LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 21, 2016

JUMUIYA YA KIMATAIFA YAPITISHA AZIMIO KUHUSU WAKIMBIZI NA WAHAMIAJI

Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano  wa 71  wa Baraza Kuu la  Umoja wa Mataifa,  Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri Augustine Mahiga (Kulia), akipewa taarifa  na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa  Balozi Tuvako Manongi kuhusu   majadiliano ya Baraza Kuu la 71 yaliyoanza  jana, Septemba  20 pamoja na mikutano  ya pembezoni  ambayo kiongozi  huyo  wa ujumbe wa Tanzania atapashwa kuhudhuria  na kushiriki  ikiwa ni pamoja na kulihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.  Mkutano huo  ulihudhuriwa pia na  Balozi  Wilson Masilingi, Balozi wa Tanzania Nchini Marekani  pamoja na   Maofisa  kama wanavyoonekana pichani
Na  Mwandishi Maalum, New York
Viongozi Wakuu wa Nchi na  Serikali, jana  ( jumatatu) wamepitish tamko la kwanza la aina yake linalolenga pamoja na  mambo mengine kuichagiza  jumuiya ya kimataifa kushirikiana katika  kukabili   wimbi  kubwa la wakimbizi na wahamiaji.

 Kupitia  Tamko hilo  ambalo linatambulika kama Tamko la New  York, linazitaka serikali za mataifa  yote, bila kuingilia uhuru wa mambo yao  kama mataifa  huru au  ukiukwaji wa sheria za kimataifa, kuwapokea, kuwahifadhi na kuwapatia huduma za kijamii wakimbizi na  wahamiaji bila ya kujali hadhi  zao.

Ni  tamko ambalo  limetokana na majadiliano ya muda mrefu baina ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa,  Asasi za kiraia na Mashirika ya Kimataifa,  majadiliano ambayo  wakati  mwingine  ililazimu  wajumbe kukubaliana  kutokukubaliana katika baadhi ya   vipengele vya tamko hilo.

 Upitishwaji wa Tamko hilo la New York kuhusu wakimbizi na wahamiaji   umefanyika  ikiwa na sehemu ya   uliokuwa mkutano wa siku moja uliojadili  changamoto kuhusu wakimbizi na  wahamiaji  ambao idadi yao imezidi kuongeza na  kubwa kuwahi kutokea.

Kwa mfano, takwimu zinaoonyesha kwamba, mwaka 2015 idadi ya wakimbizi na wahamiaji ilifikia watu milioni 224, ongezeko ambalo kasi yake ni kubwa kuliko ongezeko la idadi ya  watu duniani.

Hata hivyo inaelezwa pia  kwamba kuna takribani  watu   65 milioni ambao wamelazimishwa kuhama, wakiwamo zaidi ya wakimbizi milioni 21, milioni tatu  wanaotafuta hifadhi na zaidi ya milioni 40 wakiwa ni wakimbizi wa ndani.

Wakuu wa  Nchi na  Serikali pamoja na  wakuu wa   Mashirika  na  Taasisi za   Kimataifa,  wanaahidi kupitia tamko hilo la New York , pamoja na mambo mengine, kulinda haki za  binadamu  za wakimbizi na  wahamiaji wote bila ya kujali hadhi yao. Ikiwa ni pamoja na haki za wanawake na wasichana pamoja na kukuza fursa yao ya kushiriki kikamilifu katika   kutafuta suluhu.

Wameahidi pia kuzuia vitendo vya  ukatili wa kingono na udhalilishaji dhidi ya wanawake. kuhakikisha kwamba watoto wakimbizi na wahamiaji wanapata elimu mara tu wanapofika nchi ya ugenini.

Vile vile  tamko hilo, linashauri na kupendekeza  nchi ambazo zimekuwa  ama zikipokea wakimbizi na kuwahifadhi  au zile ambazo ni  njia  wanayopitia   kwenda  nchi nyingine   basi zisaidiwe  katika   ubebaji wa jukumu hilo.

Tamko hilo pia  linataka kukomeshwa kwa tabia ya  kuwaweka vizuizini watoto ili kubaini hadhi yao ya uhamiaji. Linataka pia kutafutiwa makazi wakimbizi wote ambao wanatambuliwa na Kamisheni ya Umoja wa  Mataifa kuhusu wakimbizi kuwa  wanaohitaji makazi,  pamoja na kuwatafutia fursa  za kuhamia nchi nyingine.

Katika kuhakikisha   changamoto  ya wakimbizi na  wahamiaji linashughulikiwa katika ukamilifu wake, Umoja wa Mataifa umeamua katika  mkutano  huo wa Jumatatu kuiingiza rasmi Shirika la Kimataifa la  Wahamiaji ( IOM)  kuwa chini ya mfumo wa  Umoja wa Mataifa.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani,  Barack  Obama,  ameeitisha siku  ya  jumatano Mkutano wa  Viongozi kuhusu  Wakimbizi. ( Leaders’ Summit on Refugees) . Katika  mkutano huo viongozi wakuu wa nchi na serikali walioalikwa  watatarajiwa  kutoa ahadi zao kuhusu namna serikali zao zitakavyo wasaidia wakimbizi.

Tanzania ni  kati ya nchi zilizoalikwa kuhudhuria na kushiriki mkutano huo. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika  Mashariki, Mhe. Augustin Mahiga ( Mb) anayeongoza ujumbe wa Tanzania  katika Mkutano wa  71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Anatarajiwa kuwasilisha ahadi ya  Tanzania katika Mkutano huo.


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages