LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 25, 2015

MWAKA 2030 UWE MWISHO WA TOFAUTI YA USAWA WA KIJINSIA: UN

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anna Maembe, akifuatilia  hitimisho la Mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu Hadhi ya  Wanawake. Kushoto ni Ndugu, Jaji Angela Kileo
------------------------
Na  Mwandishi Maalum, New York
Mkutano wa 59 wa Kamisheni kuhusu  Hadhi ya  Wanawake umemalizika kwa kutoka na maazimio mbalimbali   likiwamo  linalobainisha kuwa  tofauti zote za usawa wa kijinsia zinamalizwa ifikapo mwaka 2030.

Mkutano huo wa wiki mbili na ambao umehudhuriwa  na  mamia ya  wawakilishi  kutoka mataifa ambayo ni wanachama wa  Umoja wa Mataifa, Taasisi za UM na Asasi zisizo za Kiserikali pia  ulipitisha kwa kauli moja  tamko la kisiasa ambalo  limeainsha na kuazimia mambo kadha kwa kadha yanayohusu  fursa  sawa za kijinsia na uwezeshaji wa mwanamke.

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huu,  uliongozwa na Mhe. Sophia Simba ( Mb), Waziri wa Maendeleo ya Jamii,  Jinsia na Watoto.

Kupitia mkutano huo wajumbe hao walijadiliana na kubadilishana mawazo  kuhusu  mafanikio  katika utelekezaji wa maazimio mbalimbali yaliyokubalika wakati  wa Mkutano wa kihistoria wa wanawake uliofanyika  Beijing mwaka 1995 pamoja na changamoto zake.

Akihitimisha mkutano huo Katibu Mkuu  Msaidizi Mwandamizi na Mkurugenzi Mtendaji wa UN- Women,  Bibi.  Phumbzile Malambo-Ngacuka  amesema mwaka 2030  lazima uwe hitimisho la utofauti wa kijinsia jukumu linalotakiwa  kufanyiwa kazi kuanzia ngazi ya familia,  kijamii,  kisiasa na kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa Kamisheni Bi Kandra Vajarabhaya  akizungumzia mwenendo mzima wa  mkutano huo anamesema, kwa wajumbe  kupitisha kwa kauli  moja tamko la kisiasa, kamisheni hiyo   imerejea wajibu  wake  wa  kuchagiza na kufanikisha  upatikanaji wa fursa sawa za kijinsia, uwezeshaji wa wanawake pamoja na  kuhakikisha haki za wanawake na watoto wa kike.

Akatoa pia tathimini ya utekelezaji  wa maazimio  pamoja na  Jukwaa la utekelezaji wa mkutano wa Beijing pamoja na  changamoto zilizobakia.

Kupitia mchakato huu   Bi  Vajarabhaya amesema wajumbe  wamemejifunza kwamba bado kuna  changamoto , na kwamba   mkutano wa kamisheni hiyo umetoka na mapendekezo kadhaa ya   kuimarisha utendaji wa chombo hicho.

Pamoja na majadilianao  ya ajenda mbalimbali   mkutano huo  umepitisha  maazimio manne likiwano linalohusu namna ya kuwasaidia wanawake wa Palestina, azimio hilo lilipitishwa kwa kupigiwa kura ambapo kura 27 ziliunga mkono azimio hilo huku  mbili (  Israel na  Marekani ) zikilipinga.
 Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akiwa na wajumbe wa Tanzania waliohudhuria na kushiriki  Mkutano wa 59 wa Kamisheni  kuhusu  Hadhi ya  Wanawake ( CSW) mara baada ya kufungwa kwa mkutano huo wa wiki mbili jana Ijumaa ya wiki iliyopita.
 Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi akiwa na  wajumbe  kutoka Zanzibar  waliohudhuria mkutano wa  59 wa CSW
 Baadhi ya ya Ujumbe uliotoka Tanzania, wakifuatilia  uhitimishwaji wa  Mkutano wa  59 wa  CSW

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages