TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu wanahabari,
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa majonzi na
masikitiko makubwa sana taarifa ya kushambuliwa na kuuawa kwa askari wa jeshi
la Polisi wakiwa katika kutekeleza majukumu yao ya ulinzi eneo la Mbande, Temeke
jijini Dar Es Salaam.
CCM tayari imemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa
Jeshi la Polisi IGP Ernest Mangu pamoja na familia za marehemu waliofikwa na
umauti katika tukio hilo baya katika historia ya nchi yetu.
Tunalaani tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi
kuvipa ushirikiano wa kutosha vyombo vya dola ili kufanikisha wahusika wa tukio
hilo kusakwa popote pale na kupatikana ili wafikishwe mbele ya vyombo vya
sheria haraka.
Serikali ya Chama Cha Mapinduzi itaendelea
kuhakikisha amani ya Taifa letu inalindwa dhidi ya wachache wanaofurahia
madhila kwa wananchi wetu. Wananchi wetu wanapenda, wamezoea na wanastahili
amani. Ndio maana Tanzania imekuwa nchi ya kupigiwa mfano, ikionesha uongozi
katika maeneo mengi. Tuendelee kuilinda taswira hii.
MAFANIKIO YA AWAMU YA TANO
Ndugu wanahabari,
CCM inachukua nafasi hii kumpongeza Rais Mhe Dkt John
Pombe Magufuli na Serikali yake kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika
muda mfupi wa uongozi wake.
Rais Magufuli aliahidi mabadiliko. Tunampongeza kwa
kusimamia vema utekelezaji wa ilani ya CCM. Katika muda mfupi wa miezi tisa tu,
Rais Dk Magufuli amefanya mambo makubwa.
Sote tunafahamu kuwa Shirika letu la Ndege, ATCL,
limekuwa linafanya kazi na ndege moja. Serikali ya Dk Magufuli imekwisha lipia
ndege tatu za abiria toka Canada, ndege mbili zitaingiza nchini mwezi ujao.
Reli ya kati inajengwa kwa kiwango cha Standard Gauge. Meli katika ziwa
viktoria inanunuliwa ktk bajeti ya mwaka huu. Elimu ya msingi na sekondari
inatolewa bure. Wanafunzi wetu sasa wanakalia madawati na kujifunza vizuri
zaidi. Barabara zimeendelea kujengwa. Makusanyo ya kodi yameongezeka. Huduma za
jamii zinaendelea kuimarika. Lakini pia, nidhamu katika utumishi wa umma sasa
imeimarika. Wananchi wanastahili huduma nzuri na kuthaminiwa na wafanyakazi wa
Umma.
Mataifa mengi ya Afrika na nje ya Afrika yanaiga
mbinu za Rais wetu katika kuleta mabadiliko nchini mwao. Hapa Kenya tu, Waziri
mmoja wa Elimu anayesifika kwa utendaji kazi mzuri, anajiita “MAGUFULI.” Hata
Australia, baadhi ya wananchi waliwahi kumtaka Waziri Mkuu wao afanye kazi kama
Dk Magufuli.
Dk. Magufuli ameazimia kujenga uchumi wa viwanda.
Ifikapo mwaka 2025, Tanzania itakuwa nchi yenye uchumi wa kati. Maisha ya
wananchi wetu yataboreka. Vijana wetu wapate ajira katika viwanda, watauza
malighali na mahitaji mbalimbali ya viwanda. Wakulima watapata masoko ya bidhaa
zao katika viwanda hivyo. Kilimo kitaongezeka thamani kutokana na mahitaji
mbalimbali ya viwanda vyetu. Hatua za
kuelekea huko tayari zimechukuliwa.
Wapo wachache wanaelekea kutafuta mbinu
chafu za kuhujumu mafanikio haya, lakini hawatafanikiwa. Watanzania wamemchagua
Dk Magufuli ili awaletee maendeleo.
Serikali ya CCM, itawasaidia vijana wa Tanzania kuendesha
uongozi wa Taifa lao. Kamwe tusikubali ndoto ya kuongoza mapinduzi haya makubwa
kwa ajili ya Taifa na Bara letu ikapokonywa na watu wachache wasiokuwa na dira
ya kuliletea maendeleo Taifa letu. Tuwapuuze.
UPINZANI KUSUSIA VIKAO VYA BUNGE
Ndugu Wanahabari,
Bunge kama ilivyo kwa mhimili mingine linaongozwa
kwa katiba, sheria na kanuni katika mijadala na maamuzi yake. Kama Mbunge hajaridhika
na maamuzi ya Spika, Naibu Spika au Mwenyeki wa kikao, kuna taratibu za
kufuata. Utaratibu wa kikanuni ni kuulalamikia uamuzi huo kwa Katibu wa Bunge. Wakiwa
wanafahamu taratibu za kikanuni, kama kawaida yao, WAPINZANI, waliamua
kuzisigina na badala yake wakataka Naibu Spika aondolewe.
Hivyo wakaratibu kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Naibu Spika. Ambapo suala
hilo lilipelekwa kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Kutokana
na kutokuwepo kwa Spika nchini, hoja hiyo haikufikia ukomo. Tunamshukuru Mungu
afya ya Spika imeimarika. Sasa hoja hiyo huenda itafikishwa katika mkutano wa
Bunge litakalokaa mwezi ujao.
Kana kwamba hiyo haitoshi, kama kawaida yao,
hawakuwa na subira ya kufuata taratibu. Wakaamua kufanya kihoja. Wakaamua kutohudhuria
vikao vyote vya Bunge vilivyokuwa vikiongozwa na Naibu Spika.
Na hata walipoingia Bungeni waliziba midomo yao na
kuamua kutowasalimia wabunge wenzao wa CCM, kutopeana mikono na hata kutohudhuria
misiba na sherehe zao. Vitendo vyao hivi ndivyo vimeasisi chuki ndani ya jamii
yetu iliyozoea UPENDO, UDUGU, UMOJA NA MSHIKAMANO. Watanzania tunafahamika na
tunaona fahari kuishi kama ndugu.
Baada ya kitendo hicho cha kuwasaliti wapigakura wao
kulaaniwa kila kona ya nchi, sasa wamekubali kutumiwa kama vibaraka kuichafua
taswira ya nchi yetu, nao kwa hila iliyo wazi, wamekubali kuwafitinisha
watanzania kwa kuandaa maandamano ya nchi nzima, yasiyo na ukomo. Hatua hii ni
uvunjaji wa katiba ya nchi, Sheria na inalenga kuvunja amani, utulivu na
mshikamano wa watu wetu.
Ileleweke kwamba, wanachokifanya hawa CHADEMA ni
kuchochea wananchi kwa makusudi kutotii maagizo halali ya vyombo vya dola na Serikali
kwa visingizio mufilisi kuwa katika Katiba imewapa uhuru huo. Katika haitoi
haki na uhuru usio na ukomo. Ibara ya 29 (5) inasema;
“Ila watu wote waweze kufaidi haki na uhuru
vinavyotajwa na katiba hii kila mtu ana wajibu wa kutenda na kuendesha shughuli
zake kwa namna ambayo haitaingilia haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya
umma”
Baada ya kusema hayo, ninaomba CHADEMA wakumbuke na
kutilia maanani kuwa kila haki ina wajibu na hakuna haki au uhuru usiokuwa na
ukomo hususani pale inaposababisha kuingiliwa ama kukatizwa kwa haki na uhuru
wa watu wengine. Rejea ibara ya 30 (1) na (2) ya Katiba.
Ndugu wahabahari,
Mwisho tunatoa pole kwa wenzetu wa CUF kutokana na
mapambano huko kwao. Tumestushwa sana na yanayoendelea huko. CCM inawapa pole
na tunawatakia maelewano ili waje tusaidiane kuwaletea watanzania maendeleo.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇