LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 14, 2014

POLISI: HELKOPTA MARUFUKU KWENYE ANGA LA KALENGA SIKU YA UCHAGUZI, WALIOTUMWA KUFANYA VUJO KUKIONA

Kamanda Mungi akizungumza leo
Na Bashir Nkoromo, Iringa
JESHI la Polisi, limepiga marufuku chama chochote kurusha helkopta kwenye anga la jimbo la Kalenga, na limeahidi kushughulikia kikamilifu kundi au yeyote atakayejaribu kusababisha au kufanya vujo wakati wa uchaguzi na matokeo ya uchaguzi huo.

Onyo hilo limetolewa asubuhi hii na Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, wakati akieleza Polisi ilivyojiandaa kuhakikisha uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, unafanyika kwa amani na utulivu, Jumapili hii, ya Marchi 16, 2014.

Kamanda Mungi amesema, Intelijensia ya jeshi hilo, imeshawabaini watu ambao wameletwa na baadhi ya vyama vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huo, wakitokea mikoa mbalimbali kwa lengo la kufanya vurugu au kutisha wananchi wakati wa kupiga kura na kwamba ikiwa watathubutu kufanya vurugu watakiona cha moto.

"Tunafahamu na tunawajua watu walioletwa na baadhi ya vyama kwa lengo la kufanya vujo hapa Kalenga. Nawatahadharisha watu hao wajue kwamba wakijaribu kufanya vurugu, waliowaleta wataondoka halafu sisi tutabaki nao hapa Iringa kuhakikisha wanakiona cha moto", alisema kamanda wa Polisi.

Taarifa zaidi iliyotolewa na Kamanda Mungi hii hapa.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI JESHI LA POLISI TANZANIA
Ndugu waandishi wa habari , kwa niaba ya askari Polisi wa Mkoa wa Iringa, nitumie fursa hii kuwakaribisha hapa ofisini kwetu.

Ndugu zangu tumeitana hapa asubuhi hii ili niweze kuwapa taarifa ya usalama katika Mkoa wetu wa Iringa hususani katika Jimbo la Kalenga katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi wa Jimbo la Kalenga na usalama wa siku ya uchaguzi wenyewe.Ili iwe rahisi kueleweka taarifa hii nitaitoa kwa kifupi sana kwa kuigawa katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni juu ya wapi tunataka tupafikie  ( Where we want to go ), eneo la pili ni lile la wapi tulipo ( Where are we? ) na eneo la tatu ni jinsi gani tutafika huko ( How do we get there ). Tuanze    na  wapi   tunataka   tupafikie. Sisi  Polisi  Mkoa  wa  Iringa  tunataka  wananchi  wa  Kalenga  wapinge  kura  kwa  amani  na  utulivu  mkubwa   siku  ya   jumapili  tarehe  16/3/2014. Hii   ndio  dila  yetu  na  tutahakikisha  tunafika  hapo.

Kuhusu  wapi  tulipo  sasa, naomba   niwaelezeni  kwa  ufupi  sana  matukio  ya  kijinai  kuanzia  tarehe  19/02/14  mpaka   leo. Ndugu  zangu, kuanzia   tarehe  hiyo  mpaka  tarehe  2/03/2014  takribani  wiki  mbili  hakukuwa  na tukio  lolote  la  uvunjifu  wa  amani   lililokuwa  limepokelewa  katika  vituo  vyetu  vya  Polisi.  Hali  ilianza  kubadilika  tarehe  3/3/2014  ambapo  baadhi  ya  waandishi  walifika  ofisi  kwangu  na  kunieleza  kuwa  kumetoka  kwenye  mkutano  wa  CHADEMA  ambapo  wameelezwa  na  chama  hicho  kuwa   usiku  wa  siku  hiyo   walimkamata  mtu  mmoja  kwa  kosa  la   kujaribu  kuchoma  moto  nyumba  waliokuwa  wakiishi  wafuasi   wao  katika  kijiji cha  WASA. Waandishi  hao  walinitaka  nithibitishe  kutendeka   kwa  kosa  hilo  na  walieleza  kuwa  wameelezwa  kuwa  bado  halijaripotiwa  kituoni. Mimi  nilikataa  kusema  lolote  kuhusu   hilo  kwani   lilikuwa  bado  halijaripotiwa  Polisi. 

Tarehe  4/03/2014  nilifuatwa   tena  na  baadhi  ya  waandishi  na  kunieleza  kuwa  siku  hiyo  waliitwa  na  CCM   na  kuelezwa  kuwa  siku  ya  tarehe  27/2/2014  walitegewa  misumari  katika  kijiji  cha  WASA  ili  mabasi   yaliyokuwa  yamebeba   wafuasi  wao  yaweze  kutobolewa  magurudumu  yake, pia  nao  walisema  tukio  hilo  halijaripotiwa  Polisi. Mimi  nilikataa  kulizungumzia   swala  hilo.

Ndugu wanahabari,  vitendo   vilivyofanywa  na  vyama hivyo  vililenga  kuanzisha  propaganda  za   kisiasa   kwa   kutumia  uhalifu  kwa   kupitia  vyombo  vya   habari. Sisi   Polisi  tulibaini   hali  hiyo  na  ndiyo  sababu  tuliamua   kuwa  kimya  na  nyinyi  wenzetu  kwa  kuzingatia  maadili ya  kazi  zenu  pia   mlikaa  kimya.     Kuanzia  hapo  vyama vilianzisha   mashindano  ya   kuripoti  kesi  zao  Polisi. Leo hii  vyama  hivyo  vimeripoti  kesi  ishirini  na  moja   ambazo zilisababisha kukamatwa kwa wafuasi (19) wa vyama hivyo viwili.

Ndugu waandishi, kati ya kesi hizo ishirini na moja, kesi kumi na tisa (19) zile ambazo hazina madhara ya moja kwa moja kwa binadamu ama mali, kesi hizo ni  zile ndogondogo sana, kama vile kuchana mabango, kuteremsha bendera, kuchana vipeperushi, kutukanana n.k. kesi tatu zilikuwa zile zenye madhara kwa binadamu na mali ambazo ni kupigana hadharani, kujeruhi na kuharibu mali. Kati ya kesi ishirini na moja (21), kesi kumi upelelezi wake umekamilika na majalada yake yamefikishwa kwa mwanasheria wa serikali.
Ndugu waandishi, katika kesi hizo Polisi tumeibaini mengi mfano CHADEMA kilikuwa kikitoa malamiko kuwa tumeacha kumkamata ndugu hassan mtenga mtuhumiwa wa kesi moja iliyokuwa imefunguliwa dhidi yake.

Shutuma hizo hazina msingi kwani kesi iliyofunguliwa dhidi ya mtu huyo haikuwa ya jinai bali ya madai na tuliwajulisha hivyo. Nia ya kufanya hivyo ilikuwa kuifanya jamii iamini kuwa Polisi ni dhaifu na wenye kuonyesha upendeleo katika kushughulikia kesi za uchaguzi. Nashukuru Polisi tulikuwa watulivu, hatukujibu na jamii imetuelewa sana.

Ndugu waandishi, sijui mlijulishwa na nani kwamba Padri mmoja alifungwa kamba na alipingwa na kuburuzwa. Nanyi bila ya kuthibitisha kwetu mkaandika habari hiyo. Tuwaeleze kuwa mtu huyo ni miongoni mwa watuhumiwa tuliowakamata katika moja ya makosa yaliyotendeka, tulimhoji, aliandikwa maelezo yake na alipewa dhamana. Hata siku moja hajawahi kutoa taarifa Polisi juu ya matukio aliyotendewa. Nia ya kutangaza taarifa hiyo ni kuzua hofu kwa wananchi na kutaka kuchochea chuki kwa wafuasi wa dhehebu lake na wale wa dini yake.

Ndugu waandishi, pamoja na matukio hayo polisi tumekuwa tukipokea taarifa za vitisho vya kuwepo kwa watu mbalimbali kutoka kwa vyama vyote walioingizwa mkoani humu kwa nia ya kutenda vitendo vya uvunjifu wa amani.

Aidha, tumewasikia viongozi wa vyama wakitamba kuingiza maelfu ya watu mkoani mwetu. Kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Mbeya kwa visingizio vya kulinda kura.

Sasa nataka niwaeleze kuwa sheria iko wazi kabisa, kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na wakala wa chama kinachoshiriki katika uchaguzi huo na hao ndio wawakilishi wa chama hicho na walinzi halali wa uchaguzi ni askari wa Jeshi la Polisi. Kufuatia hali hiyo mambo yafuatayo yanasisistizwa sana.

Hatutaki kuona walinzi wa chama  chochote  katika Jimbo la Kalenga. Jukumu la kulinda uchaguzi, maisha na mali ya wana Kalenga ni la JESHI LA POLISI.

Hatutaki kuona watu wasiokuwa na shughuli maalumu wanapitapita katika maeneo ya kupigia kura.
Siku ya uchaguzi si siku ya kampeni. Hatutaki kuona helikopita za  vyama  vyote  zenye kuashiria kufanya kampeni. 

Nawaasa watu wote hasa wale waliotoka nje ya Iringa, sisi huku Iringa tunapenda sana amani kuliko kitu chochote kile hivyo ikiwa wameletwa kama MAJESHI YA KUKODIWA ili kuharibu amani ya Kalenga kama walivyozoea kufanya huko walikotoka, Sisi Polisi na wana Kalenga tupo imara, tumejipanga vizuri kukabiliana nao.

Aidha, napenda kuwatoa hofu wana kalenga, wasiwe na wasiwasi kabisa, sisi Polisi Iringa tupo imara na tumejipanga vizuri katika kuwalinda kikamilifu. Nawaomba wajitokeze kwa wingi sana siku ya kupiga kura na wapige kura zao kwa uhuru kabisa.
Ndugu waandishi, nawashukuru sana kwa jinsi mlivyofanya kazi zenu kwa ueledi mkubwa. Hata siku moja hatujawahi kusikia ama kusoma habari za uchochezi kwa kushabikia chama chochote kile.
 AHSANTENI SANA.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages