*Hauna ubavu kuteua wagombea kupambana na CCM Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
*Prof. Lipumba ataweza kupumzika kugombea Urais mwaka huu na kumwachia mgombea wa Chadema?
*CUF wapo tayari kuwapa Chadema jimbo walau moja Pemba?
NA BASHIR NKOROMO
Licha
ya hali halisi kuonyesha wazi, kuna ambao bado wanaamini kuwa
'muungano' wa baadhi ya vyama vya upinzani unaiotwa UKAWA unaweza kuwa
nyenzo ya kuvifanya vyama hivyo vifanye vizuri katika Uchagu Mkuu
unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.
Ukweli ni kwamba hadi sasa
imeshadhihirika wazi kwamba muungano huo ambao chimbuko la lake ni
kilichoitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi ulioundwa na vyama kadhaa
vikiwemo Chadema, CUF na NCCR Mageuzi, mwanzoni mwa mchakato wa Katiba
mpya, ambao sasa umefikia hatua ya Katiba inayopendekezwa, hauwezi
kufua dafu.
Hii ni kutokana na sababu nyingi ikiwemo hali halisi
za kimazingira ya kisiasa ya vyama husika na vilivyounda Ukawa na asili
yenyewe ya kuanzishwa kwake huo Ukawa.
Kwa wale wanaofuatilia
mambo ya siasa za Tanzania, wanakumbuka namna ambavyo, Ukawa ulianza.
Harakati za mwanzoni kabisa zilianza kwa Chadema kususia bunge kwa
kutoka ukumbini mara kadhaa wakati wa vikao vya bunge la Katiba.
Ikumbukwe
pia kwamba wakati wa michakato kama hiyo ya Katiba hasa katika nchi za
Kiafrika, ndiyo wakati ambao baadhi ya Taasisi binafsi za kitaifa na
kimataifa hutafuta kutambuliwa uwepo wake, kwa kujitokeza zenyewe
kukosoa au kuchangia masuala mbalimbali kwenye mchakato na nyingine
kufanya hivyo kimya kimya.
Taasisi ambazo hujitokeza waziwazi
hizo ndizo kupewa nguvu hasa kifedha kutoka kwenye taasisi zile ambazo
kufanya kazi kimya kimya. na uchunguzi unaonyesha kuwa taasisi ambazo
hutoa fedha mara nyingi ni zile za nje ya nchi.
Mara kadhaa
imekuwa ikielezwa kwamba Taasisi ambazo hujiingiza katika michakato,
hufanya hivyo kwa lengo la kuimarisha Utawala Bora na uimarishaji
Demokrasia katika nchi inayokuwa katika pilika hizo za kutengeneza
katiba mpya.
Zipo taasisi ambazo hufanya hivyo kwa lengo hilo,
lakini nyingine kufanya kwa lengo la kuvuruga huku nyingine
zikijiingiza kwa kuwa viongozi wake huona kuwa ni msimu au fursa ya
kujipatia mamilioni ya fedha kutoka kwa 'wahisani'.
'Wahsani'
hao ndio wanaoaminika kuwa chanzo cha vyama Chadema, CUF na
NCCR-Mageuzi kuamua kuunda kilichokuja kuitwa UKAWA, kwa kuwa
'wahisani' hao inadaiwa waliwalazimisha kuungana na kwa kuwa inaelezwa
kuwa kulikuwa na fungu, Kina Freeman Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema)na
Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, wakalazimika kujaribu kuwa kitu kimoja
katika huo ukawa.
Usemi wa 'tumikia kafiri upate mradi wako'
ukatimia, wakamua kutoka kwa muda katika uhasama uliokuwepo wakati
Chadema ilipokuwa ikiishambulia CUF kuwa ni CCM B baada ya kukubali
kuingia katika Serikali ya Umoja Visiwani Zanzibar, hatimaye viongozi wa
vyama hivyo sasa wakakaa kwenye meza moja kwa kapu la Ukawa.
Kwa
hiyo, kulingana na mtazamo huo, Ukawa ni umoja unaonekana kuwa
ulianzishwa kwa lengo la kimaslahi ya viongozi wa vyama husika zaidi na
siyo kweli ya dhahiri kuwa lengo lilikuwa kupata kinachodaiwa kuwa ni
Katiba ya Wananchi.
Pamoja na kwamba dodoso zinaonyesha kwamba
Ukawa ulianzishwa kimaslahi zaidi, lakini bado pia Ukawa unaonekana
kutokuwa chombo cha maana kuweza kuwaunganisha wapinzani kufanya vizuri
Uchaguzi Mkuu kwa kuwa kuanzishwa kwake hakuhusiani na kuweza kufanya
kazi kwa uhakika wakati wa uchaguzi mkuu huo.
Japokuwa vyama
kadhaa vinavyotaka uongozi wa nchi huanza na harakati za Umoja, lakini
wakati siku zinazidi kuyoyoma bado viongozi wa vyama vinavyounda Ukawa
wameendelea kufanya bla bla tu, badala ya kujenga misingi
itakayowafanya asiwepo moja wapo wa kukiuka makubaliano kama yapo.
Mfano
mdogo ni wakati wa Uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa, ambapo vyama
vya upinzani vilitangaza kushirikiana kupitia Ukawa kwa kupishana
nafasi kwenye uchaguzi huo kulingana na nguvu aliyonayo mgombea wa
upinzani katika eneo mojawapo.
Lakini wakati wa matokeo, ilikuja
kuonekana kwamba yapo maeneo mengi ambayo kama Chadema na CUF peke yake
wangeachiana wangepata viti vingi. Lakini ilishuhudiwa kwamba kuna
maeneo mengi tu, CCM iliibuka na ushindi ambao usingeweza kupatikana
kirahisi kama kura za wagombea Chadema na CUF zingekuwa za mmoja wapo.
Na
unafiki unajidhihirisha zaidi pale, wanapotangaza viongozi wa Ukawa
hasa Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kwamba, katika Uchaguzi Mkuu,
mgombea wa upinzani atakayekuwa na nguvu zaidi ndiye atapitishwa peke
yake kugombea.
Hii ni hadidhi ngumu sana kufanyika ili iweze
kusimulika baadaye, kwanza kwa sababu ni vigumu dhana ya Umoja (Ukawa)
kushinda dhana ya chama wakati wa mchakato wa kupata wagombea, hivyo si
rahisi Ukawa ukaibuka kumwambia mgombea pengine wa CUF kuwa ni dhaifu
kwa mgombea wa Chadema au wa Chadema ni dhaifu kwa mgombea wa CUF
wakati kila mmoja amejipima kupitia wapambe wake akajiona ananguvu.
Ni
vigumu kwa nguvu ya Ukawa tu, kumshawishi mgombea wa chama fulani
ampishe wa chama kingine, tena kwa kumpa kigezo kuwa ameshindwa nguvu
na anayehitaji kupishwa. Hii ni ngumu sana kwa sababu kila mgombea
anajipima nguvu kutokana na wapambe wa chama chake, sasa itakuwaje
mgombea anaona wanachama wa chama chake wanamuunga mkono halafu umwabie
hatoshi, bora wa chama kingine?
Shughuli hii ya mgombea mmoja
kumpisha mwingie kwa kushindanisha nguvu inawezekana kufanyika ndani ya
Chama, kwa wagombea kushindanishwa nguvu na mwanachama mwenzake lakini
si ndani ya Umoja kama ulivyo Ukawa.
Kuthibitisha hili, unaweza
kurejea namna ambavyo huwa changamoto vyama kuchuja wagombea kupata
mmoja atakayepeperusha bendera dhidi ya wagombea wa vyama vingine. Licha
ya kuwepo taratibu sheria na utii ndani ya chama husika lakini kumpata
mgombea huyo huwa ni kazi ambayo huacha mashimo wakati mwingine ya
hatari sana ndani ya Chama.
Kila unapotajwa utaratibu wa
kupishana majimbo, lazima kutafakari kwamba CUF ndiyo bado kina nguvu
kubwa katika Kisiwa cha Pemba na majimbo yote kisiwani humo yapo chini
ya chama hicho, lakini wakati huo huo, CUF haina mbunge wa kuchaguliwa
hata mmoja Tanzania Bara, huku Chadema nao wakiwa hawana kiti hata
kimoja cha kuchaguliwa Zanzibar yote, lakini ndicho chama cha upinzani
chenye wabunge wengi Tanzania Bara.
Je, ikiwa hali ni hivyo
kupitia UKAWA, CUF wapo tayari kuwapisha Chadema waweke wagombea katika
majimbo walau mawili tu Pemba?, Au, kupitia Ukawa huo, Chadema wapo
tayari kuwaachia CUF kugombea katika majimbo walau matano Tanzania Bara
ambako wana nguvu?.
Kwa sababu ikiwa ni kufuata kigezo cha
mgombea kuwa na nguvu, hali itabaki kama ilivyo sasa, kwa kuwa mahali
ambako CUF wanakubalika Chadema haina chake, na kule Chadema
wanakokubalika, CUF hawana chao.
Na uzoefu kupitia chaguzi
zilizopita ni kwamba, pale ambako CUF inakubalika mgombea wa Chadema
amekuwa akipata kura za chini sana, na hali kadhalika pale ambako
mgombea wa Ubunge wa Chadema anapokubalika wa CUF amekuwa akiambulia
kura za chini sana.
Kinachoweza kuonekana hapa ni kwamba mchezo
huu wa UKAWA ni njama za baadhi ya vyama kujenga mazingira ya
kuhakikisha vyama vingine havigusi majimbo wanayodhani wananguvu nayo.
Kuweka
wazi ni kwamba, chama kinachojihami zaidi ni Chadema, kwa sababu
kinajua kwamba CUF wakiweka wagombea katika majimbo wanayodhani
wanakubalika, kuna uwezekano wakagawana kura ikashinda CCM.
Lakini
Chadema hata wakiweka wagombea Pemba yote, na hata Zanzibar kwa ujumla
bado CUF inaweza kushinda, na pale itakaposhindwa itashinda CCM lakini
Chadema si rahisi.
Lakini hata upande wa Urais, kutokana na
uzoefu uliojitokeza katika miaka iliyopita, jiulize, je, Profesa
Lipumba ambaye hajawahi kukosa kugombea Urais katika Uchaguzi Mkuu
wowote tangu mfumo wa vyama vingi uanze hapa nchini, atakuwa tayari
safari hii, kumwachai mgombea kwa mfano wa Chadema au wa NCCR Mageuzi,
yeye abakie kuwa mpiga debe?
Au, je, ni rahisi Chadema
wanaojitazama kuwa chama cha upinzania chenye nguvu hapa nchini kuliko
vyama vingine, watakuwa tayari kujiweka pembeni, wasiweke mgombea wa
Urais kuunemesha Ukawa, bila shaka ni ngumu sana, na kama ni rahisi
tusubiri wakati utasema.
Sana sana Chadema, katika kujaribu
kuwatega CUF, wanaweza kuwaambia kwamba hawataweka mgombea Urais wa
Zanzibar, ili chama hicho cha CUF kiwaachie wao Urais wa Muungano,
lakini si rahisi CUF kukubali kwa sababu itakuwa sawa na kujichimbia
kaburi chama hicho kitoweke Tanzania Bara.
Na ni wazi CUF
hawawezi kukubali kwamba waache kugombea Urais wa Muungano kwa kuachiwa
Zanzibar, kwa sabau kulingana na mazingira ya Zanzibar, Chadema hata
wakiweka mgombea Urais wa Zanzibar hawaiathiri chochote CUF. kwa maana
nyingine, Chadema iweke mgombea Urais au isiweka matokeo ya CUF katika
urais hayabadliki sana.
Hata hadi sasa tayari CUF wameshateua watakaowania Ubunge na Baraza la Wawakilishi kwa majimbo yote Zanzibar, na katika kuthibitisha kuwa Ukawa ni kwa ajili ya kuwalinda viongozi, jimbo moja tu la Kikwajuni ambalo CUF wameamua kufumba mamcho na kuwaachia Chadema, wamesema wanaliacha kwa ajili' ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Salum Mwalim na si kwa ajili ya mwanachama yeyote atakayetaka!
Your Ad Spot
May 10, 2015
Home
Unlabelled
HOJA MTAMBUKA: UKAWA KUTI KAVU WALILOKALIA CHADEMA, CUF
HOJA MTAMBUKA: UKAWA KUTI KAVU WALILOKALIA CHADEMA, CUF
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇