Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limepitisha
azimio jipya ambalo pamoja na mambo mengine limeiongezea
kwa mwaka mmoja Misheni ya
kulinda Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( MONUSCO ).
Sambamba na kuiongezea
mwaka MONUSCO, Baraza la Usalama pia
limesitisha zoezi la kupunguza walinzi
wa Amani 1,700 kama ilivyopendekezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Huku
Azimio hilo likitamka bayana kuwa MONUSCO inatakiwa kuwa na walinzi wa Amani wasiopungua 19,815,
waangalizi 760, pamoja na polisi
1,050.
Ndani ya
MONUSCO kuna Brigedi maalum ijulikanayo
kama Force Intervention Brigade (FIB) yenye mamlaka nguvu ya
kuyashughulikia makundi ya waasi yenye silaha. Brigedi hii inaundwa na walinzi wa amani kutoka Tanzania,
Afrika ya Kusini na Malawi.
Kwa mujibu wa
Azimio hilo jipya lililopitishwa na
wajumbe 15 wa Baraza la Usalama,
uamuzi wa kuiongezea muda wa
mwaka mmoja MONUSCO hadi Machi 31,2017, pamoja na kutotoa baraka
za kupunguzwa kwa walinzi wa Amani
kunatokana na taarifa za kuzorota kwa
hali ya usalama hususani katika kipindi
hiki cha mpito kuelekea uchaguzi mkuu.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajiwa kufanya uchaguzi wa Rais
mwezi Novemba mwaka huu na tayari kuna taarifa za kuwapo kwa sintofahamu miongoni mwa makabila kutokana na tofauti za
kisiasa, kuongezeka kwa makundi ya waasi wenye silaha, kuzorota kwa hali ya kibinadamu hali inayoitia wasiwasi Jumuiya ya Kimataifa
kwamba kunauwezekano wa kutokea machafuko.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kupitia
Azimio hilo, limeionya Serikali ya DRC kuhusu kuchelewa kwa maandalizi ya uchaguzi wa rais, huku likitoa wito kwa
serikali wa kuwafikisha mbele ya mkono
wa sheria wale wote wanaotuhumiwa kuhusika na vitendo vya ukiukwaji wa haki za
binadamu, na makosa ya uhalifu wa kivita na ukatili dhidi ya binadamu.
Vile vile Baraza la Usalama limetoa wito kwa serikali
na wadau wengine pamoja na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi ( CENI) wa
kuhakikisha uwazi kuhusu mchakato wa
uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa kalenda ya uhakika ya uchaguzi.
Aidha serikali imetakiwa kutenga bajeti ya kutosha
kwaajili ya uchaguzi na kuweka maadili
ya uchaguzi na kuchukua hatua za kuboresha daftari la wapiga kura pasipo
kuchelewa.
Kuhusu makundi
ya waasi wenye silaha, wajumbe wa
Baraza la Usalama wametoa wito wa kutaka
kurejeshwa mapema iwezekanavyo operesheni ya
pamoja kati ya MONUSCO na Jeshi la DRC ( FARDC) dhidi ya makundi
hayo ya waasi hususani kundi la Democratic
Forces for the Liberation of Rwanda ( FDLR).Makundi mengine ya waasi na
ambayo yameendeleza matukio ya mauaji ya
raia wasio na hatia na ambayo pia yanatakiwa kushughulikiwa ni pamoja na kundi la ADF, Mai Mai na LRA
Azimio hilo
lenye kurasa 15 pia limetilia mkazo
kuhusu ulinzi wa raia, ulinzi wa watoto
na linakemea vikali
kuhusu vitendo vya udhalilishaji
wa kijinsia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇