Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akizungumza katika mkutano wa maadhimisho ya miaka 50 ya nchi za
G77 na China, uliofanyika jijini Santa Cruz, Bolivia jana Juni 15, 2014.
Picha na OMR
Sehemu ya washiriki na wawakilishi wa viongozi wa mataifa mbalimbali katika mkutano huo.Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (wa pili kushoto mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wenzake waliohudhuria na kuzungumza katika mkutano huo wa sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya nchi za G77 na China uliofanyika jana Juni 15, 2014, jijini Santa Cruz, Bolivia. Picha na OMR
Sehemu ya washiriki na wawakilishi wa viongozi wa mataifa mbalimbali katika mkutano huo.Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (wa pili kushoto mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wenzake waliohudhuria na kuzungumza katika mkutano huo wa sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya nchi za G77 na China uliofanyika jana Juni 15, 2014, jijini Santa Cruz, Bolivia. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed
Gharib Bilal amezitaka nchi wanachama wa G77+China, kuhakikisha
zinaboresha kilimo ili ziwe na hifadhi ya kutosha ya chakula kwa
wananchi wake.
Akihutubia mkutano wa mwaka kwa nchi za G77+China ambao
pia ni kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya umoja wa nchi hizi,
unaofanyika jijini St Cruz De Sierra, Dkt Bilal alisema nchi za umoja
huu zina maeneo mazuri kwa kilimo na hivyo ni muhimu kuyatumia maeneo
haya katika kuzalisha chakula kwa lengo la kuhifadhi na kuwa na usalama
wa chakula nyakati zote.
Dkt. Bilal alisema, nchi hizi kwa pamoja zinahitaji
kuwa na kauli moja kuhusu masharti yanayowekwa na nchi kubwa hasa katika
kilimo na kuelezea kuwa ili mafaniio makubwa yapatikane, lazima uwepo
uwekezaji wa ndani katika kilimo sambamba na serikali za nchi hizi
kuchangia shughuli za uzalishaji ili kuwa na kilimo chenye tija kwa
wakulima na kinachoweza kuchangia usalama wa chakula.
Kuhusu suala la mazingira, Mheshimiwa Makamu wa Rais
aliwaeleza wajumbe wa G77+China kuwa, maazimio yaliyofikiwa Rio+20 na
mapendekezo kuhusu ‘Kesho tunayoitaka’ yanazihitaji nchi hizi kupaza
sauti zake kwa pamoja kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi
kwani suala hili kwa sasa haliwezi kutatuliwa na nchi moja bali
linahitaji nguvu ya kila mtu duniani.
Makamu wa Rais alifafanua kuwa bila kuwa na
mazingira bora maendeleo endelevu yatabakia ndoto na pia kufanikisha
Malengo ya Milenia kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa itakuwa vigumu
kama suala la mazingira litaachwa kwa kila nchi kufanya inavyotaka.
“Kundi hili lina kazi kubwa iliyo mbele yetu na hasa
kuhusu malengo mapya ya maendeleo baada ya kukamilika kwa muda wa
Malengo ya Milenia mwakani. Tunahitajika kubuni njia za kuzipatia nchi
zetu maendeleo katika Nyanja za uchumi, kijamii na mazingira ili
tufanikiwe vema,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais.
Katika hotuba hiyo Mheshimiwa Makamu wa Rais pia
alizungumzia kuhusu umuhimu wa nchi hizi kuweka msisitizo wa kuwapa
wananchi maji safi na salama, umuhimu wa kuwa na nishati inayotosheleza
matumizi ya uzalishaji, uwepo wa huduma bora za afya na elimu ili kupiga
hatua kwa haraka baina ya wananchi wa nchi hizi. “Nafahamu kufanikisha
haya yote ni kazi kubwa lakini hatuna muda wa kusubiri. Ni lazima
tufanye kazi ili kubadili hali iliyopo,”alifafanua.
Mkutano huo ambao umekamilika jana kwa mwenyeji wake
Rais Evo Morales kuwashukuru wanachama wa G77+China walioweza kushiriki
mkutano huo, pia ulionesha nia kwa wanachama wa nchi hizi kutafuta
majibu ya changamoto ya ukosefu wa ajira unaokabili wananchi wengi wa
nchi hizi. Viongozi wengi walisisitiza kuwa, suala la ajira hasa kwa
vijana linatakiwa kutazamwa upya na hasa ukizingatia rasilimali zilizopo
katika nchi za G77+China ili zitumike katia kutengeneza ajira mpya
zitakazoweeza kusaidia kuboresha maisha ya watu wa nchi hizi kwa miaka
mingi ijayo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇