-Walikuwa wanakwenda mnadani
-Wawili hali zao mahututi
Na Chibura Makorongo, Shinyanga
Watu wawili
wamekufa papo hapo na wengine 46 kujeruhiwa baada ya lori aina
ya Fuso walilokuwa wakisafiria na mizigo yao kutoka katika kijiji cha Kiloleli
kwenda katika mnada wa Mhunze wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kuacha njia na kupinduka
kutokana na kile kilichotajwa kuwa mwendo kasi.
Ajali hiyo imetokea leo saa
tatu asubuhi katika kijiji na kata ya Uchunga wilaya ya Kishapu mkoani
Shinyanga baada ya lori lenye namba za usajili T680 ARL aina ya Fuso lililokuwa
limepakiza mizigo na wafanyabiashara ambao idadi yao bado haijajulikana likitokea kijiji cha Kiloleli wilayani Kishapu
kwenda katika mnada wa Mhunze uliopo Kishapu liliacha njia na kupinduka.
Walioshuhudia ajali hiyo
wamesema gari hilo lilikuwa katika mwendo kasi likamshinda dereva, hivyo
kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi.
Kamanda wa
polisi mkoa wa Shinyanga, SACP Justus Kamugisha amesema katika taarifa za awali zinaonyesha kuwa ajali hiyo imetokana na mwendo kasi wa lori hilo.
Amesema lori hilo aina ya
Fuso, mali ya Ngasa Seni, mkazi wa Kiloleli lilikuwa likiendeshwa na Shija Ngasa ambaye pia ni mfanyabiashara, mkazi wa Kiloleli wilayani Kishapu ambaye alitoroka baada ya kutokea ajali
hiyo na anatafutwa na jeshi la polisi.
“Lori hili lilikuwa linatoka
Kiloleli kwenda Mhunze mnadani,lilikuwa limepakiza abiria wengi wakiwa
wafanyabiashara,liliacha njia na kupinduka,chanzo mwendo kasi”,alifafanua kamanda
Kamugisha.
“Taarifa za awali tulizonazo
watu wawili wamefariki dunia,mmoja anaitwa Difa Shimo(28) mkazi wa Bulima
Kishapu,mwingine jina lake bado halijafahamika,majeruhi wako 46, 35 wako katika
hospitali ya mkoa wa Shinyanga, 11 wapo katika Hospitali ya Kolandoto iliyopo
katika manispaa ya Shinyanga”,aliongeza Kamugisha.
Kufuatia ajali hiyo kamanda
Kamugisha alitoa wito kwa wamiliki wa magari,wananchi wakiwemo wafanyabiashara
kuacha tabia ya kutumia magari yasiyo ya abiria kusafiria.
Kaimu mganga
mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga Dk. Maguja Daniel amesema wamepokea
miili miwili ya marehemu na majeruhi 35 na wanaendelea kuwapatia matibabu huku wawili hali zao zikiwa mbaya.
Ajali hiyo ya Fuso imetokea
ikiwa ni siku moja tu baada ya abiria 63 kunusurika kufa baada ya basi la Super
najimunisa likitokea Mwanza kwenda Dar es salaam kupinduka katika eneo la
kijiji cha Usanda kata ya Samuye wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇