Matokeo
ya Mtihani wa Majaribio (Mock) kwa mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu
na Kidato cha Sita mwakani, yatachangia alama 10 za Alama Edelevu (CA).
Kwa
utaratibu huu, matokeo ya mwisho ya mtahiniwa, yatatokana na asilimia
30 ya Alama Endelevu na asilimia 70 ni mchango wa Alama za Mtihani wa
Taifa.
Asilimia 30 za Alama Endelevu, zitapatikana kutokana na mitihani mbalimbali.
Kwa Kidato cha Nne mwaka huu, alama hizo zitatokana na matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha pili ambao utakuwa na alama 10, matokeo ya kidato cha tatu muhula wa kwanza na wa pili alama tano, matokeo ya mtihani wa majaribio (mock) wa Kidato cha Nne ni alama 10 na majaribio ya kazi alama tano.
Utaratibu
huu umetokana na viwango vipya vya ufaulu, vilivyoainishwa na Baraza la
Mitihani Tanzania (NECTA) kwenye kitabu cha Mwongozo wa Matumizi ya
Viwango vya Ufaulu na utaratibu wa kutunuku matokeo ya kidato cha nne na
sita.
Kwa
Kidato cha Sita, zitatokana na matokeo ya mtihani wa Kidato cha Tano
muhula wa kwanza na pili alama 15, matokeo ya 'mock' alama 10 na kazi
mradi itakuwa ni alama tano.
“Katika
somo ambalo mtahiniwa hakufanyia Kazi za majaribio, alama za matokeo ya
Mitihani ya 'Mock' ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita, itachangia
alama 15 badala ya 10 zilizoainishwa,” imefafanua sehemu ya mwongozo
huo.
Katika
Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka jana na Kidato cha Sita mwaka huu,
mchanganuo wa alama 30 za Alama Endelevu ni alama 15 zinazotokana na
matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili, asilimia 10 ilitokana na
maendeleo ya mitihani ya kidato cha Tatu muhula wa Kwanza na Pili na
matokeo ya muhula wa Kwanza Kidato cha Nne na kazi za majaribio asilimia
tano.
Kwa
Kidato cha Sita, alama endelevu ni matokeo ya Kidato cha Tano kwa
mihula yote miwili ni alama 15, muhula wa kwanza wa Kidato cha Sita ni
asilimia 10 na kazi za majaribio ni asilimia tano.
Aidha,
Baraza limebadili utaratibu wa kupanga madaraja ya kufaulu, kutoka
mfumo wa Pointi na kuwa wa Wastani wa Alama za Mtahiniwa (GPA).
Mfumo
unaotumiwa sasa wa pointi, huonesha wastani wa pointi alizopata
mtahiniwa kwa masomo aliyofaulu zaidi, na kupanga madaraja kuanzia la
kwanza hadi la nne.
Madaraja
ya mfumo wa GPA, hupangwa katika utaratibu wa Distinction, Merit, Pass
na Fail. Daraja la Distinction ni la ufaulu wa juu zaidi na daraja Pass
ni ufaulu wa chini.
Mtahiniwa
hutunukiwa madaraja A, B+, B, C, D, E au F kutegemeana na ufaulu wake
katika somo ambapo uzito wa alama katika madaraja A = 5, B+= 4, B = 3,
C=2, D = 1, E = 0.5 na F = 0.
Mtahiniwa
atahesabiwa kuwa amefaulu somo, endapo atapata Daraja D ambayo ni sawa
na uzito wa alama moja. Ukokotoaji wa jumla ya GPA ya mtahiniwa
hufanyika kwa kuzingatia masomo, ambayo mtahiniwa amefaulu angalau kwa
daraja D na kuendelea (D, C, B, B+ na A).
GPA
anayopata mtahiniwa hutokana na wastani wa pointi alizopata katika
masomo saba aliyofanya vizuri zaidi kwa Mtihani wa Kidato cha Nne au
masomo matatu ya mchepuo kwa Mtihani wa Kidato cha Sita.
Aidha,
GPA ya mtahiniwa huandikwa katika nafasi moja ya desimali ambapo nafasi
ya pili ya desimali hukadiriwa katika makumi yaliyokaribu.
Mfano, mtahiniwa mwenye GPA ya 3.15 itakuwa sawa na 3.2 na mtahiniwa mwenye GPA ya 3.14 itakuwa sawa na 3.1.
Muundo
wa madaraja ya GPA kwa kidato cha nne, Distinction ni 3.6-5.0, Merit
2.6 -3.5, Credit 1.6-2.5, Pass 0.3-1.5, Fail 0.0-0.2 wakati Kidato cha
sita ni Distinction 3.7-5.0, Merit 3.0-3.6, Credit 1.7-2.9, Pass
0.7-1.6, Fail 0.0-0.6
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇