Na Winner Abraham na
Rose Masaka-
MAELEZO-Dar es salaam
Mwenyekiti wa Bunge
Maalum la Katiba Samuel Sitta, amesema kuwa Mkutano wa Bunge hilo, utaendelea kama
ulivyopangwa Agosti 5, mwaka huu mjini
Dodoma.
Amesema kuwa licha ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, kuendelea
na msimamo wao wa kutaka kususia vikao
vitakavyoanza mapema mwezi ujao, lakini bado kuna mambo muhimu ya kujadiliwa.
Mwenyekiti huyo ametoa kauli hiyo leo mjini Dar es salaam,
katika taarifa yake iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu wa Bunge Maalum la
Katiba, Yahaya Khamis wakati wa mkutano wa waandishi wa habari.
“Kamati hiyo,
imeamua kupendekeza kwa Kamati ya Uongozi
kwamba Bunge Maalum la Katiba liendelee kwa
sababu yapo masuala mengi muhimu
ya kikatiba ambayo yanatuunganisha kama vile usawa wa kijinsia katika nafasi za
uongozi na kuikarabati Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC).
“Mambo mengine ni kurekebisha
kikatiba masuala ya Muungano,haki za wakulima,wafugaji,wasanii na makundi
mengineyo na ukomo wa vipindi vya uongozi,”alisema Sitta katika taarifa hiyo.
Aidha aliongeza kwamba uamuazi huo, umefikiwa baada
ya wajumbe wa Kamati hiyo waliohuduria ambao walikuwa zaidi ya theluthi mbili
ya wajumbe wote, ambapo waliendelea na kikao.
Alisema hatua ya
baadhi ya wajumbe kwenda kwa wananchi na maoni yao imekuwa siyo muafaka na si
wakati wake, hivyo Bunge hilo liwajibike katika siku za usoni kujibu
upotoshwaji wowote kuhusu mchakato wa katiba kadri unavyojitokeza.
Aliongeza kwamba Kamati
hiyo, inaona kwamba kwa kuendelea
kulisusia Bunge hilo, na kupuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali
pamoja na madhehebu ya dini inatilia shaka dhamira halisi ya viongozi wa kundi hili la wasusiaji
kupuuzia juhudi zote za usuluhishi, kunazua mashaka kuhusu lengo la ususiaji kwamba pengine agenda ya viongozi hawa ni
nyingine na siyo upatikanaji wa Katiba.
Alisema Kamati hiyo
inarejea kwamba wajumbe hao 629 wamekabidhiwa jukumu adhimu na la
kihistoria kwa niaba ya Watanzania jukumu ambalo hutokea baada ya miongo kadhaa
ya uhai wa Taifa lolote.
“ Tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ikiwa hatutafikia
maridhiano yanayotuwezesha kukamilisha kazi tuliyopewa,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo
alisema katika ngwe ya pili inayoanza mapema mwezi ujao mkutano wa Bunge
hilo, uzingatie upya baadhi ya Kanuni za
Bunge hilo, ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kwamba kazi ya kujadili na
hatimaye inayopendekezwa inakamilika
ndani ya siku 63 zilizosalia kisheria, kati ya hizo siku 60 ni za nyongeza na
tatu zilizokuwa pungufu za siku 70 za
awali.
Alisema Kamati hiyo,
inaendelea kutoa wito wa wajumbe waliosusia mikutano ya Bunge hilo, kurejea
katika Bunge hilo, ambalo pekee ndiyo lina uwezo wa kisheria wa kutatua matatizo
yaliyopo.
Amesema kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 54 kifungu cha nne na
tano ya Kanuni za Bunge Maalum la Katiba, aliteua Kamati ya Mashauriano ya
wajumbe thelathini (30) kujadili matatizo yaliyojitokeza Dodoma katika mkutano
ulipita lakini wajumbe kutoka Chama cha CUF, CHADEMA na NCCR Mageuzi,walikisusa
kikao cha jana Julai 24 mwaka huu.
“Jitihada mbalimbali zilizofanywa na sekretarieti pamoja na
mwenyekiti hadi asubuhi ya siku ya mkutano hazikuweza
kuwashawishi wajumbe hao wasusiaji kuhudhuria kikao, alisema Sitta
katika taarifa yake.
Aliitaja athari za kutoendelea na mchakato uliopangwa wa
kuandaa na hatimaye kuipigia kura Katiba
mpya ni pamoja na kupoteza mabilioni ya fedha za wananchi zilizokwisha tumika katika kazi,
baya zaidi ni kuiweka rehani amani ya nchi yetu kwa kuukuza mno mgogoro wa katiba na kuwagawa wananchi kwa
propaganda hadi uchaguzi mkuu 2015.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇