuri na kama
mnavyoniona afya yangu inaendelea vizuri tofauti na nilivyokuja jana”.
alisema Mhe. Zungu.
Aidha
Mhe. Zungu aliwataka watanzania kujiunga na mfuko wa Taifa wa Bima ya
afya ambao hata yeye ni mwanachama kwa kuwa mwanachama wa mfuko huu
kutawasaidia kupata matibabu pindi watakapoumwa bila ya kutoa
fedha mfukoni.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alisema
hali ya Mhe. Zungu inaendelea vizuri tofauti na walivyompokea
jana. Hivi sasa madaktari wako katika uchunguzi wa matatizo ya Moyo
baada ya hapo watajuwa tatizo na kumpatia tiba na anaamini baada ya
siku tatu zijazo anaweza kuruhusiwa.
“Kipindi
cha nyuma viongozi wenye matatizo kama haya walikuwa wanapelekwa nje
ya nchi kwa ajili ya matibabu hivi sasa Serikali imeboresha huduma za
matibabu ya Moyo hivyo basi wagonjwa wengi wanatibiwa hapa nchini”,
alisema Prof. Janabi.
Aliwashauri
wananchi kupima afya zao japo mara moja kwa mwaka, wakiona dalili za
viashiria vya ugonjwa wa Moyo waende haraka Kituo cha Afya kilichopo
jirani kwa ajili ya matibabu.
Prof.
Janabi alimalizia kwa kuwasisitiza wananchi kufanya mazoezi na kula
vyakula sahihi na kwa upande wa wagonjwa wa Moyo wanatakiwa kumeza dawa
kipindi chote cha maisha yao wasiache kunywa dawa kwani wagonjwa wengi
wanaorudi kupata matibabu ni wale walioacha kumeza dawa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇