LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 21, 2016

BUNGE LA BURUNDI LAPINGA AZIMIO LA UMOJA WA MATAIFA KUPELEKA POLISI NCHINI HUMO

Picha: Kikao cha Bunge la Burundi
------------------
BURUNDI
Wabunge wa Burundi wamepinga azimio nambari 2303 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kukataa kabisa suala la kutumwa nchini humo askari polisi 228 wa kimataifa.

Katika kikao chake cha jana, Bunge la Burundi lilipinga azimio hilo la Baraza la Usalama na kutangaza kuwa uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa hauendani na mtazamo wa serikali ya Bujumbura.

Wabunge wameeleza kuwa uamuzi wa kutaka kutuma kikosi cha askari polisi nchini Burundi umechukuliwa bila ya kushauriana na serikali ya nchi hiyo.

Taarifa ya Bunge la Burundi inasema, katika mpango huo haikuzingatiwa na kutiliwa maanani hali ya kisiasa na kiusalama ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa azimio hilo ambalo lilipendekezwa na Ufaransa, askari polisi 228 wa Umoja wa Mataifa watatumwa nchini Burundi kwa shabaha ya kurejesha amani na kulinda haki za binadamu nchini humo kwa kipindi cha mwaka mmoja. Muda wa huduma za kikosi hicho utaongezwa iwapo hali itakuwa mbaya zaidi. 


Kulia, Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia limeihimiza serikali ya Burundi kufanya mazungumzo na makundi yote ya upinzani wakiwemo wapinzani walioko nje ya nchi kwa lengo la kukomesha mgogoro wa ndani ya nchi hiyo. 
Azimio hilo la Baraza la Usalama limekabiliwa na upinzani mkubwa wa wananchi huko Burundi na ripoti zinasema kuwa, maandamano dhidi ya Ufaransa ambayo ndiyo iliyopendekeza muswada wa azimio hilo, bado yanaendelea.

Msemaji wa serikali ya Burundi, Philippe Nzobonariba ametangaza kuwa, suala la kutumwa askari polisi wa Umoja wa Mataifa nchini humo ni kinyume na sheria za kimataifa zinazolinda mamlaka ya kujitawala nchi wanachama.

Kabla ya hapo Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi alikuwa amesema kwamba, kutumwa askari wa kimataifa nchini humo ni kuingilia masuala ya ndani ya Burundi na kwamba nchi yake itakabiliana nao kama wavamizi.


Wapiznani wa Mkurunziza
Mgogoro wa ndani nchini Burundi unaendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na juhudi za kikanda na kimataifa za kujaribu kukomesha machafuko na ghasia nchini humo bado hazijazaa matunda. Machafuko hayo yalishika kasi baada ya kiongozi wa sasa wa nchi hiyo kutangaza kuwa atagombea kiti cha rais kwa mara ya tatu hapo mwaka jana. Suala hilo lilipingwa na vyama vya kisiasa vya upinzani vikisema ni ukiukaji wa katiba na makubaliano ya amani ya Arusha. 


Machafuko ya ndani Burundi
Hali hiyo imezidisha machafuko ya ndani kwa kadiri kwamba, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, serikali ya Bujumbura imezidisha mateso na unyanyasaji dhidi ya wakosoaji na wapinzani wake. Vilevile ripoti zinasema kuwa askari wa Burundi wanahusika na visa vingi vya kuwabaka na kuwanajisi wanawake wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama. 


Maiti ya mtu aliyeuawa Burundi
Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Mateso, Jens Modvig ameeleza wasiwasi wake kuhusu machafuko ya kikabila nchini Burundi na kusema: Ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa, manyanyaso na mateso nchini Burundi yanafanyika kwa sababu za kisiasa na kwamba ukatili unaofanyika dhidi ya makundi ya kisiasa na kikabila unapinga kengele ya hatari ya kuanza mauaji ya kimbari nchini humo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages