Na Mwandishi Maalum
Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula (Pichani), amewaaga watanzania waishio nchini Marekani, kwa kuwataka kujivunia utanzania wao na kutoionea aibu lugha yao ya taifa, Kiswahili.
Mwishoni mwa wiki, Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani, uliandaa hafla ya aina yake ya kumpongeza, kumshukuru na kumuaga Balozi Liberata Mulamula ambaye sasa ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Hafla hiyo iliyowajumuisha watanzania wa kada mbalimbali wakiwamo maafisa na wafanyakazi wa Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, wakiongozwa na Balozi Ramadhan Mwinyi, ilipambazwa kwa nasaha mbalimbali na salamu za kumtakia kheri Balozi Mulamula katika jukumu lake jipya.
Pamoja na kusikiliza salamu kutoka kwa wawakilishi wa makundi ya kijamii, na kupokea zawadi, Katibu Mkuu, Balozi Mulamula naye alipata fursa ya kuzungumza mawili matatu.
Katika salamu zake kwa watanzania waliojumuika katika makazi yake. Moja ya mambo muhimu aliyoyazungumza ni pamoja na kuwaasa watanzania waishio nchini Marekani, kujivunia utanzania wao, umoja wao na kubwa zaidi kutoona aibu kuizungumza na kuiendeleza lugha ya taifa Kiswahili.
“Niwaombeni jambo moja, msione aibu kuzungumza lugha yetu, lugha yenu ya Kiswahili, miaka kadhaa iliyopita watanzania waughaibuni walikuwa hawazungumzi Kiswahili , waliogopa kujitambulisha kwa lugha yao, lakini sasa hali imebadirika sana, unakutana na watanzania kila kona wanazungumza Kiswahili hili ni jambo la kujivunia sana na ninawaomba tuendeleze utamaduni huu wa kuzungumza Kiswahili, kuwa ugenini hakumaainishi uachane na lugha yako” akasisitiza Balozi Mulamula na kushangiliwa na watanzania.
Katika kutilia mkazo wa lugha ya Kiswahili, Balozi Mulamula aliwataka wana DMV kuendelea na darasa la kuwafundisha watoto lugha hiyo ya Kiswahili na maeneo mengine kuiga mfano huo.
Jambo jingine ambalo Balozi alililowasisitizia watanzania hao ni kuhusu upendo, mshikamano, kuheshimiana, kusaidia na kutobaguana kwa misingi ya dini, kabila, eneo ambalo mtu anatoka au kwa misingi ya itikadi za kisiasa.
“ Ninaondoka baada ya miaka miwili ya kuwa Balozi wenu, na katika miaka hii miwili nimejifunza mengi sana kutoka kwenu, mmeshirikiana nami na Ubalozi katika mambo mengi yakiwamo ya kuchangia maendeleo yenu wenyewe na maendeleo ya watanzania wenzenu endeleeni na moyo huu”.
Kaongeza “nitakuwa nanyi na kama mjuavyo tunakitengo kizima kinachoshughulia masuala ya diaspora, na kama ningekuwa mwanasiasa basi nyie wanadiaspora mngekuwa mtaji wangu, jimbo langu”. akabainisha na kuamsha tena vifijo kutoka kwa wana-diaspora hao.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu, Balozi Mulamula amewahimiza watanzania walioko nje, kumchangamkia hasa kwa wale wenyekutaka kujaza fomu za maombi ya pasi zao za kusafiria ambazo zimekwisha muda.
Your Ad Spot
Jul 28, 2015
Home
Unlabelled
BALOZI LIBERATA MULAMULA AWAAGA RASMI WATANZANIA WAISHIO MAREKANI
BALOZI LIBERATA MULAMULA AWAAGA RASMI WATANZANIA WAISHIO MAREKANI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇