Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu Kiongozi wa Japan,
Yoshihiro Suga, wakati alipofika ofisini kwake Jijini Tokyo Japan ,
Mei 21, 2014, akiwa katika ziara ya kikazi. Picha na OMR
JAPAN YAAHIDI KUENDELEA KUCHANGIA BAJETI YA TANZANIA
Mwandishi Maalum, Tokyo
Serikali ya Japan imeelezea
nia yake ya kuendelea kuchangia bajeti ya Tanzania na kufafanua kuwa, inafanya
hivyo kwa kutambua kuwa Tanzania ni mshirika mkubwa wa maendeleo na kwamba ni
nchi yenye kutia matumaini katika kupiga hatua za kimaendeleo.
Akizungumza jana katika
Ofisi yake jijini Tokyo, Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Japan Mheshimiwa
Yoshihide Suga alisema, serikali ya Japan inaifahamu Tanzania kama mshirika wa
maana katika maendeleo na kwamba inafahamu mchango wa Tanzania katika kuendeleza
ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki. Katibu Mkuu huyo pia aliongeza kuwa,
Tanzania imemudu kudumisha amani kwa kipindi kirefu huku ikipiga hatua za
kimaendeleo na kwamba watu wake wamebakia wamoja kwa miaka mingi licha ya kuwa
na tofauti za kitamaduni, kijiografia na kidini.
Kauli hiyo ya Katibu wa
Baraza la Mawaziri wa Japan, imetolewa kufuatia mkutano wake na Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ambaye yupo
jijini Tokyo kwa ziara ya kikazi. Katibu huyo alisema, “tunaifahamu Tanzania
kama nchi muhimu inayodumisha amani. Nchi yenu imeweza kudumisha Muungano kwa
miaka 50, Japan inawapongeza sana. Tunafahamu mnafanya kazi kubwa katika
kuwaendeleza wananchi wenu na sisi kama ndugu na rafiki zenu tuko tayari kabisa
kushirikiana nanyi.”
Katibu Mkuu Suga alieleza
pia kuwa, Tanzania ni nchi iliyo thabiti katika ukanda wa Afrika Mashariki na
inayo nguvu katika kuhakikisha ukanda huu unaendeleza utengamano hali ambayo
inachangia kuwepo maingiliano ya wananchi wa ukanda wa Afrika Mashariki
sambamba na kutanua fursa kwa wawekezaji kutoka nje ya Afrika.
“Mko thabiti katika mambo
mengi na hasa kuweza kumudu kuwa na amani na utulivu, mnategemewa sana na nchi
za Afrika Mashariki na kwa hali hii sisi tupo tayari kuendelea kutenga fedha
katika bajeti yetu kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya Tanzania katika
ushirikiano wa serikali na sekta binafsi (PPP),” alisema.
Kwa upande wake Mheshimiwa
Makamu wa Rais Dkt. Bilal alimueleza Katibu Mkuu Suga kuwa, Tanzania inapokea
kwa heshima kubwa mchango wa Japan kwa kutambua hali yake ya utulivu na kwamba
anatumia ziara yake Japan kuhamasisha wawekezaji kuja kuwekeza Tanzania.
“Tuna kazi kubwa mbele yetu
katika kuwaendeleza Watanzania. Hatuwezi kufanya kazi hiyo peke yetu, hivyo
basi nitumie nafasi hii kukuomba Mheshimiwa Katibu Mkuu kutusaidia kuhamasisha
wawekezaji kutoka Japan ili waje kushirikiana nasi katika kuiendeleza Tanzania.
Urafiki kati yenu na sisi ni wa siku nyingi na tungetegemea sasa tuubadili na
utazame fursa za kuchangiana kiuchumi na hasa katika kuwekeza kwa kubadilishana
teknolojia pamoja na mtaji,” Makamu wa Rais alisema.
Mheshimiwa Makamu wa Rais
yuko nchini Japan kwa ziara ya kikazi na tayari amefanikiw akukutana na wakuu
wa makampuni mbalimbali makubwa duniani yenye makao yake makuu nchini Japan na
kisha kutumia nafasi hiyo kuelezea fursa za uwekezaji nchini Tanzanja sambamba
na kubainisha umuhimu wa sekta binafsi kushiriki katika kusaidia maendeleo ya
nchi zinazoendelea zilizopo Afrika, Tanzania ikiwa ni kipaumbele.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇