NA MWANDISHI MAALUM, NEW YORK
Mwishoni mwa wiki, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
lilijadili ajenda ya Afya na Sera ya Mambo ya Nje ambapo pamoja na mambo
mengine lilipitisha azimio linalotathmini utayari wa nchi wanachama kukabiliana
na magonjwa ya milipuko na dharura nyingine za kiafya.
Katika mjadala huo,
wazungumzaji wengi, walisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa mifumo ya afya,
hususan katika nchi za kipato cha chini na cha kati zisizo na uwezo wa kutosha
wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko. Wazungumzaji hao walieleza umuhimu wa
kung’amua mafunzo muhimu ya janga la ugonjwa wa Ebola uliosababisha maafa makubwa
katika nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia.
Akichangia katika
mjadala huo kwa niaba ya serikali ya Tanzania, Bw. Noel Kaganda, Afisa
Mwandamizi katika Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika Umoja wa Mataifa alisema kuwa pamoja na jitihada zilizolenga kuimarisha
sekta ya afya katika kipindi kilichomalizika cha utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo ya Milenia, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama
vile upungufu wa madaktari na wauguzi; vifaa finyu na vichakavu; na mazingira yasiyo
salama.
Aksisitiza kuwa, jitihada za kuboresha afya ya binadamu,
hususan ya akina mama na watoto, lazima ziendelezwe kwa ufanisi zaidi katika
muktadha wa Agenda ya Maendeleo Endelevu
hadi kufikia mwaka 2030.
Aliongeza kuwa pamoja
na kuzuia vifo vya watoto wachanga, ambavyo idadi yake ulimwenguni kwa mwaka
2015 imefikia milioni 6, sawa na vifo 16,000, jumuiya ya kimataifa haina budi
kuzijengea nchi zinazoendelea uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko kama
vile Ebola na mengineyo, ambayo yanaweza kuathiri jamii nyingi duniani kufuatia
kushamiri kwa utandawazi na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na binadamu.
Pamoja na kusisitiza
kuwa wananchi wote wapatiwe huduma bora za afya, Tanzania iliunga mkono
mapendekezo ya ripoti ya wa Shirika la Afya Duniani kuhusu ulinzi na ustawi wa
watumishi katika sekta ya afya.
Kwa mujibu wa ripoti
hiyo, watumishi wengi wa sekta ya afya wanadhalilishwa na kushambuliwa wakiwa
kazini na wanaathirika na majanga mengine kama vile Tsunami na matetemeko ya
ardhi. Tanzania ilisema kuwa vitendo hivyo vinachangia katika kuzorota kwa
sekta ya afya, hivyo ilitaka vikomeshwe mara moja. Pia ilipendekeza wahusika
wachukuliwe hatua kali za kisheria katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
Vilevile ilitaka
watumishi wa sekta ya afya wapatiwe mafunzo na zana za kujilinda na maambukizi,
ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo. Kadhalika ilisisitiza umuhimu wa
mashirikiano baina ya nchi wanachama na wadau wengine wa afya, kama vile
Shirika la Afya Duniani, yenye lengo la kuzijengea nchi zinazoendelea uwezo wa
kukabiliana na dharura za kiafya.
Taarifa ya Shirika la
Afya Duniani imekuja siku chache kabla ya jopo la Ngazi ya Juu lililoteuliwa na
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupendekeza namna bora ya kukabiliana na
magonjwa ya milipuko duniani. Jopo hilo linaloongozwa na Rais Mstaafu wa awamu
ya nne, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
linatarajia kuwasilisha taarifa yake mwezi Januari 2016.
Katika hatua nyingine,
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeazimia kufanya mkutano wa ngazi ya juu
kuhusu “antimicrobial resistance” kwa lengo la kubaini kiini cha magonjwa sugu
kama kama ilivyo kwa baadhi ya jamii za ugonjwa wa Kifua Kikuu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇