Katibu wa kamati maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Bi, Waride Bakar Jabu akiwafariji wahanga wa mafuriko katika kambi ya mwanakwere Zanzibar.
Kambi ya kipindupindu iliyopo Chumbuni Zanzibar.
Na Mwandishi Wetu,
Zanzibar.
CHAMA chama cha
Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka wananchi kuendelea kufuata kanuni na
taratibu zinazotolewa na wataalamu wa kiafya
ili kujikinga na maambukizi ya maradhi ya kipindupindu yaliyopo nchini.
Wito huo umetolewa na
Katibu wa Kamati Maalum NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Waride Bakar Jabu katika ziara ya
kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa wa Kipindupindu wa kambi iliyopo Chumbuni
Zanzibar, alisema endapo wananchi watafuata kanuni za kiafya itasaidia kutoweka
ugonjwa huo kwa haraka.
Waride alisema CCM
itaendelea kutoa misaada ya hali na mali kwa wagonjwa wa kipindupindu ili
kusaidia serikali huduma za uendeshaji kwa wagonjwa hao.
“ Tunawaomba wananchi
waendelee kuweka mazingira yao katika hali ya usafi sambamba na kutumia maji
salama, vyoo kuwa visafi na wagonjwa wenye dalili za maradhi hayo kupelekwa
haraka katika kambi za kipindupindu.
Pia CCM inawapa pole
wananchi wote waliopata maradhi ya kipindupindu na kuwasihi waendelee kuwa
wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha matibabu yao.”, alisema Bi, Waride na
kuzisihi taasisi zingine za serikali na binafsi kutoa misaada kwa wagonjwa hao
kwani maradhi ya Kipindupindu hayana itikadi za kisiasa bali yanawapata wananchi
wote.
Aliwashauri wanawake
nchini ambao ni walezi wa watoto na mama wa nyumbani kuacha tabia ya kutupa
ovyo pempasi za kuwafungia watoto kwani nazo ni miongoni mwa vitu
vinavyopelekea kuenea kwa maradhi ya kipindupindu nchini.
“ Wanawake tukumbuke kuwa
kila janga lolote sisi pamoja na watoto ndiyo waathirika wa mwanzo hivyo lazima tuwe makini katika kuweka mazingira
yetu katika hali ya usafi pia tusitupe pempasi ovyo bali tuziweke katika sehemu
zinazostahiki.” Alisisitiza Waride.
Naye Daktari dhamana wa
Wilaya ya Magharibi Unguja ambaye pia ni Mkuu wa Kambi ya Kipindupindu Chumbuni
Zanzibar, Ramadhan Mickdad Suleiman ameshukru msaada uliotolewa na CCM na
kuahidi kuutumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Akitoa takwimu za hali
ya maambukizo ya ugonjwa huo kwa sasa, Mickdad alisema ya hali ya maambukizo
kwa sasa imepungua kutoka wagonjwa 40 kwa siku hadi 21 wanaolazwa katika kambi
hiyo.
Alisema hali hiyo
imetokana na utekelezaji wa agizo la
Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein alipowaagiza wananchi wanaofanya
biashara za vyakula na vinywaji kuacha kuuza kwa muda ili kudhibiti kupunguza
kasi ya maambukizi ya kipindupindu.
Alifafanua kuwa mpaka
sasa kambi hiyo tayari imeshapokea wagonjwa 2026 waliopatiwa matibabu na kupona
na wakaondoka na kati ya hao wamefariki wagonjwa 43 mpaka sasa.
“ Tunaishauri jamii
kudumisha usafi wa vyoo na kula vyakula na maji vilivyokuwa salama kwani
ugonjwa huu unaambukizwa kwa kasi katika maji ya kunywa yenye bakteria wa kipindupindu
ama kumgusa maiti yaliyekufa kwa ugonjwa au kugusana na mtu aliyeambukizwa
kipindupindu.”, alisema Bi, Micjdad.
Aliwaomba wananchi
wenye uwezo pamoja taasisi binafsi na serikali kutoa misaada kujitokeza kutoa
misaada mbali mbali ya kuwasaidia
wagonjwa wa maradhi hayo waliopo katika kambi hiyo.
Mapema Waride
alitembelea na kuwafariji Wahanga wa
mafuriko waliopo katika kambi ya Shule
ya Mwanakwerekwe “ C” Unguja, aliwapa
pole kwa matatizo yaliyowafika na kuwaomba waendelee kuwa wavumilivu katika
kambi hili huku serikali ikiendelea kutafuta mbinu za kuwasaidia ili wapate
makaazi katika sehemu salama.
Alitoa wito kwa
wananchi wanaoishi katika sehemu za mabonde na sinazojaa maji wakati wa msimu
wa mvua za maska kuhama haraka kabla hawajapata athari za kukumbwa na mafuriko
hayo.
Kwa upande wake Katibu
mkuu wa Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar, Joseph Abdallah Meza alitoa
shukrani kwa uongozi wa CCM kwa msaada wao wa kuisaidia kambi hiyo yenye
wananchi zaidi 400.
Alisema serikali bado
inaendelea kuwahudumia wananchi hao ambao wamepata maafa ya mafuriko na kupoteza
makaazi yao hivyo bado panahitajika misaada mbali mbali ya maji na vyakula
pamoja na huduma za kibinadamu.
Misaada iliyotolewa na
CCM katika ziara hiyo ina thamani zaidi ya shilingi milioni tano (5) kwa upande wa kambi ya kipindupindu Chumbuni
ni pamoja na Maji ya kunywa, Dawa za Chroline, Sabuni za kufulia na kuogea,
viatu vya mvua, dawa ya choo na mashine za kufukizia dawa Sprayers.
Vingine vilivyotolewa katika kambi ya wahanga wa mafuriko iliyopo
Mwanakwere “C” ni pamoja na Pempasi za watoto, maji ya kunywa, sabuni za kuogea
na kufulia, sabuni za chooni na madaftari ya wanafunzi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇