LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 1, 2016

RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AFUNGA MAADHIMISHO YA MIAKA 52 YA JWTZ WILAYA YA BAGAMOYO

RAIS JOHN POMBE MAGUFULI AKIPIGA NGOMA WAKATI AKIFUNGA MAADHIMISHO YA MIAKA 52 YA JWTZ JANA WILAYA YA  BAGAMOYO
 
Na  Nassir Bakari

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli,  tarehe 30 Septemba, 2016 amefunga maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kushuhudia zoezi la medani liitwalo ''Amphibious Landing'' lililofanyika katika Kijiji cha Baatini Wilaya ya Bagamoyo. Mkoani Pwani.

Zoezi hilo lililochukua muda wa wiki mbili, limeshirikisha kamandi zote tano za JWTZ  ambazo ni Nyika, Majini, Anga, Kamandi ya Makao Makuu na  Jeshi la Kujenga taifa limefanyika katika ufukwe wa bahari ya Hindi na limetekelezwa kwa mfano wa mapambano ya kivita yaliyohusisha kutua nchi kavu kutoka majini na kukomboa eneo lililotekwa.
 
Akizungumza baada ya kukamilika kwa zoezi hilo Rais na Amiri jeshi Mkuu Dkt.John Pombe Magufuli amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange pamoja na Makamanda na Wapiganaji wote wa JWTZ walioshiriki katika zoezi hilo ambalo limefanywa kwa umakini, uhakika na weledi wa hali ya juu.
 
''Kwa kweli nimefurahi na nimeamini tuna wapiganaji wa kutosha katika maeneo yote, hii mikakati na mipango iliyotumika inaonesha tuna jeshi imara na linaloaminika'' amesema Dkt. Magufuli.  
 
Rais na Amiri Jeshi Mkuu amewahakikishia Makamanda na Wapiganaji wote wa JWTZ kuwa Serikali yake itahakikisha inaendeleza na kuongeza zaidi juhudi zilizofanywa na Marais waliopita kwa kuimarisha na kuwa na jeshi la kisasa linalotumia vifaa na teknoljia ya kisasa na pia itahakikisha maslai ya askari yanaboreshwa.
 
Aidha, Dkt. Magufuli ametaka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuimarishwa zaidi na kujielekeza katika uzalishaji mali ikiwemo uwekezaji katika viwanda.
 
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye pamoja na kuipongeza  JWTZ amesema miaka 52 tangu kuanzishwa kwa Jeshi hilo Watanzania wanashuhudia jeshi lao likiwa imara na makini zaidi kwa ajili ya kulinda nchi.
 
Nae Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange amemshukuru Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli kwa jitihada zake na nia yake ya kuliimarisha Jeshi na kuboresha maslai ya Makamanda na Wapiganaji na ameongeza kuwa anajivunia kuwa kiongozi  wa Jeshi hilo.
 
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Viongozi wengine wakiwemo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar Abdulhamid Yahaya Mzee.
 
Rais na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli, amemuagiza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Davis Mwamunyange kuwapa ajira za JWTZ askari mgambo wote walioshiriki zoezi la Amphibious Landing.
 
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam.
30 Septemba, 2016

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages