Tume ya Taifa
ya Uchaguzi imeanza rasmi zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura baada ya kukamilika kwa maandalizi muhimu ya Uboreshaji wa Daftari,
ikiwemo manunuzi ya vifaa na upatikanaji wa fedha kutoka Serikalini.
Zoezi la
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, tofauti na Uboreshaji wa
Daftari hilo kwa Awamu zote za Chaguzi zilizopita, linafanyika kwa kutumia
teknolojia mpya ya Biometric Voter Registration (BVR). Zoezi la Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lilianza kufanyika katika Kata tisa (9) za
Halmashauri ya Mji wa Makambako katika Vituo 54 vilivyowekwa katika Mitaa na
Vitongoji, kuanzia tarehe 23/2/2015 katika Kata za Kitisi, Kivavi, Lyamkena,
Maguvani, Majengo, Makambako, Mji Mwema, Mlowa na Mwembetogwa.
Tume
ililenga kuandikisha Wapiga Kura 32,370 kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya
Takwimu za Sensa ya Idadi ya watu ya mwaka 2012. Tume ililenga kuandikisha kwa siku jumla ya
watu 1,850. Hata hivyo mara baada ya uandikishaji kuanza idadi ya Wapiga Kura
waliokuwa wanajitokeza iliendelea kuwa kubwa na kuongezeka kila siku ambapo
kulikuwa na misururu mirefu ya watu waliojitokeza kujiandisha katika Vituo
vyote vya Uandikishaji. Tume ilivuka malengo yaliyowekwa ya Uandikishaji
kutokana na kujitokeza kwa wingi kwa Wapiga Kura waliofika katika Vituo vya
Uandikishaji kila siku kwa Kata zote tisa (9) za Mji wa Makambako ambazo
zilikuwa zinaandikisha Wapiga Kura.
Idadi ya
Wapiga Kura waliojitokeza na kuandikishwa kwa kila siku katika Kata tisa (9) za
Mji wa Makambako ilikuwa kama ifuatavyo:-
i.Tarehe 23/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura
3,014;
ii.Tarehe 24/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura
4,727;
iii.Tarehe 25/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura
5,301;
iv. Tarehe 26/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura
6,354;
v. Tarehe 27/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura
6,731;
vi.Tarehe 28/2/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura
6,545;
vii.Tarehe 1/3/2015 Tume iliandikisha Wapiga Kura 6,906;
viii.Tarehe 2/3/2015 kutokana na Watu waliokuwa
wanajitokeza kujiandikisha kuendelea kupungua, Tume iliandikisha Wapiga Kura
4,662; na
ix. Tarehe 3/3/2015 ambayo ndio ilikuwa siku ya mwisho
ya uandikishaji, Tume iliandikisha Wapiga Kura 2,469.
Hivyo,
jumla ya Wapiga Kura wote walioandikishwa katika Kata tisa (9) za Mji wa
Makambako ni 46,709. Zoezi la Uboreshaji wa Daftari katika Kata tisa (9) za
Halmashauri ya Mji wa Makambako limefanyika kwa ufanisi na mafanikio makubwa
ambapo Tume imevuka lengo lililowekwa la Uandikishaji kwa kuandikisha jumla ya
Wapiga Kura 46,709 na kuvuka lengo
lililowekwa la kuandikisha Wapiga Kura
32,370 waliolengwa kuandikishwa kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Takwimu za
Sensa ya idadi ya Watu ya mwaka 2012.
Mashine
nyingi za BVR zimeonyesha ufanisi mkubwa kwa kuwa zimekuwa zikiandikisha idadi
ya Wapiga Kura kuanzia 80 kwa siku hadi watu 160. Pamoja na mafanikio hayo,
kumekuwa na changamoto chache zilizojitokeza ikiwemo ya watu wengi zaidi
kujitokeza kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kusababisha
kuwepo kwa misururu mirefu ya watu waliojitokeza katika Vituo kujiandikisha
katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Changamoto
hiyo ilishughulikiwa na Tume kwa kuongeza muda wa ziada wa siku mbili za
kuandikisha Wapiga Kura baada ya muda wa siku saba za uandikishaji kumalizika.
Lengo la kuongeza siku mbili zaidi za uandikishaji lilikuwa ni kutoa fursa kwa Wapiga Kura wote ambao
walikuwa bado hawajajiandikisha kujiandikisha. Vilevile, katika kushughulikia
changamoto hizo, Tume iliongeza idadi ya BVR Kits katika baadhi ya Vituo
vilivyokuwa na idadi kubwa na misururu mirefu ya Wapiga Kura waliojitokeza
kujiandikisha. Wapiga Kura wote waliojitokeza kujiandikisha waliandikishwa pasipo
kuachwa. Kwa ujumla changamoto zote zilizojitokeza zilishughulikiwa na kupatiwa
ufumbuzi.
Tume
inaendelea na Ratiba ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika
Kata nyingine za Halmashauri ya Mji wa Makambako ambapo Ratiba ya zoezi la
Uboreshaji litafanyika kama ifuatavyo:-
i. Katika Kata ya Kitandililo Uboreshaji umeanza
kufanyika kuanzia tarehe 3/3/2015 na utamalizika tarehe 9/3/2015.
ii. Kata ya Mahongole, Uboreshaji utaanza kufanyika
tarehe 11/3/2015 na kumalizika tarehe 17/3/2015.
iii.
Kata ya Utengule, Uboreshaji utaanza kufanyika
tarehe 11/3/2015 na kumalizika tarehe 17/3/2015.
Tume
itaendelea na zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani
Njombe katika Wilaya za Njombe, Makete, Ludewa na Wanging’ombe kuanzia tarehe
16/3/2015 hadi 12/04/2015.
Tangu
zoezi hili lianze katika Halmashauri ya Mji wa Makambako na kumalizika,
Wananchi wameonyesha mwamko mkubwa sana wa kujiandikisha. Ni matumaini ya Tume
kuwa Viongozi wote, Vyama vya Siasa, Asasi za Kiraia na Vyombo vya Habari
vitahamasisha Wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha katika Wilaya za
Njombe, Makete, Ludewa na Wangingo’mbe kujitokeza kwa wingi kujiandikisha
katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Baada ya
kukamilisha Ratiba ya Uboreshaji katika Mkoa wa Njombe, Tume itatoa Ratiba ya
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Mikoa mingine.
Tangazo
hili limetolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇