SALAAM ZA RAMBIRAMBI
ZILIZOTOLEWA NA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA MAPINDUZI NDUGU ABUDLRAHAMAN KINANA
WAKATI WA KUAGA MWILI WA BRIG. GEN. HASHIM MBITA (Mst)
TAREHE 29 APRILI,
2015 – LUGALO DAR ES SALAAM
Ndugu Rais, Amiri Jeshi Mkuu na Ndugu
Waombolezaji,
Maisha
ni safari na kila safari huwa na mwisho wake,
Tuko hapa kwa kuwa safari ya Brig. Gen. Hashim Mbita duniani imefika
ukingoni. Tumekusanyika hapa siyo
kuhuzunika bali kujivunia safari ya mafanikio makubwa ya Mwanamapinduzi,
Mpiganaji, Mwanadiplomasia, Mwanahabari, Mwanasiasa na Mzalendo wa mfano.
Mwanasayansi
mashuhuri Albert Enstain aliwahi kusema kuwa, thamani ya mtu itapimwa kwa
mchango wake kwa jamii siyo kwa kile alichokipata kutoka kwa jamii
yenyewe. Hakuna ubishi, Brig. Gen Mbita
alitoa mchango mkubwa kwa Watanzania na Waafrika. Aliipenda na kulitumikia Taifa lake. Alishiriki kikamilifu kulijenga na
kuliimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania katika miaka ya awali na
aliongoza Chama cha TANU kwa ufanisi.
Lakini mchango na umahiri wake ulidhihirika katika kuiongoza Kamati ya
Ukombozi ya Bara la Afrika.
Kwa
kumbukumbu zilizopo kila kazi na jukumu alilopewa Brig. Gen. Mbita iwe Jeshini,
Serikalini, katika Chama, katika kuongoza Ukombozi na baadaye kuandika historia
ya Ukombozi, aliteuliwa kwa makusudi maalum na kwa malengo maalum. Alipelekwa Uingereza kutoka Ikulu kwa lengo
la kusaidia kulijenga Jeshi la Wananchi Tanzania liwe la kizalendo baada ya
maasi ya mwaka 1964. Kwa kuamini kuwa Chama imara ndicho kinachotoa uongozi
bora kwa Taifa, Brig. Gen. Mbita aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU
ili kuleta ufanisi na nidhamu katika Chama.
Kuna
msemo maarufu jeshini usemao Kamanda aliye jasiri anaweza kuwa na bahati.
Lakini hakuna Kamanda anayeweza kuwa na bahati bila ya kuwa jasiri. Ujasiri
aliokuwa nao Brig. Gen. Mbita ndiyo iliyokuwa sababu ya kuteuliwa kwake
kuiiongoza Kamati ya Ukombozi wa Afrika.
Alishiriki kuvijenga vikosi vya Frelimo (Msumbiji), ZANU-PF (Zimbabwe),
SWAPO (Namibia), ANC (Afrika Kusini), MPLA (Angola), MOLINACO (Comoro), PAIGC
(Guinea Bissau, Cape Verde) na vyama
vingine. Aliviandaa vikosi hivi
kupambana na majeshi makubwa yenye silaha nzito na za kisasa na yenye nguvu
nyingi. Lakini mwaka 1994, Brig. Gen
Mbita alihitimisha kazi ya Ukombozi wa Afrika kwa ushindi mkubwa.
Chama
Cha Mapinduzi kinatambua na kuthamini mchango na kazi kubwa iliyofanywa na
Brig. Gen. Mbita katika kukiendeleza na kukiimarisha Chama cha TANU na baadaye
Chama Cha Mapinduzi. Katika maisha yake kazini na hata baada ya kustaafu
aliendelea kutoa ushauri, maoni na wakati mwingine kutoa uzoefu wake ndani ya
Chama. Tutauenzi mchango wake, tutajifunza utendaji wake, tutajitahidi kuiga
mwenendo wake na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na ardhi na
mwenye kutupa na kutuondolea uhai, ili amuonee huruma mja wake huyu. Brig. Gen. Mbita atabaki kuwa na nafasi
muhimu katika historia ya mapambano dhidi ya ukoloni, ubeberu, ubaguzi wa rangi
na uonevu.
Alikuwa
kiongozi mwenye msimamo na mwenye kuelewa mambo mengi lakini msikivu.
Inawezekana Watanzania wengi hatukumjua kwa kuwa hakushughulika kujulikana.
Alikuwa jasiri na vile vile alikuwa na wingi wa unyenyekevu. Ujasiri wake
ulidhihirika katika kufanikisha majukumu aliyokabidhiwa lakini unyenyekevu
ulimzuia kujinadi. Alitanguliza utumishi
na kujiepusha na utukufu. Nafasi alizoshika zilikuwa za juu na zenye
kuheshimika. Kama angependa angeweza
kupata umaarufu mkubwa katika nafasi aliyokuwa nayo lakini hiyo haikuwa hulka
yake. Maisha na Utumishi wake ni darasa
kamili kwetu sote.
Tunawashukuru
viongozi waliokuja kuwakilisha vyama mbalimbali kuungana na Watanzania kumuenzi
Brig. Gen. Hashim Mbita. Wanafalsafa
wanatuambia ushindi wa kumbukumbu za wale tutakaowakumbuka zitadumu katika
mioyo ya watu na katika historia ya Taifa walilolitumikia. Sihitaji kuwashawishi
Ndugu waombolezaji wenzangu kukiri kuwa Brig. Gen Mbita atabaki kwenye mioyo
yetu na kuendelea kukumbukwa na wananchi wengi wa Bara la Afrika alioshirikiana
nao kuwarudishia Uhuru wao na heshima yao.
Kwa
kumalizia, kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi natoa pole kwa Mama Mjane, Watoto,
Ndugu na Jamaa, Marafiki na kwa Jeshi la Wananchi Tanzania.
Mwenyezi
Mungu amfungulie milango ya Pepo.
Imetolewa
na:
Idara ya Itikadi na
Uenezi
Chama Cha Mapinduzi
30/04/2015
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇