Katibu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu akionyesha kadi nne ya mgombea
uenyekiti wa Kitongoji, mgombea uenyekiti wa Kijiji sambamba na Wajumbe
wawili kupitia tiketi ya Chadema waliojitoa kugombea na kuhamia CCM
Mgombea pekee mwanamke nafasi ya
uenyekiti wa Kijiji cha Ifupila, Kata ya Ifwagi Sevelima Ngunda akiomba
kura wakati wa kufunga kampeni
Na Mathias Canal, Mufindi
Wakati ikiwa imebaki siku moja kabla ya kupiga kura kwa
ajili ya kuwachagua viongozi watakaowakilisha mitaa, Vitongoji pamoja na
vijiji wagombea nafasi ya Uenyekiti wa Kijiji,Kitongoji na wajumbe
wawili kupitia tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
ambao ni Mgombea uenyekiti wa Kitongoji cha Mpanga Yustin Kadege,
Mgombea Uenyekiti wa Kijiji cha Mpanga, Yudita Mutung'e sambamba na
wajumbe Anjela Ngenzi na Betson Nkongwa, wametimukia CCM hivyo kuongeza
idadi ya mitaa, Vitongoji na Vijiji ambavyo CCM imepita bila kupingwa.
Akipokea kadi hizo kutoka kwa wagombea hao wakati wa
mkutano wa kufunga kampeni Wilayani Mufindi, Katibu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mufindi, Miraji Mtaturu, aliwataka wananchi
kujitokeza kwa wingi na kutovaa sare za chama siku ya kupiga kura
Jumapili ya Disemba 14 mwaka huu.
Mtaturu alisema kuwa watanzania watapiga kura mwa wagombea
nafasi ya uenyekiti wa Vitongoji 64,000 Tanzania nzima ambapo pia kuna
jumla ya Vijiji 13,000 wakati Mitaa ipo 3000 Tanzania nzima.
Akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Ifupila Kata ya Ifwagi,
lakini pia Kijiji cha Mtwango Kata ya Mtwango Mtaturu, alisema kuwa
hakuna mwananchi atalayerusiwa kufanya kampeni siku ya chaguzi kwani
tayari kampeni hizo zimefungwa Wilayani humo na Tanzania kwa ujumla.
Aidha alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa familia ya
mgombea nafasi ya Kitongoji cha Fukalendi aliyefariki dunia hivi
karibuni na kusema kuwa kutokana na msiba huo hakutakuwa na uchaguzi
badala yake utafanyika uchaguzi mdogo mara baada ya uchaguzi wa kesho
kupita.
"Vyama vya upinzani vimelewa amani na utulivu tulioachiwa
na baba wa Taifa hili Mwl Julius K. Nyerere hivyo vinatumia vibaya amani
hii kwa kuhamasisha maandamano hatimaye kusababisha wanachi kuuwawa kwa
kasi pasipo sababu ya msingi" Alisema Mtaturu
Hata hivyo akiwa Kijiji cha Ifupila Kata ya Ifwagi, Mtaturu
alimpongeza Sevelina Ngunda ambaye ni mwanamke pekee anayegombea nafasi
ya uenyekiti katika Kata hiyo na Wilaya nzima ya Mufindi.
Mtaturu alisema kuwa mtaji wa CCM sio maneno pekee au
kujaza watu kwenye mikutano bali mtaji pekee ni kuwa na watu wenye imani
ya kukupigia kura kama ilivyo kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo kina
wanachama wengi jambo ambalo linasababisha CCM kutamba kushinda kwa
kishindo uchaguzi huo.
"Naamini kila mtu anajua kuwa CCM haiombi kura pekee bali
inatoa pia elimu juu ya umuhimu wa kupiga kura, hivyo mnapaswa kutambua
kuwa kila baada ya miaka 5 uchaguzi wa serikali za Mitaa hufanyika kwa
kuwa ndio msingi wa maisha ya wananchi katika maendeleo yao" Alisema
Mtaturu
Aidha kesho ni siku iliyokuwa inasubiriwa na watanzania
wengi kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa ajili ya kuwapata
wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji ikiwa ni pamoja na wajumbe ambalo hata
hivyo Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho chenye nafasi kubwa ya kuibuka na
Mitaa, Vitongoji, na Vijiji kutokana na mtaji iliyonayo ya kupita bila
kupingwa kwa asilimia 85% mpaka hivi sasa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇