SHERIA,
SHERIA, SHARIA
(Dr.
Muhammed Seif Khatib)
Labda tukubaliane kuwa kila jambo huwa na
utaratibu wake ili likamilike. Mfano
mzuri ni wa taratibu za mchezo wa
kabumbu au wengine huiita kandanda,
mchezo unaongozwa kwa kupendwa duniani. Una muda wake wa kucheza. Dakika tisini. Una idadi yake ya wachezaji, ishirini na
mbili. Wengine husema hata refaa naye ni
mchezaji. Unao mwamuzi na wasaidizi wake
wawili. Unao muda wa kupumzika. Lakini pia unao sheria zake za kuongoza
mchezo huo. Ingawa unaitwa mpira wa
miguu, lakini golikipa yeye anaruhusiwa kutumia mikono yake! Ingawa unaitwa mpira wa miguu, lakini
mchezaji akitumia kichwa kufunga goli
siyo kosa. Lakini lenye uzito zaidi ni kuwa mwamuzi ndiye
mwenye kauli ya mwisho akiwa uwanjani.
Kwa hali hii, wale wote wanaocheza mchezo huo hutakiwa wafate sheria,
kanuni na maamuzi ya mwamuzi. Na kwamba
maamuzi yake hayawezi kutenguliwa.
Hayo ndiyo yaliyojiri huko Zanzibar mwaka 2015
mwezi wa Oktoba. Ulikuwepo Uchaguzi Mkuu ambao ulishirikisha vyama vya
siasa ambavyo vina usajili wa kudumu.
Zipo taratibu za kuendesha uchaguzi unaohusika. Vyama
vya siasa na viongozi wake wote waliweka saini kukubali kushiriki katika
uchaguzi. Wote walikubaliana kuwa chombo
kinachosimamia ni Tume na siyo mtu aitwaye Jecha. Na kwa bahati mbaya ndani ya Tume wamo pia
wawakilishi wa vyama vikuu vya siasa vya Zanzibar. Nao wote walikubaliana kuwa Tume ndiyo
mwamuzi halali na kwamba uamuzi wake wowote hauwezi kuhojiwa na mtu yeyote au
mahakama yeyote. Aidha Tume haitakiwi kuingiliwa na mtu
yeyote. Si Sheikh si Askofi. Si Jaji si Rais.
Ni Tume huru Tume baada ya kutanabahi kuwa uchaguzi umefanyiwa hujuma,
takwimu za kura zimechezewa, wapiga kura
hasa Pemba wamenyimwa haki yao ya kupiga kura, ikaamua uchaguzi ufutwe. Baya na kubwa kuliko yote ni kule kwa mgombea
wa Rais mmoja kunyakua mamlaka ya Tume ya kujitangazia matokeo yake ya ushindi
wa urais. Hili ni kosa kubwa la kijinai
ambalo lingeweza kuzua maafa makubwa na kusababisha umwagaji wa damu. Huyu
aliyetenda kitendo hiki hapaswi kuacha bila mkono wa sheria kuchukua
mkondo wake. Zanzibar hakuna mgogoro na
wala hakuna kosa kwa mtu aitwaye Jecha.
Uchaguzi umefutwa na chombo halali. Uchaguzi umefutwa na Tume kwa kufata taratibu, kanuni
na sheria. Uchaguzi haukufika hatima yake hivyo hakuna mshindi wa Uraia wala
hakuna wawakilishi au madiwani. Utaratibu wa kutangaza mshindi wa urais wa Zanzibar
unajulikana. Mwenyekiti wa Tume anaweza
kwa Jecha au Mazurui, muhimu ni mamlaka siyo jina, nasaba au dini ya mtu. Mwenyekiti hakukamilisha kazi ya kukusanya matokeo
halali na kuyatangaza yote. Hivyo
hakupata jumla ya kura halali za
wagombea wote. Ili mgombea wa urais wa Zanzibar ashinde kihalali
yafuatayo yafanyike. Kura halali za wagombea wa urais zikusanywe zijumlishwe,
zihakikiwe na baada ya kuridhika, zitamkwe rasmi na Mwenyekiti wa Tume. Atamkwe rasmi nani ameshinda kwa kura
ngapi. Hilo bado halikufanyika. Pia aliyetajwa kama ameshinda apewe cheti cha
uthibitisho ya ushindi wake. Hakuna
aliyetajwa wala aliyepewa cheti cha uthibitisho wa ushindi. Hatua nyingine ingafata kwa aliyeshindwa ni
kuwekwa siku maalum ya kuapishwa huyu Rais mteule. Siku hiyo haikuwekwa kwa sababu Jaji hajapewa
jina la mgombea aliyeshinda. Hatua ya
mwisho ingekuwa Rais Mteule wa Zanzibar kuapishwa hadharani na Jaji Mkuu wa
Zanzibar. Nalo hilo halikufanyika kwa
vile hakuna mgombea urais aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Hivi basi kwa kufata taratibu na utawala wa
sheria uchaguzi wa Zanzibar haukufika mwisho.
Kurejewa siyo kosa, dhambi wala kuvunjwa kifungo chochote cha sheria au
Katiba. Urais ni kazi ya heshima. Ikulu ni pahapa patakatifu. Huwezi kukabidhi vitu hivi kwa mtu mmoja kinyume
na sheria. Utawala bora ni kufata sheria
na taratibu ambazo watu wenyewe wamejiwekea. Watu waungwana na wastaarabu
hufata sheria. Rudini Wazanzibar katika
uchaguzi ili muwapate viongozi halali akiwemo Rais. Sheria, sheria, sheria!
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇