Na
Mwandishi Maalum, New York
Wakati Tanzania ikipongeza, kusifu na kushukuru
uhusiano na ushirikiano wake na Umoja wa Mataifa kupitia Mifuko na Mashirika yake ya Maendeleo,
imeutaka pia Umoja huo kutekeleza
majukumu yake kwa kuzingatia, kanuni, taratibu, sheria na misingi iliyojiwekea
ili iendelee kujijenga heshima.
Hayo yameelezwa jana jumatatu na Mwakilishi wa
Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa
Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, wakati wa mkutano wa Bodi za Mashirika ya
Umoja wa Mataifa UNDP, UNFPA
na UNOPS. Tanzania ni mjumbe wa Bodi
katika Mashirika hayo.
Katika siku ya kwanza ya mkutano ,
mkutano uliofunguliwa na Mtendaji Mkuu wa UNDP, Bi Helen Clark, Balozi
Manongi amesisitiza kwamba, ili
Umoja wa Mataifa uendelee
kujijenga heshima na kuheshimika, unapashwa kutoruhusu watendaji wenye ajenda na maslahi binafsi kufanya kazi
katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa.
“ Umoja wa Mataifa wakati wote
umekuwa sehemu na mdau mkubwa
katika uimarishaji na ujenzi wa utawala bora katika nchi nyingi , Tanzania ikiwamo. Wajibu wa Umoja wa Mataifa utabaki
kuwa halali na wenye nguvu endapo wale ambao wamepewa dhamana ya kutenda kwa niaba yake watatambua
na kuheshimu imani na wajibu uliotukuka
ambao wamepwa kuutekeleza ” akasisitiza Balozi Manongi
Akaongeza kwamba, mashabiki
hawapaswi kupewa nafasi, wala kuvumiliwa
na kuwa sehemu ya miongoni mwa watendaji wa chombo hicho wasipewe nafasi, wala wasivumiliwe kuwa miongoni mwa watendaji wa chombo hicho.
Akizungumzia kuhusu rasimu
ya Taarifa ya Mpango wa Utekelezaji kuhusu
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Country report) kwa kipindi cha
2016-2021) ambayo imewasilishwa mbele ya Wajumbe wa Bodi wa UNDP, Balozi Manongi amesema, mapendekezo
yaliyomo kwenye rasimu na ambayo
imeshirikisha wadau mbalimbali inajumuisha mawazo na mapendekezo kutoka pande
zote za Muungano na imetokana na misingi
ya ushirikiano kati ya UNDP na Serikali ya Tanzania.
Vile vile akasema
rasimu hiyo imejumuisha vipaumbele
vinavyoainishwa katika Dira ya Taifa ya 2025 kwa upande wa Tanzania Bara , Dira ya
2020 kwa upande wa Zanzibar, mkakati wa
kupunguza umaskini kwa pande zote za Muungano pamoja
na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano.
“ Tunaishukuru UNDP- Ofisi
ya Tanzania kwa ushirikiano wake katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya
maendeleo ikiwano mikakati ya kupunguza
umaskini, ushirikiano huu umekuwa mzuri
ingawa unachangamoto zake” akasisitiza Balozi Manongi
Akaeleza kwamba,
kutokana na umuhimu wa mwaka huu wa 2016
ambao pamoja na mambo mengine ni kuanza kwa utekelezaji wa Agenda ya Maendeleo
Endelevu ( Agenda 2030) Tanzania itaendelea kushirikiana kwa
karibu na UNDP katika utekelezaji
wa Agenda hiyo huku mkazo ukiwa ni
katika kupungua ama kuondoa
umaskini uliokithiri kwa makundi ya mbalimbali ya jamii hususani wanawake.
Akasema , Serikali
imejipanga vema katika utekelezaji wa mipango mbalimbali inayolenga katika
kuboresha maisha ya wananchi wake. Ikiwa ni pamoja na kutatua tatizo la uhamaji wa wananchi wake
kutoka vijijini na kwenda katika
miji mikuu hususani vijana kwa lengo la kutafuta ajira na hali bora ya maisha.
Akasema kuwa wajibu
au madhumuni ya msingi UNDP ni kupunguza umaskini, ni kwa sababu
hiyo Tanzania ingependa kuiona UNDP ikijielekeza zaidi katika jukumu lake hilo
la msingi kama inavyoelekezwa
katika maazimio mbalimbali ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kwa upande wa ukusanyaji
na uchambuzi wa takwimu zinazohusu maeneo mbalimbali,
Balozi Manongi amesisitiza kwamba
UNDP inapashwa kufanya kazi kwa karibu na kwa ushirikiano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kile alichosema
ndicho chombo cha serikali chenye dhamana juu ya masuala yote
yahusuyo takwimu.
Na kwa sababu hiyo akasema
Tanzania inaridhishwa na taarifa ya kwamba UNDP itashirikiana na Ofisi hiyo ya Taifa ya Takwimu katika Nyanja mbalimbali zikiwamo za
uwezeshaji kwa lengo la kusaidia katika uhuishaji wa takwimu.
Aidha Tanzania
imesisitiza kuhusu umiliki katika uendeshaji na usimamizi wa miradi ya
maendeleo pamoja na kiushauri UNDP
kuhakikisha kwamba fedha zinazotengwa kwaajili ya miradi ya maendeleo zinakwenda kufanya kazi
iliyokusudiwa na si vinginevyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇