LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 21, 2016

JK AKUTANA NA RAIS HAGE GEINGOB WA NAMIBIA, SWAKOPMUND JANA

Na Mwandishi Maalum
Rais Mstaafu na Kamishna wa Kamisheni ya Kupendekeza Namna Bora ya Kugharamia Fursa ya  Elimu  Duniani  ( Education Commission on Financing Global Education Opportunity) Dk. Jakaya Kikwete, jana Desemba 20, 2016, amekutana na Rais wa Namibia,  Hage Geingob alipomtembelea mapumzikoni huko Swakopmund, Namibia.

Katika nafasi yake ya Mjumbe Maalum wa Kamisheni hiyo, Rais Mstaafu amemkabidhi  Rais Hage Geingob Ripoti ya Kamisheni hiyo yenye mapendekezo ya namna Dunia inavyoweza kukabili janga la Elimu kwa kuwekeza katika Mpango wa Kizazi cha Elimu (A Learning Generation). Mpango huo unalenga kuleta mapinduzi makubwa ya Elimu katika nchi zinazoendelea ndani ya Kizazi Kimoja  (miaka 30). Azma kuu ya Mpango huo ni kuwezesha ifikapo mwaka 2040, watoto wote kote duniani wawe wanapata elimu iliyo sawa, na kwa kiwango cha ubora unaolingana dunia nzima.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa sasa, hali ya elimu katika nchi zinazoendelea inalingana na ile ambayo nchi zinazoendelea zilikuwapo miaka 70 iliyopita. Aidha, ripoti inasisitiza kuwa, ikiwa nchi zinazoendelea zitaendelea kwa kasi ya sasa, itazichukua nchi hizo kati ya miaka 90 na 110 kufikia viwango vya sasa vya nchi zilizoendelea. Aidha, ripoti inatahadharisha kuwa takribani ajira bilioni 2 zitakufa ifikapo mwaka 2050 kutokana na maendeleo ya teknolojia, ambapo asilimia 70 ya kazi hizo ziko katika nchi zinazoendelea. Hivyo, nchi zinazoendelea zinapaswa kuangalia upya aina ya elimu na stadi zinazotolewa ili kuendana na wakati ujao.

Kwa ajili hiyo, Kamisheni inapendekeza njia mpya na bora za kufanya mageuzi katika elimu ikiwemo kuongeza usimamizi, kupanua fursa, kuingiza ubinifu na teknolojia na kuongeza uwekezaji katika elimu kwa kushawishi ushiriki wa Jumuiya ya Kimataifa na Sekta Binafsi. Iwapo mapendekezo hayo yatatekelezwa, nchi zinazoendelea zinaweza kufidia pengo hilo ndani ya miaka 30 ijayo. Rais Mstaafu ameiomba Namibia kujiunga na Mpango huo.

Rais Mstaafu amempongeza Rais Geingob kwa mafanikio makubwa ambayo Namibia imeyapata katika sekta ya elimu ikiwemo kugharamia elimu kwa kiwango cha kati ya asilimia 25-30 ya bajeti, uwekezaji mkubwa kwenye elimu ya ufundi na matumizi ya teknolojia katika kufundishia. Kwa mujibu ya Ripoti ya Kamisheni, endapo itafanya mageuzi yanayopendekezwa, Namibia ina uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kuwa na Kizazi cha Elimu ifikapo mwaka 2040.

Kwa upande wake, Rais Geingob amepokea kwa furaha taarifa hiyo na kuelezea nia na dhamira ya nchi yake ya kujiunga na Mpango wa Kizazi cha Elimu. Ameelezea kuwa pamoja na mafanikio makubwa, changamoto bado ni kubwa kutokana madhara ya historia ya nchi hiyo
 iliyopitia kipindi kirefu chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Ziara hiyo imefikisha nchi ambazo zimeshafikiwa na ujumbe wa Kamisheni kuwa tano ambazo ni Uganda, Malawi, Ethiopia, Msumbiji na Namibia.
Rais Wa Namibia Hage Geingob akiipitia Ripoti ya Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu aliyokabidhiwa jana na Rais Mstaafu wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete, yenye Mapendekezo Mahsusi kwa nchi ya Namibia

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages