NA BASHIR NKOROMO
HALI inazidi kuwa mbaya ndani ya Kambi ya
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kufuatia taarifa za mgogoro mkubwa
uliopo kati ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia.
Chanzo
cha mgogoro huo ambao unafukuta, ni madai ya Slaa ya kutomwamini Mbatia
anayedai ni pandikizi anayetumiwa na serikali na Chama cha Mapinduzi
(CCM) kuvuruga umoja huo.
Inaelezwa, Slaa anamshutumu Mbatia kuwa
ni Afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa, hivyo ni hatari kwa ustawi wa
umoja huo, na kuna uwezekano akasababisha kusambaratika kwake iwapo
ataendelea kuwepo.
"Ukiwa nje huwezi kuona hali halisi ya mambo,
kwa tulio ndani ndio tunaona kila kitu, huu umoja hauwezi kufika popote
maana watu hawaamiani hata kidogo na kuna migogoro kila kukicha"
"Sasahivi
Slaa anashinikiza Mbatia aondolewe UKAWA, anadai akiachwa atavuruga
mpango wa kwenda ikulu" kilisema chanzo chetu kilichopo ndani ya kambi
ya UKAWA.
Chanzo hicho kilisema, msimamo huo wa Slaa umewapa
wakati mgumu vongozi wengine wa kambi hiyo na wanaona wakimtosa Mbatia
watasababisha mgawanyiko wa wanachama, hivyo kuna uwezekano mkubwa
wakampuuza Katibu Mkuu huyo.
"Slaa hapendi kumuona Mbatia akiwa
UKAWA, ila Mbatia ni muhimu zaidi kuliko Slaa kwenye umoja huu maana
anawakilisha chama na iwapo chama chake kitatoka kutasababisha mpasuko,
kwahiyo kuna uwezekano mkubwa wakampuuza katibu mkuu, ila wakimpuuza
unamjua mambo yake, ataanza vurugu ndani ya chama" kilisema chanzo
chetu.
Aidha, mbunge mmoja wa CUF akizungumza na mwandishi wa
habari hizi alisema, baadhi ya wanachama wa UKAWA wanamshutumu Mbatia
kuwa mmoja wa walioshinikiza kambi hiyo kususia mchakato wa Katiba mpya
na kushawishi wasirudi bungeni.
"Kuna mambo yanatia mashaka sana
na leo viongozi wetu wanajuta, uamuzi wa kususia bunge la Katiba haukuwa
sahihi, vongozi wetu walipotoshwa kususia bunge. Naamini kama
tungebakia bungeni na kushindana kwa hoja, kingeeleweka"
"Mbatia
alikuwa kinara wa kusisitiza tusirudi na kuna taarifa feki zilikuwa
zinakuja ambazo zilionekana wazi mchakato ungekwama, lakini tumeona
kilichotokea, CCM na baadhi ya wabunge wa UKAWA wakaendelea na
wameandika walichotaka, na kwa hali ilivyo katiba wanayotaka wao
itapita" alisema mbunge huyo kutoka Zanzibar (jina tunalihifadhi).
Mbunge
huyo alisema, hali hiyo inaonyesha wazi kuna watu ndani ya kambi hiyo
wanatumika na CCM, na mbinu ya kushawishi UKAWA wasirudi bungeni ilikuwa
ni maagizo maalum yenye lengo la kuwapa nafasi CCM kupitisha mambo
waliyotaka kwenye Katiba mpya.
Taarifa zaidi zinasema, jambo
jingine ambalo linampotezea imani Mbatia kwa baadhi ya viongozi wenzake,
ni uhusiano wake na kigogo mmoja mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa
(TISS), ingawa mwenyewe mara kadhaa amekuwa akikana madai hayo na
kushusha lawama kwa CCM kuhusika kusambaza madai hayo.
Inaelezwa,
Mbatia amekuwa karibu na kigogo huyo na wamekuwa wakikutana mara kwa
mara nyumbani kwake maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kwa lengo
la kupeana maelekezo ambayo hawana shaka yanalenga kufanya hujuma kwa
kambi hiyo.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa waliozungumza na
mwandishi wa habari hizi wamesema, kambi ya UKAWA ipo kwenye wakati
mgumu ukiachilia mbali mgawanyiko uliopo katika suala la kuteua mgombea
Urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, kuna hali ya kutoaminiana na kila mmoja
anamuona mwenzake ni msaliti.
"Kabla hawajaungana Chadema
waliwahi kukishutumu CUF kuwa ni tawi la CCM (CCM B), Wenje (Ezekiel
Wenje) aliwahi kuwashutumu CUF kuwa ni chama cha mashoga, Chadema hao
hao walishamuita Mbatia ni mbunge wa Rais Kikwete kwa kuwa aliteuliwa na
Rais hivyo ni mbunge anayefuata maagizo ya CCM" alisema John Malingumu
mchambuzi wa masuala ya kisiasa.
Mchambuzi huyo aliongeza kuwa,
kila mmoja ndani ya kambi hiyo ameungana na mwenzake kwa malengo
binafsi, ila hakuna mwenye imani na mwenzake.
"Pale kuna unafki
mkubwa, kila mmoja amebaki na historia yake kichwani ya mambo ambayo
walifanyiana kabla hawajaungana, utakumbuka pia Chadema waligoma kuunda
Kambi ya Upinzani na CUF, haya yote hayajafutika"
Your Ad Spot
Jan 25, 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇