Rais Dk Magufuli |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 07 Oktoba, 2016 amekutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani ambapo pamoja na mambo mengine ametaka utekelezaji wa diplomasia ya uchumi utiliwe mkazo katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jijini Dar es Salaam, imesema, katika
Mkutano huo uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Makamu wa
Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Rais
Magufuli aliyehutubia na kuongoza majadiliano juu ya masuala mbalimbali ya
shughuli za mabalozi, amesema Tanzania imeweka dhamira ya kuikuza sekta ya
viwanda kutoka ukuaji wa asilimia 7.3 hadi kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka
2021 na kuzalisha ajira kwa asilimia 40.
"Sasa
nimeona niwaite waheshimiwa Mabalozi ili tuelewane, mjue mwelekeo tunaoutaka na
mjue ni namna gani mtakavyoshiriki kuhamasisha uwekezaji wa viwanda.
"Nataka
badala ya kubaki mmejifungia ofisini, mtoke mwende mkawatafute wawekezaji waje
wawekeze katika viwanda ili nchi yetu inufaike kwa watu wetu kupata ajira,
Serikali kukusanya kodi na tuinue maendeleo yetu" Taarifa hiyo imemnukuu Rais Magufuli.
Imesema, maeneo
mengine ambayo Rais Magufuli ametaka Mabalozi wayafanyie kazi ni kutangaza na
kuwavutia watalii kuja hapa nchini, kufanyia kazi fursa zote zenye manufaa kwa
Tanzania katika nchi wanakowakilisha, kulinda mali za nchi zilizopo katika nchi
hizo na kufuatilia utekelezaji wa mikataba ya biashara na uwekezaji inayofanywa
kati ya Tanzania na nchi wanakowakilisha.
Pia
Rais Magufuli amewataka waheshimiwa Mabalozi wote kufanya kazi kwa juhudi,
kuondoa kasoro za utendaji kazi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa katika ofisi zao
na kubana matumizi ya fedha yasiyokuwa ya lazima.
Dkt.
Magufuli ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
kujipanga na kudhibiti mianya yote ya matumizi mabaya ya fedha za umma ambazo
zimekuwa zikitumika katika safari za nje ya nchi na matumizi mengine yasiyo ya
lazima, pamoja na kuhakikisha watumishi wote ambao wapo katika ofisi za ubalozi
kwenye nchi mbalimbali bila sababu za msingi wanarejeshwa nchini ili kupunguza
mzigo wa gharama kwa Serikali.
"Kuna
wafanyakazi wapo kwenye Balozi zetu wakati hata sifa za kuwa katika nafasi
wanazoshikilia hawana, ilifika mahali mtu akiharibu hapa nyumbani anapangiwa
ubalozini.
"Wakati
mwingine unakuta ubalozi wa Tanzania kwenye nchi fulani una idadi kubwa ya
wafanyakazi kuliko mahitaji ya ubalozi huo, haiwezekani"
amesisitiza Rais Magufuli.
Hata
hivyo Dkt. Magufuli amewapongeza Mabalozi wote wa Tanzania kwa kazi
wanazozifanya kwenye nchi wanazowakilisha na amewahakikishia kuwa Serikali ina
matumaini nao na inawategemea kuwa wataendelea kuiwakilisha na kuitangaza
vizuri Tanzania.
Mkutano
huo pia umehuduriwa na Viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri,
Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama,
Viongozi wa Taasisi mbalimbali na Wakurugenzi wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇