NA AUGUSTINO CHIWINGA |
HAKI YA DHAMANA KWA MSHTAKIWA
Dhamana inamaanisha uhuru wenye masharti apewao mtuhumiwa au mshitakiwa wakati shauri lake likiendelea kupelelezwa, likiendelea kusikilizwa mahakamani au likisubiri matokeo ya rufaa yake.
Katiba ya Tanzania inaeleza wazi kuwa kila mtu anastahili kuwa huru kwani binadamu wote wamezaliwa huru na wote ni sawa. Katika katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 13(a) b imeeleza kwamba kila mtu ni hana kosa hadi hapo atakapothibitishwa na mahakama kuwa ni mhalifu.
Hii hali ya kuonekana kutokuwa na makosa mbele ya sheria inaleta msingi mwingine wa haki za asili za kimsingi ambazo zinasema mtu asihukumiwe bila ya kusikilizwa.
Vile vile kila mtu anastahili kutambuliwa na kuheshimiwa utu wake. Kwa kutambua kanuni hizi za msingi Katiba imeendelea kusisitiza yakuwa ili kuhakikisha watu wote wako sawa mbele ya sheria, mamlaka ya serikali inapaswa kuweka taratibu nzuri na ambazo zitazingatia kuwa mtu yeyote anayeshtakiwa kwa kosa la jinai hapaswi kufanyiwa kama vile ameshatiwa hatiani kwa kosa aliloshtakiwa.
Maelezo haya ya Katiba yana maana kwamba, mshitakiwa anatendewa kama mtu asiye na hatia hadi pale mahakama itakapothibitisha kosa lake. Ili kukazia msimamo huu, sheria inatoa msingi kuwa mtu asiadhibiwe kabla hayapewa haki ya kusikilizwa utetezi wake.
Kwa hali hiyo, kuwepo kwa utoaji wa dhamana kwa mshitakiwa ni kuendelea kuheshimu haki yake ya kuwa huru hadi atiwe hatiani kwa kosa analoshitakiwa. Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai imefafanua taratibu zote za utoaji wa dhamana na masharti yake.
Dhamana ni Haki na Siyo Upendeleo
Kwa kuwa dhamana ni haki ya mtu, hivyo anapoomba hapaswi kukataliwa bila sababu za msingi. Mahakamani na wanaharakati wa haki za binadamu wamesisitiza mara nyingi kuwa dhamana ni haki ya mshitakiwa pale anapotimiza masharti yake; kumnyima bila sababu ni kumkosesha haki ya msingi ya kuwa huru kwa mujibu wa sheria. Vile vile polisi au mahakama inapokataa kutoa dhamana ni lazima kuwe na sababu nzito zenye kuridhisha kabla ya kufikia uamuzi huo.
AINA ZA KESI AMBAZO HAZIWEZI KUWEKEWA DHAMANA
Sheria ya mienendo ya makosa ya jinai imeorodhesha aina ya makosa ambayo hayawezi kuwekewa dhamana.
Sheria ya mienendo ya makosa ya jinai imeorodhesha aina ya makosa ambayo hayawezi kuwekewa dhamana.
Makosa kama hayo ni kama yafuatao;
1.Makosa ya uhaini;
2.Wizi wa kutumia silaha ;
3.Kesi za mauaji.
VYOMBO VYENYE MAMLAKA YA KUTOA DHAMANA
Kutoa dhamana ni wajibu wa kisheria ambao unapaswa kufanywa kwa kuzingatia misingi na kanuni za sheria kwa hali hiyo siyo kila mamlaka inaweza kutoa dhamana.
Dhamana ya Polisi
Kwa ujumla kuna dhamana zitolewazo na Polisi na kuna zile zitolewazo na mahakama. Dhamana ya polisi hutolewa kwa mtuhumiwa aliyeko chini ya ulinzi na mkuu wa kituo cha polisi ambapo mtuhumiwa anashikiliwa.
Kwa ujumla Polisi wanapaswa kumwachia mtuhumiwa baada ya kujidhamini mwenyewe kwa maandisi au kudhaminiwa na wadhamini wanaoaminika ikiwa: mtuhumiwa alikamatwa pasipo hati ya kumkamata mshitakiwa; au ikiwa baada ya upelelezi imebainika kuwa hakuna ushahidi wa kutosha; au ikiwa mashitaka yake siyo ya makosa makubwa; au ikionekana kuwa upelelezi wa ziada unahitajika na kwamba hauwezi kukamilika ndani ya saa ishirini na nne tangu kukamatwa mtuhumiwa.
Dhamana ya Mahakama
Dhamana ya Mahakama ni dhamana inayotolewa na mahakama baada ya mshitakiwa kusomewa mashitaka yake na kukana kosa.
Dhamana ya Mahakama ni dhamana inayotolewa na mahakama baada ya mshitakiwa kusomewa mashitaka yake na kukana kosa.
Kisheria dhamana hii ina lengo la kumruhusu mtuhumiwa kuwa nje ya mahabusu hadi pale mahakama itakapotoa hukumu. Dhamana hii huweza kutolewa na Jaji au Hakimu. Mahakama Kuu ya Tanzania ndiyo iliyo na uwezo wa mwisho wa kuamua kutoa dhamana au kutokutoa kwa yale makosa ambayo sheria inaruhusu dhamana.
Kwa hali hiyo madhumuni ya dhamana ni kwamba hata kama mtu ameshitakiwa kwa kosa la jinai bado ana haki zake zote za kimsingi kwani bado hajathibitika kisheria kutenda kosa hilo.
Kwa kusema kuwa dhamana ni haki ya mshitakiwa ina maana kuwa pale mshitakiwa anaposhitakiwa anayo haki ya kuwekewa dhamana ila kuna mazingira yanayoweza kusababisha mshitakiwa asipewe dhamana kama vile kuhofia kuvuruga ushahidi , kulinda maisha ya mtuhumiwa, upatikanaji wa mtuhumiwa.
AINA ZA DHAMANA
Kuna aina mbali mbali za dhamana kama zifuatazo:
Dhamana ya Mkataba wa Maandishi
Huu ni mkataba wa maandishi anaoandikiana mshitakiwa au mdhamini na mahakama na itakapotokea kuwa mshitakiwa atashindwa kuhudhuria mahakamani katika siku iliyopangwa mdhamini atapaswa kutimiza masharti fulani fulani ambayo yakuwa yameelezwa kwenye mkataba Mara nyingi sharti linalopaswa kutekelezwa ni mdhamini kutoa kiasi fulani cha fedha. Hii ni ahadi atakayokuwa ameitoa katika mkataba huo.
Huu ni mkataba wa maandishi anaoandikiana mshitakiwa au mdhamini na mahakama na itakapotokea kuwa mshitakiwa atashindwa kuhudhuria mahakamani katika siku iliyopangwa mdhamini atapaswa kutimiza masharti fulani fulani ambayo yakuwa yameelezwa kwenye mkataba Mara nyingi sharti linalopaswa kutekelezwa ni mdhamini kutoa kiasi fulani cha fedha. Hii ni ahadi atakayokuwa ameitoa katika mkataba huo.
Dhamana ya Utambulisho
Hii ni aina ya dhamana ambayo inafanana na ile ya mkataba wa dhamana, ila katika dhamana hii ni mtu mmoja tu ndiye anayetakiwa kuweka sahihi yake.
Kama saini itawekwa na mshitakiwa, mdhamini hana haja tena ya kuweka saini yake, vivyo hivyo kwa mdhamini.
Dhamana ya aina hii inaelezea ahadi ya kulipa ambapo mara nyingi, malipo hayo hufuata baada ya kushindwa kutekeleza masharti fulani yaliyowekwa.
Kwa hiyo aina hii ya dhamana ni ahadi ya kulipa, ni wajibu wa kulipa unaoibuka baadaye pale masharti fulani yaliyoelezwa ndani ya mkataba huu yanapokuwa hayajatimizwa.
Masharti ya aina hii ya dhamana ni mepesi zaidi kuliko yale ya mkataba wa maandishi.
Kuomba Dhamana kwa Kuweka Fedha
Hii ni aina ya dhamana ambayo mshitakiwa, ndugu au rafiki huweka kiasi fulani cha fedha mahakamani. Hivyo mahakama badala ya kumtaka mshitakiwa aingie kwenye mkataba, huwa inaamuru mshitakiwa aweke kiasi fulani cha fedha, na kutoa ahadi kuwa kama mshitakiwa hataonekana siku ya kusikilizwa kesi, fedha hizo zitachukuliwa na serikali.
Pamoja na kuwa mtu yeyote anaweza kutoa fedha mahakama inaweza kuagiza kuwa fedha hizo zitolewe na mshitakiwa mwenyewe na inapaswa kufanywa hivyo. Mara nyingi aina hii ya dhamana huitwa dhamana ya fedha taslimu.
Dhamana ya Mali
Kama mshitakiwa hana fedha, mahakama itamtaka aweke vitu kama dhamana yake. Hii dhamana inawasaidia wale ambao hawana fedha ila wana vitu vyenye thamani kuviweka vitu hivyo kama dhamana.
Vitu au vifaa vitakavyowekwa ni vile ambavyo mshitakiwa anavimiliki au vinamilikiwa na mdhamini wakati anaomba dhamana, viwe ni vitu visivyoondosheka. Vitu kama pasi ya kusafiria, leseni za udereva, hati za nyumba huweza kuwekwa kama dhamana ingawa si mara nyingi sana kwani mshitakiwa anapokiuka masharti unatokea ugumu wa kutaifisha vitu hivyo.
Iwapo vitu vya thamani vinawekwa kama dhamana thamani yake inapaswa kueleweka katika maandishi.
ANAYERUHUSIWA KUOMBA DHAMANA
Dhamana inaweza kuombwa na mtuhumiwa mwenyewe au wadhamini wake. Kama dhamana itaombwa wakati mshitakiwa amekwisha hukumiwa, yaani wakati rufaa imewasilishwa, ni lazima iombwe na mtu mwingine, yaani wakili wa mshitakiwa au mtu mwingine.
Hivyo kama mshitakiwa yupo rumande mtu mwingine yeyote yule anaweza kumwombea dhamana. Hakuna njia maalum ya kuomba dhamana bali itatosha tu pale mshitakiwa au wakili wa mshitakiwa atakaposema kuwa anaomba mshitakiwa apewe dhamana.
Siyo lazima mshitakiwa awepo wakati wa kuomba dhamana ila kama anayeomba ni mshitakiwa, basi lazima awepo wakati wa kuomba dhamana.
Wakati/Muda wa Kuomba Dhamana
Dhamana inaweza kuombwa wakati shitaka linatengenezwa au muda wowote kabla ya hukumu kutolewa. Kabla ya kuomba dhamana lazima kwanza kuwepo na mashitaka ya kusikilizwa Ni haki ya mshitakiwa kupewa hati ya mashitaka kwani huisaidia kufahamu mshitakiwa anashtakiwa kwa kosa gani na vilevile hufafanua kwa undani kosa anapoweza kuomba dhamana.
Mara nyingi baada ya mshitakiwa kusomewa shitaka na kujibu, kabla ya kuahirisha kesi hakimu humtamkia mshitakiwa kuwa dhamana ipo wazi na masharti ya dhamana ni yapi.
Kukubali Kosa na Athari Zake Kwenye Dhamana.
Kama mshitakiwa baada ya kusomewa hati ya mashitaka anakiri kutenda kosa, dhamana inaweza pia kutolewa katika kipindi cha kukiri kutenda kosa na kutiwa hatiani au kuachiwa.
Kama mshitakiwa anang’ang’ania kukiri kosa mahakama inamhukumu moja kwa moja na suala la dhamana halitakuwepo tena hata baada ya kufafanuliwa kwa kina kosa lenyewe.
Kupewa dhamana Dhamana inaweza ikatolewa na mahakama yaani na hakimu, jaji, au mkuu wa kituo cha polisi mtuhumiwa alipowekwa.
Hii itatokea baada ya jaji au mkuu wa kituo cha polisi kujiuliza maswali kadhaa iwapo atampa mshitakiwa dhamana, Je! Mshitakiwa atahudhuria kesi yake au la. Uamuzi wa kutokutoa dhamana utoke kwa hakimu au jaji mwenyewe na siyo vinginevyo
Mambo ya Kufanya Maombi ya Dhamana Yanapokataliwa
Kama mtu hatapewa dhamana katika mahakama za chini mshitakiwa itabidi awasilishe maombi ya dhamana Mahakama Kuu.
Kama mtu hatapewa dhamana katika mahakama za chini mshitakiwa itabidi awasilishe maombi ya dhamana Mahakama Kuu.
Hii ni kwa sababu mahakama za chini na mahakama kuu zinatofautiana kingazi lakini zina uwezo sawa katika suala la dhamana Maombi ya dhamana mahakama kuu siyo rufaa. Ila ni maombi yanayotokana na kukataa kwa mahakama ya chini kutoa dhamana au kuweka dhamana yenye masharti magumu. Kwa hiyo atakachokuwa anafanya mshitakiwa ni kuandaa upya maombi ya dhamana na kuyapeleka mahakama kuu na siyo kukata rufaa.
Maombi kama haya hupelekwa mahakama kuu kwani ndio yenye uwezo kubadili maamuzi ya mahakama za chini au hutoa dhamana pale mahakama za chini zitakapokuwa zimekataa kutoa.
VIKWAZO NA MASHARTI YA DHAMANA
Dhamana ni haki ambayo upatikanaji wake unategemeana na jinsi mshitakiwa alivyofuata taratibu na masharti yaliyowekwa na sheria.
Kwa kawaida vipingamizi vya kumnyima mshitakiwa dhamana hutolewa na waendesha mashitaka wa serikali na mara nyingi vipingamizi hivyo hutolewa mara tu mshitakiwa anapoomba dhamana.
Vipingamizi vya kumkatalia mshitakiwa asipewe dhamana havina budi kuwekwa kabla mshitakiwa hajapata dhamana, kama akishapewa dhamana hivyo havitakuwa vizuizi tena ila huweza kutumika kama sababu za maombi ya kufuta dhamana iliiyowekwa.
Vipingamizi dhidi ya maombi ya dhamana vyaweza kuwa kimoja kati ya vifuatavyo, baadhi yake au hata vyote kwa pamoja: (a) (b) (c) (d) (e) (f) Kama mshitakiwa ataachiwa kwa dhamana, ataingilia na kuharibu ushahidi na pia atavuruga uchunguzi wa polisi kwenye kesi; Kama mshitakiwa ataachiwa kwa dhamana atafanya kosa kama lile aliloshitakiwa nalo au kosa jingine lolote la jinai; Mshitakiwa siyo raia wa nchi hii na ana vitu vyenye thamani katika nchi nyingine; Mshitakiwa anaishi mpakani karibu sana na nchi jirani na kwamba akipewa dhamana anaweza kutoroka na kuingia nchi nyingine; Mshitakiwa hana sehemu maalum ya kuishi; Uzito wa kosa analoshitakiwa mshitakiwa iwapo ni zito na iwapo atatiwa hatiani adhabu kali itatolewa, ni rahisi kwa mshitakiwa kushawishika kutoroka.
Sababu hii ndiyo inayofanya mshitakiwa dhidi ya mauaji, wizi wa kutumia silaha, kupatikana na madawa ya kulevya na uhaini kukataliwa dhamana kutolewa na ukali wa adhabu atakayopewa mtu pindi atiwapo hatiani ambayo ni kifo, kifungo cha maisha au cha muda mrefu.
Ili mshitakiwa apewe dhamana ni lazima awe na mdhamini au wadhamini. Mdhamini ni mtu mbali na mshitakiwa ambaye hukubaliana na Mahakama husika kwamba endapo mshitakiwa hatafika mahakamani kujibu mashitaka aliyopangiwa na Mahakama, atawajibika kutekeleza masharti aliyoahidi kwenye maombi ya dhamana kama ilivyopangwa na Mahakama. Aidha, mdhamini huihakikishia Mahakama kwamba atasaidia katika kutimiza azma ya kumfikisha mshitakiwa mahakamani kujibu shitaka lake.
Endapo mtuhumiwa hatafika kujibu shitaka kama ilivyokubaliwa, basi mdhamini atawajibika kulingana na masharti yaliyokuwa katika dhamana iliyotolewa. Vilevile, mpewa dhamana (mshitakiwa) hutakiwa kusaini hati maalum ya kuonyesha atatii masharti yote ya dhamana.
Hati hii ya utiifu hueleza kwamba endapo mshitakiwa hajafika mahakamani kujibu shitaka kama ilivyopangwa, atawajibika kulipa kiwango fulani cha fedha mahakamani. Kwa hiyo mdhamini hujifunga kwa kuihakikishia mahakama husika kuwa mshitakiwa.
MAMBO YA KUZINGATIA
Siyo kila mtu anaweza kumdhamini mtu hivyo lazima yafuatayo yazingatiwe: Mwenye kumdhamini mshitakiwa lazima awe ni mtu wa kuaminika; Uwezo wa Mahakama kutoa dhamana umewekwa na sheria kwa hiyo mahakama haina budi kuzingatia misingi ya sheria katika kutekeleza wajibu wake kuhusiana na dhamana; Ikumbukwe:
Mahakama inapaswa kuhakikisha kwamba misingi ya haki na kanuni za sheria ya jinai hazikiukwi katika kutoa au kukataa kutoa dhamana. Isipokuwa pale sheria inapotamka vinginevyo, dhamana ni haki ya kikatiba ya mtuhumiwa kwa utaratibu uliowekwa na sheria kwa hiyo mtuhumiwa ana haki ya kuomba dhamana wakati wowote kabla hajapatikana na hatia.
MUAANDAAJI.
AUGUSTINO CHIWINGA
LEGAL OFFICER.
PHONE: 0756 810804
E-MAIL. augustino162@gmail.com
AUGUSTINO CHIWINGA
LEGAL OFFICER.
PHONE: 0756 810804
E-MAIL. augustino162@gmail.com
Nimeipenda hii na ndio maana nazidi kukiamini chama cha mapinduzi
ReplyDelete