Na Mwandishi Maalum, New York
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema, posho ya dola 1.28 kwa siku wanayolipwa walinzi wa amani wanaohudumu katika Misheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, hailingani na mazingira magumu na hatari ya utekelezaji wa mamlaka wanayokabidhiwa na Umoja wa Mataifa.
Na kwa sababu hiyo ,na kwa zingatia hali halisi, Tanzania imesisiza kwamba, wakati umefika sasa wa kuangalia upya posho hiyo ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 20.
Balozi Tuvako Manongi, Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa mataifa, ametoa rai hiyo mwanzo mwa mkutano wa Kamati Maalum ya Usimamizi wa Operesheni za Ulinzi wa Amani maarufu kama C-34.
Kamati hii ambayo wajumbe wake ni kutoka nchi zinazochangia walinzi wa Amani katika misheni mbalimbali za kulinda amani, imeanza mkutano wake wa mwezi mmoja hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo wajumbe watajadili mambo yote yanayohusu sera za ulinzi wa Amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Balozi Manongi amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba Kamati ilikuwa inaanza mkutano wake, wakati ambapo , operesheni za ulinzi wa amani zinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za malipo duni.
“ Tunaposhindwa kukubaliana kujadili hoja ya kuongeza kiwango cha posho ya kila siku kwa walinzi wa amani, posho ambayo imebaki dola 1.28 kwa zaidi ya miaka 20, siyo tu kwamba tumewaangusha walinzi wa amani, bali pia tunawavunja moyo na kuwakatisha tamaa katika utekelezaji wa majukumu yao”. akasisitiza Balozi Manongi.
Akasema waeleza wajumbe licha ya malipo duni na mazingira magumu, walinzi hao wanajitolea uhai wao kwaajili ya watu wengine na kwamba,kutokana umuhimu wao , Umoja wa Mataifa umejikuta ukilazimika kuwapeleka katika Misheni ambazo ama hakuna amani ya kulinda au mahali ambako kuna vikundi vingi vyenye silaha vinavyokinzana.
“Hii ndiyo hali halisi inayozikabili Misheni zetu zote katika utekelezi wa mamlaka tunazokabidhiwa na Umoja wa Mataifa. Inasikitisha na kukatisha tamaa pale baadhi yetu tunaposisitiza kwamba Misheni mpya inayoundwa au kuongezewa mamlaka itekeleze mamlaka hayo kwa kuzingatia rasilimali zilizopo, ili hali tunafahamu wazi kwamba rasilimali zinazozungumzwa ama hazipo au hazikidhi hali halisi ya Misheni hizo”. Akabainisha Balozi Manongi.
Na kuongeza. “Ni vema tukaunganisha nguvu zetu kukabiliana na changamoto hizi na nyingine nyingi ili walinzi wa amani ambao wanategemewa sana waweze kusaidia katika ulinzi wa amani kwa raia wasiokuwa na hatia, lakini pia kujihakikishia usalama wao wenyewe.
Akaeleza kwamba ni matumaini ya Tanzania kuwa hoja ya kuongezwa kwa posho hiyo pamoja na nyongeza ya malipo ya vifaa itapewa umuhimu na kujadiliwa ipasavyo katika mkutano ujao wa Kamati ya Tano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya Utawala na Bajeti ya Umoja wa Mataifa.
Pamoja na changamoto hizo, Muwakilishi huyo wa Tanzania, ameuhakikishia Umoja wa Mataifa kwamba, Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuwajibika kwa kushiriki katika operesheni za ulinzi wa Amani kwa mujibu wa Mamlaka inayokabidhiwa na Umoja wa Mataifa.
“ Tumedhamiria na tunajivunia ushiriki wetu wa ulinzi wa Amani katika maeneo mbalimbali ikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambako tunashiriki kupitia Misheni ya Kulinda Amani katika DRC ( MONUSCO). Misheni ambayo ndani yake kuna Force Intervention Brigade ( FIB)”.
Vile vile akabainisha kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Mpango Mpana wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa, kuhusu Ulinzi, Usalama na Ushirikiano wa Ki- maendeleo katika DRC na eneo la Maziwa Makuu.
Akizungumzia zaidi kuhusu Misheni ya MONUSCO na mchango wake katika usimamizi wa amani katika DRC.
Balozi Tuvako Manongi amesema, Tanzania inaamini kwamba utendaji kazi wa Misheni hiyo unasimama katika misingi ya Misheni Moja, Jeshi Moja, Nguvu Moja ya Mamlaka, kuwa ndiyo mweleko sahihi na wenye tija katika ngazi zote kiutendaji.
Misheni ya MONUSCO inaundwa na walinzi wa Amani kwa upande mmoja kutoka Pakistani, India na Bangladeshi pamoja na Tanzania, Afrika ya Kusini na Malawi kupitia FIB.
Aidha, Muwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amezitaka Mamlaka za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kutumia mafanikio yaliyopatikana hivi karibuni, kuimarisha taasisi zake za kisiasa, kiulinzi , kiuchumi pamoja na kuongeza kasi ya majadiliano na maridhiano. Baadhi ya Waambata wa Kijeshi wanaoziwakilisha nchi zao Katika Umoja wa
Mataifa, wakiwa katika picha ya pamoja muda mfupi kabla ya ufunguzi
wa Mkutano wa Mwezi mmoja wa Kamati Maalum ya Usimamizi wa Operesheni za
Kulinda Amani. Katika Mkutano huu wajumbe ambazo ni kutoka nchi
ambazo zinachangia walinzi wa amani watajadili sera zote zinazohusu
ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa.
Your Ad Spot
Feb 25, 2014
Home
Unlabelled
TANZANIA YASISITIZA NYONGEZA YA POSHO KWA WALINZI WA AMANI WA UMOJA WA MATAIFA
TANZANIA YASISITIZA NYONGEZA YA POSHO KWA WALINZI WA AMANI WA UMOJA WA MATAIFA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇