LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 10, 2015

AFYA YA MAMA NA MTOTO NI AJENDA ENDELEVU - WADAU

Na  Mwandishi Maalum, New  York
Kundi la  Nchi  Marafiki kuhusu  afya ya mama na mtoto limekutana na kufanya  kikao  chake cha kwanza na kukubaliana kwa kauli moja  kwamba mama  anapokuwa na afya njema anakuwa na uhakika wa  maisha yake na maisha ya mtoto wake.

Kama hiyo  haitoshi  kundi hilo la nchi marafiki  na ambalo  limekutana nchi ya  uenyekiti- wenza wa   Wakilishi wa  Kudumu wa Tanzania na Canada katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi na  Balozi  Gillermo Rishchynski,  limekubaliana haja na umuhimu wa  kuhakikisha  kuwa ajenda  kuhusu afya ya mama na mtoto  inaendelea  na kubaki kuwa  moja ya vipaumbele vya   malengo mapya ya maendeleo baada ya 2015

Kundi la nchi hizo marafiki kuhusu afya ya mama na mtoto , linaundwa na   wawakilishi kutoka nchi  40 zilizoendelea na zinazoendelea.    Kikao hicho kwanza,  kimehudhuriwa pia maafisa wa ngazi za juu kutoka  Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwamo    Bi. Amina Mohammed ambaye ni   Katibu Mkuu Msaidizi Mwandamizi na Mshauri wa Katibu Mkuu, kuhusu  Mipango ya Maendeleo baada ya 2015.

Akizungumza mwanzoni mwa  kikao hicho Balozi Tuvako Manongi amesemea,  Tanzania  imekubali  na inajisikia fahari kuwa mwenyekit- wenza wa kundi hilo,  kutokana na ukweli kwamba, Idadi kubwa ya vifo vya akina mama vitokavyo na matatizo ya uzazi  pamoja na vifo vya watoto wachanga vinatokea Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“ Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara ni wadau wakubwa katika kulikabili tatizo hili kwa kushirikiana na wadau wengine, tumepiga hatua za kuridhisha katika    kuhakikisha kwamba mama mjazito hapotezi maisha yake wakati wa kujifungua au mtoto mchanga hapotezi maisha yake mara tu baada ya kuzaliwa ingawa changamoto bado ni nyingi”

Na kuongeza kuwa  juhudi hizi  zinahitaji pamoja na mambo mengine uwajibikaji wapamoja,  uwezeshwaji wa  raslimali fedha  lakini kubwa zaidi utashi wa kisiasa na utimizwaji wa ahadi zinazotolewa na wadau mbalimbali.

Aidha Balozi Manongi amesisitiza pia  umuhimu wa  elimu kwa wanawake   na hasa watoto wa kike kwa kile anachosema, mtoto wa kike akielimishwa kwa maana ya kupata fursa ya kwenda shule na kusoma,  anakuwa na uelewa mpana wa mambo mbalimbali yakiwamo yanayohusu  afya yake mwenyewe lakini pia afya ya mtoto wake.

“ Elimu kwa wanawake na watoto wa kike, ni jambo muhimu sana,  na hasa ikizingatiwa wanawake ndio  uti wa mgongo wa  Bara la Afrika,  mwanamke na mtoto wa kike anapopata fursa ya kupata elimu anao mchango mkubwa kwake mwenyewe, kwa familia yake na  kwa jamii inayomzunguka” amesisitiza Balozi Manongi.

Naye Balozi wa Canada,  Gillermo Rishchynski, pamoja na kusisitiza ushirikiano baina ya  wadau  mbalimbali katika jitihada hizi za  kuimarisha  kuboresha  huduma za afya ya mama na mtoto. Amesema  serikali yake imetenga dola  za kimarekani 3.5bn kwa pindi cha  2015-2020 kwaajili ya  afya ya mama na mtoto.

Kundi la Nchi Marafiki kuhusu afya ya mama na mtoto litakuwa linakutana kila baada ya wiki sita au nane   na litajielekeza  Zaidi  katika  katika kufanya tathimini ya hali ya sasa  ya  utekelezaji wa malengo  namba nne na tano ya maendeleo ya millennia   mabayo utekelezaji wake unafikia ukingoni  mwishoni mwa wamaka huu. 

Kundi hili pia litakuwa na fursa ya  kujadiliana, kubadilishana mawazo  pamoja na kujiwekea mipango ya namna gani ya kuongozea jitihada za kusukuma mbele ajenda hii ya afya ya mama na mtoto kwa dhumuni la kupunguza vifo vitokanavyo na  uzazi, vifo vya watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano.

Mwezi Mei mwaka 2014 Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Canada  Stephen Harper  ambao ni wenyeviti wenza wa Kamisheni ya Habari na Uwajibikaji kuhusu  afya ya mama, mtoto mchanga na mtoto waliongoza huko Toronto Canada,  mkutano maalum wa wakuu wa nchi  ambapo  ilikubalika kwamba suala  hilo   lipewe kipaumbele katika kukalimisha Malengo ya  Millennia yanayofikia ukiongoni mwaka huu.

Ni katika mkutano huo, ambapo  ilikubalika kwamba Wawakilishi wa Kudumu wa Tanzania na Canada katika Umoja wa Mataifa waunde kundi la nchi Marafiki  kuhusu afya ya  mama na mtoto.
 Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete  katika picha hii ya maktaba anaonekana  akimpa hongera mama ambaye amejifungua salama yeye na mtoto wake. Afya   ya mama na mtoto   ni moja ya ajenda ambayo  inapewa umuhimu wa pekee katika duru ya Jumuiya ya Kimataifa. Tanzania na Canada kupitia wakilishi zao za  Kudumu katika Umoja wa Mataifa zimeanzisha kundi la  Nchi  Marafiki kuhusu ajenda hiyo ya Afya ya Mama na Mtoto lengo kuu   kuhakikisha kuwa mama na mtoto ni ajenda ambayo haifi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages