Mbunge
wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, akizungumza na mmoja wa
wakulima wa kahawa wilayani Kigoma Vijijini katika mojawapo ya ziara
zake za kuhamasisha kilimo na kuhimiza wakulima kujiunga na Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii.
.............................................................................................................................................................................
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto
Kabwe, ameibuka mwanasiasa wa kwanza barani Afrika kutwaa Tuzo ya Mtetezi wa
Haki ya Hifadhi ya Jamii, imefahamika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa mwishoni mwa
wiki na Umoja wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya Nchi za Afrika Mashariki na Kati
(ECASSA), Zitto anatarajiwa kukabidhiwa tuzo yake hiyo katika sherehe rasmi
iliyopangwa kufanyika Oktoba 30 na 31 mwaka huu katika mji wa Livingstone nchini
Zambia.
“Tuzo hii imetolewa kwako kwa kuzingatia mchango
wako mkubwa unaoutoa kuhakikisha sehemu kubwa ya Watanzania ambao walikuwa
hawanufaiki na mifuko hii wanafaidika nayo.
“ECASSA, mahususi kabisa, imevutiwa sana na
jitihada zako za kuhakikisha kwamba wasanii wananufaika na mifuko ya hifadhi ya
jamii pamoja na wakulima kupitia chama chao cha ushirika cha Rumako kilichopo
Kigoma Vijijini,” ilisema sehemu ya barua ya umoja huo kwa Zitto ambayo gazeti
hili imefanikiwa kupata nakala yake.
RUMAKO ni Ushirika wa Msingi wa Vijiji vya
Mkabogo, Rusaba na Matyazo wilayani Kigoma Vijijini ambako zaidi ya wakulima
wake 750 wameingia kuwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)
katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Kwa takribani miaka minne sasa, Zitto amekuwa
akipigania wakulima wa Tanzania kupewa uanachama wa wa mifuko hiyo ili
kuwakwamua kiuchumi na pia kuwawezesha kupata huduma ya hifadhi kama ilivyo kwa
wafanyakazi katika sekta rasmi wanaopata huduma hizo.
Baada ya wakulima hao wa Kigoma, kumekuwepo na
wimbi la vyama vingi vya wakulima katika maeneo mbalimbali nchini kutaka
kuingia katika mifuko hiyo na ECASSA inaamini kwamba Zitto ana mchango mkubwa
katika hilo.
Akizungumzia tuzo hiyo, Zitto alisema, "
nimeipokea tuzo hii kwa unyenyekevu mkubwa. Naamini kuwa siku za usoni haki ya
Hifadhi ya jamii kwa wananchi itakuwa ni haki ya kikatiba. Nchi masikini
zinapaswa kuongeza uwekaji akiba ili ziweze kuendelea kwa kasi. Bila akiba
uwekezaji unakuwa mdogo na hatimaye uchumi haukui. Hifadhi ya jamii ni moja ya
njia mwafaka kabisa ya kukuza uwekaji akiba katika nchi kwani wanachama
wanafaidika na mafao ya muda mrefu kama pensheni na yale ya muda mfupi kama
Bima ya Afya na mikopo kupitia saccos".
Azimio la kutolewa kwa tuzo hiyo lilitokana na Mkutano
Mkuu wa Sita wa ECASSA uliofanyika jijini Kampala, Uganda miaka miwili
iliyopita, ambapo wakuu wa mifuko hiyo walikubaliana iwepo ili kuchochea
wanasiasa kuhamasisha wananchi kuelewa umuhimu wa Hifadhi ya Jamii.
ECASSA ni umoja unaounganisha Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii takribani 20 katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi
na Zambia
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇