Na Mwandishi Maalum, New York
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya, anatarajiwa Ijumaa wiki hii, kueleza mbele ya wajumbe wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo ya kazi ya jopo hilo tangu kuundwa kwake.
Jopo la Ngazi ya juu kuhusu mwitiko wa Kimataifa wa majanga ya kiafya liliundwa mwezi wa nne mwaka huu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambapo Rais Kikwete amepewa jukumu la kuongoza jopo hilo.
Taarifa ambazo zimeufikia Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, zimebainisha kuwa Mhe. Rais atawazungumza wajumbe wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa tatu wa jopo hilo unaofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Wajumbe wengine wa Jopo hili ni Bw. Celso Amorim ( Brazil), Micheline Calmy ( Switzerland), Marty Natalegawa ( Indonesia) Joy Phumapi ( Botswana) na Rajav Shah ( USA).
Jukumu kubwa ya jopo hilo kwa mujibu wa hadidu za rejea, pamoja na mambo mengine, ni kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa katika kuzuia na kukabiliana na majanga ya kiafya ikiwa ni pamoja na kujifunza kuhusu mwitikio wa Jumuiya ya Kimataifa kufuatia kuibuka kwa janga la ugonjwa wa Ebola.
Katika utekelezaji wa majukumu yake Jopo limekuwa likikutana na kufanya majadiliano ya kina na makundi mbalimbali yakiwamo ya wataalamu, wawakilishi wa nchi tatu ambazo zimeathirika sana na ugonjwa wa ebola ( Liberia, Siera Leone na Guinea),Mashirika ya Kimataifa na Kikanda , Taasisi za Fedha za kimataifa, wahudumu wa Afya, Wasomi , Watafiti, Sekta Binafsi na wataalam wa fani na kada mbalimbali.
Pamoja na kuhudhuria na kuongoza mikutano ya Jopo, Mhe, Rais Kikwete akiwa hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, pia atahudhuria Mikutano Mikubwa miwili ambayo ni, Mkutano wa Kilele wa Kisiasa, ambao Wakuu wa Nchi na Serikali watapisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ( SDGs). Mhe. Rais atazungumza katika mkutano huu muhimu kwa mstakabali wa maendeleo na ustawi wa binadamu kwa miaka 15 ijayo.
Malengo Mapya ya Maendeleo yanachukua nafasi ya Malengo ya Maendeleo ya Millenia ( MDGs) yanayomaliza muda wake mwishoni mwa mwaka.
Aidha Mhe. Rais atashiriki na kuhudhuria Mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Na anaratajiwa kulizungumza Baraza Kuu na hii itakuwa ni hotuba yake ya mwisho akiwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vile vile Mhe. Rais atahudhuria mikutano mingine kadhaa. Baadhi ya mikutano hiyo ni ule ambao umeandaliwa kwa pamoja baina ya Kansela wa Ujerumani Mhe. Angela Merkel , Waziri Mkuu wa Norway Mhe. Erna Solberg na Rais wa Ghana Mhe. John Dramani Mahama.
Mhe Rais anahudhuria mkutano huu kwa mwaliko rasmi aliopewa na Kansela Angela Markel. Washirika na waandaji wengine wa mkutano huu ni Mfuko wa Bill na Melinda Gates, Shirika la Afya Dunia ( WHO) na Bank ya Dunia.
Mkutano huu unatarajiwa kuzindua misingi na hatua muhimu ambazo kwayo zitaratibu ufanisi na upimaji wa matokeo ya juhudi za kuimarisha mifumo ya afya.
Your Ad Spot
Sep 16, 2015
Home
Unlabelled
RAIS KIKWETE KUELEZEA UMOJA WA MATAIFA MAENDELEO YA KAZI YA JOPO ANALOLIONGOZA
RAIS KIKWETE KUELEZEA UMOJA WA MATAIFA MAENDELEO YA KAZI YA JOPO ANALOLIONGOZA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇