Na
Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, imesema, waathirika wa
dawa haramu za kulevya wanatakiwa kusaidiwa badala ya kuwafunga jela.
Hayo yameelezwa
jana ( Alhamis) na Balozi Tuvako
Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, katika Mkutano
Maalum wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
uliokuwa ukijadili mafanikio, juhudi na changamaoto za kukabiliana
na tatizo la dawa
za kulevya duniani.
Balozi Manongi
ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano
huu wa siku tatu na ambao umewashirikisha Viongozi Wakuu
wa Nchi, Serikali na Mawaziri kutoka mataifa mbalimbali.
“Tunapoangalia
mbele, mkazo wetu uwe katika kuhakikisha
tunapunguza idadi ya watu wanaojihusisha na matumizi ya
dawa haramu za kulevya na tunapunguza idadi ya watu wanaofariki kutokana
na matumizi ya dawa hizo” akasema Balozi
Na kusisitiza “ Lazima tuhakikishe wale wenye
makosa madogo hawaishii jela ambako
matatizo yao yatokanayo na dawa za kulevya yatazidi kuwa makubwa zaidi. Lakini pia tunao wajibu wa
kuhakikisha huduma wanazopewa
zinazingatia afya na haki za binadamu.”
Mwakilishi huyo
wa Tanzania, amewaeleza washiriki wa
mkutano huo kuwa Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengine Tanzania haijapona na balaa hilo la dawa za
kulevya.
“Tanzania
hatujasalimika na balaa hili, nchi yetu,
imekuwa sehemu ya kupitisha dawa za kulevya kuelekea nchi nyingine.
Lakini kiasi fulani cha dawa hizo kina baki nchini
na hivyo kuathiri wananchi wetu
ambao wengine wao tayari wameshaathirika kwa umaskini na matatizo mengine”.akaeleza Balozi
Akasema, ni
kweli kwamba, tatizo la dawa za kulevya, ni kubwa na lenye changamoto nyingi, na ni tatizo ambalo halina ufumbuzi wa mara moja, lakini pia ni tatizo
ambalo lisiifanye jumuiya ya kimataifa
kukata tamaa.
Akasema Jumuiya
ya Kimataifa inatakiwa kupitia mkutano huo
kuhakiksha kwamba inakuja na mikakati
mipya ikiwa ni pamoja na kutekeleza yale
yaliyopendekezwa kwenye tamko lililopitishwa kwenye mkutano huo.
Balozi
Manongi ameongeza kuwa hapana shaka sera na
sheria zilizopo hivi sasa zimeshindwa kudhibiti wimbi la athari za dawa
za kulevya. Na kwa kutambua ukubwa na
changamoto za tatizo hilo na athari zake kwa wananchi wa Tanzania , Serikali
imejiwekea mipango na mikakati mbalimbali
ya kulikabili.
Baadhi ya mikakati hiyo ni pamoja na kuwasaidia waathirika wa dawa za
kulevya na ambao wapo katika hatari
kubwa ya kuambukizwa na kuambukiza magonjwa mbalimbali yakiwamo ya
virusi vya ukimwi na Hepatitis B na
C,
Akaelezea pia juhudi
zinazofanywa na serikali katika utungaji
na uboreshaji wa sheria zinazolenga kuwabana wasafirishaji, wauzaji na
wasambazaji wa dawa hizo, ikiwamo
mikakati ya kufuatilia kwa makini mwenendo mzima wa biashara ya dawa za kulevya , matumizi
na matumizi ya madawa mengine ya aina hiyo.
Balozi Manongi amesema pia kwamba tatizo la dawa za
kulevya linarudisha nyuma juhudi za pamoja na kuwapatia watanzania maisha yenye hadhi na inaathiri nguvu kazi ambayo inahitajika
kufikia malengo ya kiuchumi na maendeleo ya jamii.
“ Kama hiyo haitoshi dawa za kulevya
zinachochea uhalifu na vitendo vya jinai vikiwamo vinavyohusisha ujagili
wa wanyamapori na misitu, na kuongeza kazi ya ziada kwa vyombo vya sheria na mfumo
wa kitaifa wa utoaji huduma za afya”.
Amesisitiza Balozi
Katika vita hivyo dhidi ya dawa za kulevya na umuhimu wa kuwasaidia waathirika, Balozi Manongi amesisitiza kwamba ushirikiano wa
pamoja baina ya mataifa, taasisi za
kimataifa na asasi zisizo za kiserikali unahitajika sana kwa kile alichosema hakuna
nchi inayoweza kukabiliana na
tatizo hilo peke yake.
Akaongeza pia
kwamba utekelezaji wa mikataba
mbalimbali ya kimataifa, utasaidia
sana katika kuyakabili makundi na mitandao ya kihalifu na rushwa.
Hoja
zilizopewa msisitizo na wazungumzaji
wengi ni pamoja na hiyo ya kuwapatia waathirika matibabu na kutowafunga
kwa kile walichosema hakuna mzazi anayependa kuona mtoto wake akifungwa na
badala yake angefurahi kuona anasaidiwa.
Pamoja na kuzungumzia adhabu ya kuwafunga waathirika wa
dawa za kulevya, wazungumzaji wengi pia wamepinga au kukemea adhabu ya kuwanyonga wanaokamatwa kuhusika na
masuala ya mihadarati.
Aidha viongozi
wengine walieleza kwamba wameanza
mikakati ya kuwapatia wananchi wao hasa maskini utalaamu wa kulima mazao
mbadala badala ya kutegemea kulima mazao yanayotumika kutengeneza dawa
za kulevya kama sehemu ya kuendesha
maisha yao.
Wengine
wameeleza juhudi ambazo serikali zao zinafanya katika
kukabiliana na mitandao na magenge wafanyabiashara wa dawa za kulevya
, juhudi zinazohusisha pia kukamata na
kutaifa mali zao.
Wako
waliokwenda mbali Zaidi kwa kutaka nchi ambazo kwa namna moja ama nyingine
zimelegeza sheria zao na kuruhusu
matumizi ya dawa za kulevya kama vile bangi basi nazo ziwajibike kwa kutoa
ushirikiano na kuonyesha utashi wa
kisiasa.
Marais wanaotoka
katika nchi ambazo zimeathirika zaidi na biashara za dawa za kulevya na mitandao ya
kihalifu inayojihusisha na biashara
hiyo, walikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa, ikiwa
nchi zilizoendelea na ambazo ni
wadau wakubwa hazitaonyesha ushirikiano ni wazi kwamba vita dhidi ya dawa za kulevya itashindikana.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇