MKURUGENZI WA MANISPAA YA UBUNGO MH. JOHN KAYOMBO AKIONYESHA BOKSI LILILOKUWA NA DAWA ZA BINADAMU ZILIZOTUPWA KWENYE BONDE MPIJI MAJOHE, NJE KIDOGO YA JIJI LA DAR ES SALAAM. |
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo, John Kayombo ameitia matatani kampuni ya Indepth Scientific kwa kutupa kiholela dawa za binadamu zilizokwisha muda wake.
Mkurugenzi Kayombo, ameitia matatani kampuni hiyo, baada ya kufika kwenye dampo lisilo rasmi amabalo lipo karibu na chanzo cha maji ambayo hutumiwa na wananchi katika eneo la Mpiji Majohe, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Dawa hizo za kutibu binadamu zilimwagwa na kampuni hiyo yenye ofisi zake Mikocheni, Dar es Salaam, Octoba 3, 2016, na kusababisha hali mbaya ya hewa kwa wakazi wa eneo hilo
Akizungumza wakati wa tukio hilo Mkurugenzi Kayombo alisema amesikitishwa na kitendo cha kampuni hiyo kumwaga dawa kwenye makazi ya watu.
“Nimesikishwa sana na hili lililojitokeza sijafahamu lengo lenu haswa ni nini, hapa kuna makazi ya binasamu na pia kuna chanzo cha maji huu ni uuaji,” alisema Mkurugenzi Kayombo.
Pia alisema atatoa adhabu kali kwa kampunin hiyo ili wengine wasiige na kusisitiza kuwachukulia hatua stahiki kwa jambo hilo.
“Polisi waliwakamata wafanyakazi wawili wa kampuni hiyo ambao ni Mzee Ali na Amosi na kukaa mahabusu saa 24 na jana ndio tumewatoa, sitaishia hapo nitatoa adhabu kali ili iwe fundisho,” alisema Mkurugenzi Kayombo na kuendelea,:-
“Watalipa faini kwa mamlaka husika na pia waongee na wananchi wa eneo hili na maeneo ya jirani waangalie namna gani ya kulimaliza tatizo hili,” alisema Mkurugenzi Kayombo.
Baadaye alimtaka Meneja wa kampuni hiyo ahakikishe dawa hizo zinatolewa ndani ya masaa mawili na kuzipeleka mahala zinapotakiwa.
Wakati huo huo Meneja wa Kampuni hiyo Risper Monyagi aliwaomba radhi wakazi wa maeneo hayo na kusema hawatarudia tena kufanya kitendo hicho.
“Tunaomba mtusamehe hatumwagi tena dawa huku, tutatafuta eneo linalotakiwa, poleni sana kwa mliopata matatizo kwa namna moja au nyingine na tunaahidi kutoa hizi dawa ndani ya masaa mawili,” alisema Monyangi.
Pia wananchi wa eneo hilo walisema watashirikiana na serikali katika shughuli zote za maendeleo na kutoa taarifa linapotokea jambo la kinyume na maadili.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇